Cerca

Vatican News
Papa Francisko: Watoto wenye ulemavu ni zawadi kwa familia, fursa ya kukua katika upendo, umoja na mshikamano, kwa kutambua na kuthamini haki zao msingi! Papa Francisko: Watoto wenye ulemavu ni zawadi kwa familia, fursa ya kukua katika upendo, umoja na mshikamano, kwa kutambua na kuthamini haki zao msingi! 

Papa Francisko: Watoto wenye ulemavu ni zawadi: Upendo na Umoja!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, watu wenye ulemavu ni zawadi kwa familia na fursa ya kukua katika upendo, umoja na mshikamano pamoja na kutambua haki zao msingi kama binadamu, Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika tiba kwa magonjwa ya watoto, hata wale ambao bado hawajazaliwa. Waamini wakate kabisa kishawishi cha utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, ambao ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa familia anawaalika wanafamilia  kushughulikia changamoto ya ulemavu wa watoto wao kwa imani, mapendo na matumaini makuu; ushuhuda unaopaswa kuungwa mkono ili kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Watu wenye ulemavu ni zawadi kwa familia na fursa ya kukua katika upendo, umoja na mshikamano pamoja na kutambua haki zao msingi kama binadamu. Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika tiba kwa magonjwa ya watoto, hata wale ambao bado hawajazaliwa.

Tiba hizi wakati mwingine zimekuwa ni changamoto kubwa katika shughuli za kichungaji mintarafu kanuni maadili na utu wema bila kusahau mafundisho ya Kanisa kuhusu Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, kuanzia tarehe 23-25 Mei 2019 linaendesha mkutano wa kimataifa unaoongozwa na kauli mbiu “ Yes to life! Utunzaji wa zawadi ya uhai katika hali zake tete”. Mkutano huu unawajumuisha wajumbe 400, wawakilishi kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki katika nchi 70, wanafamilia, madaktari pamoja na wataalam bingwa katika huduma ya tiba kwa watoto wachanga.

Lengo la mkutano huu ni kutaka kukazia utambuzi kwamba, hata katika hali yake tete kutokana na magonjwa mbali mbali, uhai daima utaendelea kuwa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, chemchemi ya kukua na kustawisha upendo, kwa kusaidiana pamoja na kujenga umoja na mshikamano wa kifamilia! Wanandoa wengi wanapofunga pingu za maisha wanatamani sana kupata watoto kama zawadi ya umoja na upendo wao. Wakati mwingine wanandoa wanakabiliwa na changamoto kubwa inayohitaji maamuzi magumu, ili kuweza kupokea zawadi ya mtoto ambaye ana ulemavu, badala ya kufumbata utamaduni wa kifo unaojikita katika sera za utoaji mimba. Maendeleo makubwa ya sayansi ya tiba kwa watoto wadogo, yamewezesha familia nyingi kupata msaada unaohitajika.

Mama Kanisa anawaalika viongozi wa Kanisa wanaojihusisha na shughuli za kichungaji, hususan utume wa familia, kuwa karibu zaidi na familia zinazokabiliwa na changamoto za namna hii, ili kuwapatia faraja katika maisha yao ya kiroho. Kwa wazazi ambao wana watoto wenye ulemavu, hapa panakua ni mahali ambapo sayansi ya tiba ya magonjwa ya mwanadamu inasaidia na imani katika matendo, ili kuweza kuwasindikiza wanandoa hawa kuupokea ukweli kama ulivyo kwa imani na upendo mkuu! Wahamasishaji katika mkutano huu wa kimataifa wanapenda kukazia pamoja na mambo mengine: umoja na mshikamano wa upendo katika huduma kwa watoto wenye ulemavu; ushuhuda wa imani kwa watoto wanaozaliwa na ulemavu; huduma ya upendo pamoja na kuondokana na kishawishi cha kutaka kuchagua watoto hata wakingali bado tumboni mwa mama zao.

Ni vyema, ikiwa zawadi ya uhai, itasindikizwa hatua kwa hatua pamoja na kuendelea kushirikishana uzoefu na mang’amuzi ya ulinzi na tunza ya watoto wenye mahitaji ya pekee ndani ya familia. Mama Kanisa anasema, hata wahudumu katika sekta ya afya wanapaswa kusaidiwa ili kukabiliana na changamoto za maisha na utume wao. Watoto wenye ulemavu wanahitaji  huduma ya tiba inayozingatia kanuni maadili na utu wema. Wajumbe wa mkutano huu wa kimataifa unaoongozwa na kauli mbiu “ Yes to life! Utunzaji wa zawadi ya uhai katika hali zake tete”, Jumamosi, wanatarajiwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko!

Papa: watoto Walemavu
22 May 2019, 15:32