Cerca

Vatican News
Askofu mkuu Tymon Tytus Chmielecki amewekwa wakfu ili aweze kuwa ni chombo cha haki na majadiliano Barani Afrika! Askofu mkuu Tymon Tytus Chmielecki amewekwa wakfu ili aweze kuwa ni chombo cha haki na majadiliano Barani Afrika! 

Askofu mkuu Tymon Chmielecki: Chombo cha amani na majadiliano!

Askofu mkuu Tymon Tytus Chmielecki alizaliwa Mwaka 1965, Poland. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 26 Mei 1991. Askofu mkuu Tymon Tytus Chmielecki, ana shahada ya Sheria za Nchi na Sayansi ya Binadamu. Askofu mkuu Tymon Tytus Chmielecki ameteuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Guinea na Mali, Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Fatima, tarehe 13 Mei 2019, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, amemweka wakfu Monsinyo Tymon Tytus Chmielecki kuwa Askofu mkuu, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kardinali Parolin, katika mahubiri yake, amekazia kuhusu: Ushuhuda wa Askofu kama kielelezo cha uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake; anatumwa kwenda Barani Afrika kama shuhuda na chombo cha haki, amani na majadiliano na kwamba, atapaswa kuwa ni mjenzi wa umoja na mshikamano kati ya Makanisa mahalia na Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Kardinali Parolin, amemtaka Askofu mkuu Tymon Tytus Chmielecki kuiga mfano wa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, anapotekeleza dhamana na utume wake wa: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, kadiri ya Mapokeo ya Kitume. Askofu awe ni chombo na shuhuda wa furaha ya Injili; umoja na mshikamano wa watu wa Mungu; majitoleo na sadaka katika huduma ya upendo, hadi tone la mwisho katika maisha. Askofu mkuu Tymon Tytus katika maisha na utume wake kama Askofu mkuu anaongozwa na kauli mbiu “Eskatos kai diakonos” yaani “Wa mwisho na Mtumishi” sehemu ya Injili ya Marko 9: 35. “Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote”.

Huu ni ushuhuda na utambuzi makini kutoka kwa Askofu mkuu Tymon Tytus kwamba, ameteuliwa kumwalikisha Khalifa wa Mtakatifu Petro, zawadi na utume unaomwezesha kuwa chombo cha huduma ya kichungaji kwa ajili ya Makanisa mahalia. Atakuwa ni chombo kitakachoisaidia Vatican kutambua hali halisi ya Makanisa mahalia; furaha, mahangaiko na matamanio yao halali; mafanikio na changamoto katika maisha na utume wa Makanisa haya. Kama Askofu mkuu, atakuwa ni shuhuda na alama hai ya uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake, kama kielelezo cha huruma na upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu.

Upendo wa Mungu uwe ni chachu ya kuwaendea maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; upendo wa Mungu umsaidie kutambua kwamba, uongozi ni huduma na kwamba, ameitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, kiasi hata cha kuweza kujisadaka na kutosa bila ya kujibakiza, hata ikibidi, kumwaga damu kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Asaidie kukuza na kuimarisha imani ya waamini kwa njia ya Neno, Sakramenti za Kanisa na ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Askofu mkuu Tymon Tytus anatumwa Barani Afrika kama chombo cha haki, amani na majadiliano; mambo yanayobubujika kutoka katika uzoefu na mang’amuzi ya maisha na utume wake kama Padre tangu mwaka 1991 alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre na kuanzia mwaka 1995 alipoanza utume wa diplomasia ya Kanisa. Askofu mkuu Tymon Tytus anatumwa katika nchi ambazo wananchi wake wengi ni waamini wa dini ya Kiislam, changamoto na mwaliko wa kukuza na kudumisha: haki, amani na maridhiano kati ya watu kwa kukuza majadiliano ya kidini. Hii ina maana kwamba, mchakato mzima wa uinjilishaji unafumbatwa katika upatanisho sanjari na kuimarisha mifumo ya demokrasia.

Tofauti msingi za kidini na kiimani, uwe ni utajiri na amana dhidi ya misimamo mikali ya kidini na kiimani; chuki na uhasama kwa misingi ya udini. Watu watambue kwamba, Mwenyezi Mungu ni chemchemi na asili ya umoja, upendo na udugu na kamwe hawezi kuwa ni chanzo cha: vita, mauaji na vitendo vya kigaidi. Waamini wana wajibu wa kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni vyombo vya haki, amani na maridhiano, kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu. Waamini walinde na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwa uchafuzi wa mazingira ni kielelezo pia cha kumong’onyoka kwa utamaduni, kanuni maadili na utu wema!

Kardinali Parolin amemkumbusha Askofu mkuu Tymon Tytus Chmielecki kwamba, anatumwa nchini Guinea na Mali kama Balozi wa Vatican na mjenzi wa umoja na mshikamano. Ni wajibu wake msingi, kusimama kidete kulinda na kutetea: utu, heshima na haki msingi za binadamu na hasa zaidi za maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Uwepo wa Mabalozi wa Vatican katika nchi mbali mbali duniani ni kuiwezesha Vatican kushiriki kikamilifu katika uchungu na fadhaa; furaha na matumaini ya watu wa Mungu kutoka katika nchi hizi.

Mwishoni mwa mahubiri yake, Kardinali Pietro Parolin amemwombea Askofu mkuu Tymon Tytus Chmielecki kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, ili aweze kuwa ni mlinzi na msimamizi wake katika mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa dhati; Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili pamoja na kuendeleza Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Watakatifu Stansilaus, Timone na Tito, wawe wasimamizi wake katika hija ya maisha na utume wake Barani Afrika.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Tymon Tytus Chmielecki, aliteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Guinea na Mali. Askofu mkuu Tymon Tytus Chmielecki kabla ya uteuzi huu, alikuwa ni Mshauri wa Ubalozi wa Vatican. Alizaliwa kunako tarehe 29 Novemba 1965, Torun, Poland. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 26 Mei 1991. Askofu mkuu Tymon Tytus Chmielecki, ana shahada ya Sheria za Nchi na Sayansi ya Binadamu.

Askofu mkuu Tymon Tytus Chmielecki, alianza utume wake katika diplomasia ya Vatican kunako tarehe 1 Julai 1995. Tangu wakati huo, amebahatika kutekeleza dhamana na utume wake katika Balozi za Vatican nchini Georgia, Senegal, Austria, Ucrain, Kazakhstan, Brazil na hatimaye, alipangiwa utume kwenye Idara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Sekretarieti kuu ya Vatican.

Kardinali Parolin: Balozi
14 May 2019, 15:59