Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Protase Rugambwa anawahimiza Wakristo kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu; Kudumisha Utakatifu wa maisha na kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu! Askofu mkuu Protase Rugambwa anawahimiza Wakristo kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu; Kudumisha Utakatifu wa maisha na kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu!  (Vatican Media)

Utakatifu wa maisha; Msikilizeni Roho Mt. Jengeni Mji wa Mungu!

Wakristo wanaitwa na kutumwa kushiriki katika ujenzi wa mji wa Mungu, yaani Ufalme wa Mungu, ili hatimaye, waweze kuingia katika utukufu wa Mungu. Ufalme wa Mungu unafumbatwa katika misingi ya haki, amani, upendo na huruma; mambo ambayo yanapata utimilifu wake wote kwa sababu yanapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, utimilifu wa utakatifu wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Jumapili, tarehe 26 Mei 2019 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Petro mjini Roma, kwa ajili ya Jumuiya Wanafunzi Wakatoliki Watanzania wanaosoma na kuishi Roma. Lengo kuu ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Mapadre na Watawa waliohitimu masomo yao na sasa wako njia moja kurejea nchini Tanzania ili kumwilisha hayo waliyojifunza katika maisha na utume wa Kanisa la Tanzania.

Pili ilikuwa ni nafasi ya kumshukuru Mungu kwa ajili ya Mashemasi 7 kutoka Tanzania, ambao hivi karibuni walipewa Daraja ya Huduma Altareni, ili waendelee kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kujisadaka tayari kushiriki katika mchakato mzima wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili! Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Protase Rugambwa amewakumbusha watanzania kwamba, kipindi hiki cha Pasaka, kinatoa fursa kwa waamini kuendelea kumshangilia Kristo Mfufuka, aliyemkomboa mwanadamu na kumwongoza katika njia inayoelekea kwenye mji mpya, Yerusalemu ya mbinguni, mji ambao Mungu mwenyewe ndiye asili yake na unaangazwa kwa mwanga wa Mwanakondoo wa Mungu, kielelezo cha utakatifu wa maisha!

Wakristo wanaitwa na kutumwa kushiriki katika ujenzi wa mji wa Mungu, yaani Ufalme wa Mungu, ili hatimaye, waweze kuingia katika utukufu wa Mungu na kumwona jinsi alivyo kama Mama Kanisa anavyofundisha, yaani kuonana na Mwenyezi Mungu: uso kwa uso! Mubashara! Ufalme wa Mungu unafumbatwa katika misingi ya haki, amani, upendo na huruma; mambo ambayo yanapata utimilifu wake wote kwa sababu yanapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, utimilifu wa utakatifu wote! Askofu mkuu Protase Rugambwa anakaza kusema, Kristo Yesu, Siku ile ya Alhamisi Kuu, aliwaahidia Mitume wake, zawadi na nguvu ya Roho Mtakatifu atakayewafundisha na kuwakumbusha yote aliyowafundisha alipokuwa hapa duniani.

Mapaji na karama za Roho Mtakatifu ziwawezeshe Wakristo kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Lakini, jambo la msingi ni kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu kama ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo kama ambavyo imefafanuliwa katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Roho Mtakatifu ndiye aliyewaongoza Wakristo wa Kanisa la mwanzo, wakajadiliana na hatimaye, kufikia muafaka wa kuwatuma Paulo na Barnaba pamoja na wengine wapande kwendsa Yerusalemu kwa Mitume na wazee wa Kanisa kuhusu tatizo la kutahiriwa. Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na Mitume, ili wasiwatwike mzigo, bali kukazia mambo msingi katika imani yaani: kujiepusha na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu na nyama zilizosongolewa, na uasherati.

Mitume wanaheshimu uhuru wa wale wanaotaka kujiunga na Kanisa ili kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Kwa kufanya hivyo wanapaswa kuachana na mambo ambayo yanakwenda kinyume cha mapenzi ya Mungu na utashi wake wa kutaka kumkomboa mwanadamu. Lengo ni kujenga umoja, udugu na mshikamano katika mambo msingi ya imani, maadili na utu wema. Askofu mkuu Protase Rugambwa anawakumbusha waamini kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anawakumbusha Wakristo wote kwamba, wao ni wafuasi wamisionari, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kuwashirikisha wengine huruma na upendo wa Mungu unaookoa.

Kila Mkristo ni mmisionari mahali alipo, changamoto ni kuelekea katika ukomavu wa kiimani unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Nguvu ya Roho Mtakatifu iwasaidie Wakristo kushirikiana na kushikamana na viongozi wa Kanisa kwa kutambua kwamba, chini ya kazi tendaji ya Roho Mtakatifu na ufunuo, Kanisa limejipatia mambo ambayo sasa yamekuwa ni sheria, taratibu na kanuni zinazoongoza maisha na utume wake hapa duniani. Watu wazingatia mambi msingi ya imani na kamwe wasiwatwishe mizigo jirani zao, kiasi cha kuwakatisha tamaa ya kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Askofu mkuu Rugambwa
27 May 2019, 17:47