Tafuta

Kardinali Filoni: Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba, Makatekista na Upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa kwa kukumbatia toba, wongofu na utakatifu wa maisha Kardinali Filoni: Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba, Makatekista na Upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa kwa kukumbatia toba, wongofu na utakatifu wa maisha 

Kardinali Filoni: Mpango mkakati, Makatekista, Upyaisho wa Kanisa

Kardinali Fernando Filoni katika hotuba yake kwenye mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa amekazia umuhimu wa uteuzi na majiundo makini kwa makatekista; utekelezaji wa mbinu mkakati wa mwezi Oktoba 2019; Ushirikiano kati ya Maaskofu mahalia na mihimili ya Uinjilishaji pamoja na kutambua umuhimu wa madhabahu katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maandalizi ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa”, Maandalizi ya Kongamano la Kimisionari Amerika ya Kusini, CAM5; Umuhimu wa kutandaza msingi wa kitaalimungu katika sera na mikakati ya shughuli za kimisionari ni kati ya mambo ambayo yamejadiliwa kwenye mkutano wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, unaoendelea hapa mjini Roma hadi tarehe 1 Juni 2019. Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika hotuba yake, amekazia kuhusu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019; Umuhimu wa majiundo makini na endelevu kwa Makatekista pamoja na kuendeleza mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia na kuambata utakatifu wa maisha; mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko.

Mwezi Oktoba 2019 Kanisa litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume"Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Papa Benedikto XV katika Waraka huu, alifungua rasmi ukurasa mpya wa maisha na utume wa Kanisa mintarafu shughuli za kimisionari, kwa kulitaka Kanisa kuanzisha mchakato wa majiundo na malezi kwa ajili ya kuyategemeza Makanisa mahalia kwa rasilimali watu, yaani wahudumu wa Injili! Kardinali Filoni anasema, Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika utume”. 

Kanisa linataka kuendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake. Maadhimisho haya ni muda wa: sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma! Ni wakati kwa waamini walei kutambua haki, dhamana na wajibu wao katika maisha na utume kwa Kanisa. Hii ni fursa ya kuwahimiza waamini kujiwekea sera na mikakati ya kuyategemeza Makanisa mahalia: kwa njia ya rasilimali watu, vitu na fedha, ili Kanisa liendelee kutangaza Injili ya huruma na upendo hadi miisho ya dunia!  Uinjilishaji unafumbatwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Makatekista ni kati ya mihimili ya uinjilishaji hasa katika maeneo ya vijijini na mahali ambapo bado kuna uhaba wa wakleri.

Makatekista wamekuwa ni wahudumu wa Neno, wahamasishaji wa maisha ya sala na huduma ya upendo. Makatekista ni viongozi waliokabidhiwa jukumu la kutoa katekesi kwa waamini wanaojiandaa kupokea Sakramenti mbali mbali za Kanisa ni vyombo na mashuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, waamini wanavumbua njia mpya za kuwa Makatekista, ili kuendeleza ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Majiundo awali na endelevu ni muhimu kwa Makatekista ili kuwawezesha kutekeleza vyema dhamana na utume wao ndani ya Kanisa. Uteuzi wa Makatekista ufanywe kwa uangalifu mkubwa; wapewe mahitaji yao msingi kwa kutambua kwamba, hawa ni wasaidizi wakuu katika mchakato wa uinjilishaji katika maeneo ambayo wamekabidhiwa na Mama Kanisa!

Kardinali Filoni amewataka Maaskofu na Mapadre kwenye Makanisa mahalia kushirikiana na kushikamana kwa dhati katika malezi na majiundo ya Makatekista; kwa kusoma alama za nyakati na kuangalia mahitaji ya Makanisa mahalia. Kutokana na changamoto mamboleo, kuna haja ya kuibua mbinu mpya ya kusali, kuragibisha utafutaji wa fedha kwa ajili ya kuchangia maisha na utume wa Kanisa kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”. Papa Francisko anawakumbusha Wakristo wote kwamba, wao ni wafuasi wamisionari, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kuwashirikisha wengine huruma na upendo wa Mungu unaookoa.

Kila Mkristo ni mmisionari mahali alipo, changamoto ni kuelekea katika ukomavu wa kiimani unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kardinali Filoni amegusia muhimu wa Madhabahu kuwa ni mahali ambapo panapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, Amri za Mungu, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi. Ni mahali pa shuhuda za imani, matumaini na mapendo, kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima! Madhabahu ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu. Maeneo kama haya yanahitaji wakleri waliofundwa barabara, watakatifu, vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Kard. Filoni
30 May 2019, 16:48