Tafuta

Vatican News
Urithi kutoka kwa Mtakatifu Rita wa Cascia: Wito wa utakatifu wa maisha; Toba, msamaha na wongofu wa ndani pamoja na kuupenda Msalaba! Urithi kutoka kwa Mtakatifu Rita wa Cascia: Wito wa utakatifu wa maisha; Toba, msamaha na wongofu wa ndani pamoja na kuupenda Msalaba! 

Mtakatifu Rita wa Cascia: Utakatifu; Msamaha & Kupenda Msalaba!

Urithi wa Mtakatifu Rita wa Cascia: Wito wa utakatifu wa maisha kwa Wakristo wote; umuhimu wa kusamehe na kusahau pamoja na kupenda Msalaba, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa: Hekima, huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Mtakatifu Rita wa Cascia anakumbukwa na wengi kama mwombezi wa mambo yaliyoshindikana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 22 Mei, Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Rita wa Cascia aliyezaliwa kunako mwaka 1381 huko Roccaporena. Akafariki dunia tarehe 22 Mei 1457 na kutangazwa kuwa Mtakatifu hapo tarehe 24 Mei 1900 na Baba Mtakatifu Leo XIII. Ni mwanamke wa shoka, aliyeweza kuvumilia ndoa shuruti kwa muda wa miaka 18, akiwa anamwombea mumewe ili aweze kutubu na kuongoka! Katika kumbu kumbu ya miaka 18 ya ndoa yao, mumewe akauwawa kikatili katika ugomvi! Kifo hiki kiliacha machungu katika familia ya Mtakatifu, ambaye, watoto wake walitaka kulipiza kisasi, ili “kumwonesha cha mtema kuni” yule aliyesababisha kifo cha baba yao!

Mawazo haya yakeleta majonzi makubwa tena katika maisha ya Mtakatifu Rita wa Cascia, akawaombea watoto wake ili wasilipize kisasi, akafanikiwa na watoto hawa wakawa ni mashuhuda wa huruma na msamaha katika maisha yao, kiasi hata cha kuitupa mkono dunia wakiwa katika hali ya neema! Katika hali ya upweke na majonzi makuu, Rita wa Cascia akajiunga na maisha ya kitawa, akawa kweli ni chemchemi ya huruma na upendo kwa jirani pamoja na watawa wenzake. Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, Jumatano, tarehe 22 Mei 2019 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Rita wa Cascia, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Rita wa Cascia huko mjini Cascia, nchini Italia.

Kardinali Becciu katika mahubiri yake, amekazia zaidi kuhusu wito wa utakatifu wa maisha kwa Wakristo wote; umuhimu wa kusamehe na kusahau pamoja na kupenda Msalaba, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa: Hekima, huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Mtakatifu Rita wa Cascia anakumbukwa na wengi kama mwombezi wa mambo yaliyoshindikana. Katika maisha na wito wake, daima alijiaminisha katika ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu! Baba Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, utakatifu wa Mtakatifu Rita wa Cascia unafumbatwa katika maisha yake ya kila siku, kama: Mama wa familia; mjane na hatimaye kama mtawa mmonaki  wa Shirika la Mtakatifu Agostino.

Katika maisha na wito wake, daima alijitahidi kutembea katika mwanga angavu wa maongozi ya Mungu kwa kujiaminisha kwake na daima Mungu amekuwa msaada na kimbilio lake katika shida, magumu na changamoto za maisha. Yote haya akayatumia kuwa ni chachu ya utakatifu wake. Kila mbatizwa anaitwa na kuhamasishwa kuwa ni Mtakatifu, kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili na utu wema, ili kuyatakatifuza malimwengu. Lakini, ili kufanikisha azma hii, kuna haja kwa waamini kushikamana na kushirikiana na Kristo Yesu katika maisha yao. Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma ni kati ya mambo yanayoweza kumsaidia mwamini kuchuchumalia na kuambatana utakatifu wa maisha, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani inayojenga mshikamano, umoja na udugu.

Mama Kanisa anatambua mchango wa watakatifu na mashuhuda wengi ambao bado hawajaandikwa katika orodha ya watakatifu wanaotambuliwa rasmi na Kanisa. Lakini hawa ni watu ambao wamemwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, wakaungana na kushibana kabisa na Kristo Yesu! Kardinali Becciu anakaza kusema, hakuna utakatifu pasi na upendo unaofumbatwa katika uvumilivu, maridhiano na msamaha. Mtakatifu Paulo katika Waraka wake kwa Warumi anakazia: Unyenyekevu na upendo katika Jumuiya; Upendo kwa watu wote hata adui. Anasema, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, si walegevu na kamwe wasimlipe mtu ovu kwa ovu!

Mtakatifu Rita wa Cascia ni mfano bora wa kuigwa katika kusamehe na kusahau bila kulipiza kisasi. Ni mfano wa upendo wa kidugu unaofumbatwa katika msamaha wa kweli; sala na toba ya ndani! Waamini wanahamasishwa kushinda ubaya kwa wema, kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu pamoja na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Mtakatifu Rita wa Cascia aliupenda sana Msalaba, akaukumbatia katika maisha yake! Alijifunza kwamba, Msalaba ni ufunuo wa hekima, huruma na upendo wa Mungu na kwake ukawa ni kimbilio la maisha na chechemi ya upendo kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wanahamasishwa kuwa ni wajenzi na mashuhuda wa Ufalme wa Mungu. Mtakatifu Rita wa Cascia awe ni mwombezi wa familia zinazokabiliana na changamoto na matatizo mbali mbali.

Mtakatifu Rita wa Cascia awawezeshe waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kujenga mtandao wa mshikamano wa upendo, katika kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mtakatifu Rita wa Cascia awe ni mfano bora wa kuigwa katika imani, ukarimu, amani na maridhiano kati ya watu!

Mt. Rita wa Cascia
22 May 2019, 15:18