Tafuta

Vatican News
Chuo Kikuu cha Kikatoliki: Kiwe ni mahali muafaka pa malezi na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya; kwa kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari Chuo Kikuu cha Kikatoliki: Kiwe ni mahali muafaka pa malezi na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya; kwa kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari 

Chuo Kikuu cha Kikatoliki: Malezi na Makuzi ya Vijana!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Chuo hiki kitaendelea kuwa ni mahali muafaka pa malezi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya na jukwaa la majadiliano kati ya imani na maswali yanayoendelea kuibuliwa katika ulimwengu mamboleo! Maadhimisho ya Mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu “Shauku, Karama, Uwajibikaji. Nikitafuta nafasi yangu ulimwenguni”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa Katoliki Nchini Italia, Jumapili tarehe 5 Mei 2019 limeadhimisha Siku ya 95 ya Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” yaani “Moyo Mtakatifu wa Yesu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Chuo hiki kitaendelea kuwa ni mahali muafaka pa malezi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya na jukwaa la majadiliano kati ya imani na maswali yanayoendelea kuibuliwa katika ulimwengu mamboleo! Maadhimisho ya Mwaka huu yameongozwa na kauli mbiu “Shauku, Karama, Uwajibikaji. Nikitafuta nafasi yangu ulimwenguni”.

Katika maadhimisho haya, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amemwandikia ujumbe Askofu mkuu Mario Enrico Delpini wa Jimbo kuu la Milano, Italia ambaye pia ni Rais wa Taasisi ya Giuseppe Toniolo. Katika ujumbe huu, Kardinali Parolin anakazia umuhimu wa majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya, uinjilishaji unaofumbatwa katika majadiliano na umuhimu wa tunu msingi za maisha ya kiroho miongoni mwa wanafunzi wanaopata elimu kutoka chuoni hapo! Kardinali Parolin anasema, katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, 2018 iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”, Kanisa limeweza kugusa matatizo, changamoto na fursa zilizoko miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Tema ya malezi na majiundo makini ni kati ya mambo yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na vijana kuomba kusindikizwa katika hija ya maisha yao hapa duniani, ili kukuwa na kukomaa: kiutu, kitamaduni na katika maisha ya kiroho! Huu ni utume unaoweza kutekelezwa kwa ufasaha zaidi katika taasisi ya elimu kama hii. Mababa wa Sinodi walikazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa kupyaisha utume wa Kanisa katika shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, kwa kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayofumbatwa katika majadiliano yanayotekelezwa kwenye ngazi mbali mbali.

Kumbe, kuna haja ya kukazia mchakato wa utamaduni wa watu kukutana, ili kujenga mtandao utakaotoa kipaumbele kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mafanikio haya yanaweza kufikiwa ikiwa kama kutakuwepo na uwiano mzuri wa maarifa yaliyoko kichwani, moyoni na yanayotekelezwa. Chuo hiki Kikuu cha Kikatoliki, kilianzishwa ili kujibu hitaji la mahali pa malezi na majiundo makini ya vijana nchini Italia, changamoto iliyovaliwa njuga na Padre Agostino Gemelli na wasaidizi wake wa karibu. Matokeo, katika kipindi cha miaka 95 Chuo hiki kimeendelea kukua na kupanuka na hatimaye, kuwa ni jukwaa la malezi na majiundo ya kielimu kitaifa na kimataifa!

Haya ni matokeo ya sadaka kubwa ya akili na ukarimu inayotekelezwa na wadau wa Jumuiya ya Chuo Kikuu, bila kusahau kwamba, wanafunzi wana imani na wanathamini sana mchango huu. Kumbe, kuna haja ya kukazia ari na mwamko wa kimisionari, tayari kutoka na kuanza kufanya tafiti za ukweli, ustawi na maendeleo ya wengi. Chuo kiwe ni mfano bora wa kuigwa katika ukarimu, huduma makini kwa wanafunzi, kwa kutafuta na kuambata mafao ya wengi, sanjari na kupambana na changamoto mamboleo kuhusu: utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; mifumo mbali mbali ya ubaguzi, ukosefu wa haki pamoja baa la umaskini duniani!

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, kauli mbiu “Shauku, Karama, Uwajibikaji. Nikitafuta nafasi yangu ulimwenguni” ni changamoto inayowataka kuwaangalia vijana wa kizazi kipya kuwa ni wadau muhimu sana kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Chuo kikuu kiwaundie wanafunzi mazingira ya kuthubutu katika masuala ya kazi, shughuli za kitamaduni na kichungaji kwa ajili ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Vijana watambue kwamba, katika hija hii ya maisha, wanasindikizwa na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake, ili kuwakirimia nguvu na matumaini ya kusonga mbele.

Kardinali Parolin, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuipongeza Jumuiya ya Chuo Kikuu cha “Sacro Cuore” kwa kazi kubwa wanayoifanya. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, mchango mkubwa uliobainishwa na Mababa wa Sinodi ya Vijana kwa mwaka 2018 utaweza kutoa msukumo mpya wa utume wa taasisi za Kikatoliki nchini Italia kwa kuwasaidia vijana. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa taasisi hii na kuwaomba pia wamkumbuke katika maisha na utume wake!

Parolin: Chuo Kikuu
06 May 2019, 11:42