Tafuta

Vatican News
Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu wanaendelea kusoma alama za nyakati ili kusikiliza na kujibu kilio cha maskini katika ulimwengu mamboleo! Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu wanaendelea kusoma alama za nyakati ili kusikiliza na kujibu kilio cha maskini katika ulimwengu mamboleo!  (Vatican Media)

Askofu mkuu Rugambwa: Ujumbe kwa Shirika la Roho Mtakatifu!

Maadhimisho ya Pentekoste kwa Mwaka 2019 yamekuwa ni chachu mpya katika maisha na utume wao. Huu ni wakati wa kuweka divai mpya katika viriba vipya na kuendelea kusoma alama za nyakati ili kusikiliza na kujibu kilio cha maskini katika ulimwengu mamboleo. Hawa ndio wale wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na kwenye mifumo ya utumwa mamboleo.!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wamisionari Roho Mtakatifu, ni Shirika lililoanzishwa na Padre Claude Poullart des Places, huko Ufaransa, tarehe 27 Mei 1703 katika Sherehe ya Pentekoste, yaani miaka 316 iliyopita na miaka 151 ya uwepo na huduma yao nchini Tanzania. Hiki kilikuwa ni kikundi cha Waseminari waliojiaminisha na kujiweka wakfu chini ya ulinzi na tunza ya Roho Mtakatifu na kwa msaada wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ili kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili huduma kwa Kanisa, hususan katika maeneo na mazingira tete na hatarishi. Ni Wamisionari wanaokita utume wao katika mchakato wa uinjishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Wamisionari wa Roho Mtakatifu wamekuwa mstari wa mbele katika huduma ya elimu makini Barani Afrika; huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; pamoja na kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu wa Mataifa, ili hatimaye, dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Maadhimisho ya Pentekoste kwa Mwaka 2019 yamekuwa ni chachu mpya katika maisha na utume wao. Huu ni wakati wa kuweka divai mpya katika viriba vipya na kuendelea kusoma alama za nyakati ili kusikiliza na kujibu kilio cha maskini katika ulimwengu mamboleo.

Hawa ndio wale wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; ni wasichana, wanawake na watoto wanaosukumiziwa kwenye mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo kama vile: utalii wa ngono; athari za mabadiliko ya tabianchi zinazopelekea wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Changamoto za utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yanaendelea kumong’onyoa na kusigina tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, changamoto kwa wanandoa na familia kusimama kidete, ili kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya familia inayosimikwa katika Injili ya uhai na huduma!

Changamoto, matatizo na fursa zote hizi zinahitaji sera na mikakati makini ya shughuli za kichungaji, kwa kukazia elimu bora, malezi na majiundo endelevu, katekesi makini sanjari na majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi! Shirika la Wamisionari wa Roho Mtakatifu linaendelea kuwekeza katika malezi na majiundo makini ya wamisionari wake, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa: haki, amani na upatanisho; umoja na mshikamano wa kweli unaosimikwa katika tofauti ambazo ni amana na utajiri katika maisha na utume wa Kanisa!

Huu ni ushuhuda unaobubujika kutoka katika tunu msingi za Kiinjili, utu, heshima na haki msingi za binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza. Umefika wakati kwa wamisionari wazalendo kujifunza kujisadaka kwa kujitoa na kujimega zaidi kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa uinjilishaji mpya ndani na nje ya Bara la Afrika! Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, tarehe 9 Juni 2019 ameadhimisha Sherehe ya Pentekoste kwa jumuiya na Wamisionari wa Roho Mtakatifu, kwenye Kikanisa cha Watawa Wamisionari wa Comboni, mjini Roma, kama kumbu kumbu ya kuanzishwa kwa Shirika na Padre Claude Poullart des Places, huko Ufaransa kunako mwaka 1703. Shirika limeenea katika nchi 62 zinazohudumiwa na Wamisionari zaidi ya 2, 600.

Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Protase Rugambwa, amewataka Wamisionari wa Roho Mtakatifu kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Roho Mtakatifu, Roho wa kweli, Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu anayeongoza na kulitakatifuza Kanisa. Wamisionari wa Roho Mtakatifu wawe ni mashuhuda na vyombo vya Kristo Mfufuka anayeendelea kupyaisha Kanisa lake kwa nguvu ya Neno, Sakramenti na Mafumbo ya Kanisa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kama ilivyokuwa kwa Mitume na Wakristo wa Kanisa la mwanzo. Nguvu ya Roho Mtakatifu iwasukume waamini kutoka kifua mbele ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Ni wakati wa kusimama kidete kupambana na ukosefu wa haki msingi za binadamu; mmong’onyoko wa kanuni maadili na utu wema pamoja na kuendeleza mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Roho Mtakatifu awawezeshe waamini kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa ili liendeelee kuwa ni: Kanisa moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume! Askofu mkuu Protase Rugambwa anakaza kusema, huu ni umoja unaofumbatwa katika utofauti. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa ni Sakramenti ya umoja unaopata utimilifu wake ndani ya Kristo Yesu.

Hii ni changamoto kwa waamini wote kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari; kwa kubaki thabiti kwa Roho Mtakatifu na kuzama zaidi katika kukuza na kudumisha moyo wa ukarimu. Waamini wawe na ujasiri wa kumruhusu Roho Mtakatifu aweze kuwaangaza, kuwaongoza na kuwaelekeza, kadiri ya mapenzi yake. Askofu mkuu Protase Rugambwa amekumbusha kwamba, Mwezi Oktoba 2019 Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Ni muda wa: sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma! Ni wakati kwa waamini walei kutambua haki, dhamana na wajibu wao katika maisha na utume kwa Kanisa.

Hii ni fursa ya kuwahimiza waamini kujiwekea sera na mikakati ya kuyategemeza Makanisa mahalia: kwa njia ya rasilimali watu, vitu na fedha, ili Kanisa liendelee kutangaza Injili ya huruma na upendo hadi miisho ya dunia! Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa”.  Kanisa linaendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake. Hiki ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni muda wa kutangaza furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa; Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ari na ushiriki mkamilifu na hatimaye, Kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Askofu Mkuu Rugambwa
15 June 2019, 15:42