Tafuta

Vatican News
Dr. Paolo Ruffini: Simameni kidete kulinda na kutetea uhuru wa kidini kimataifa! Dr. Paolo Ruffini: Simameni kidete kulinda na kutetea uhuru wa kidini kimataifa!  (AFP or licensors)

Simameni kidete kulinda uhuru wa kidini kimataifa!

Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano akichangia hoja katika mkutano huu, amesema kwamba, kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ubalozi wa Marekani mjini Vatican, chini ya uongozi wa Callista L. Gingrich, Jumatano, tarehe 3 Aprili 2019 umeandaa kongamano la kimataifa kuhusu uhuru wa kidini, lililongozwa na kauli mbiu “Tusimame kidete Kulinda Uhuru wa Kidini”. Hizi ni juhudi za kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; ili kuwapatia sauti waamini wanaoteseka, kunyanyasika na kubaguliwa kutokana na imani yao.

Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano akichangia hoja katika mkutano huu, amesema kwamba, kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii. Wahanga wakuu wa madhulumu ya kidini ni Wakristo; kwani kuna watu ambao wamehukumiwa kuuwawa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Leo hii anasema Baba Mtakatifu kuna idadi kubwa ya Wakristo wanaouwawa pengine kuliko hata ilivyokuwa kwenye Kanisa la mwanzo! Lakini, jambo la kushangaza vifo vya waamini hawa si  habari tena! Mauaji kwa kisingizio cha udini ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa pamoja na kuhakikisha kwamba, vyombo vya mawasiliano ya jamii, vinawajibika barabara katika kufichua maovu haya yanayoendelea kujificha katika jamii. Waandishi wa habari wanapaswa kuwa ni wahudumu wa ukweli mkamilifu bila kupindisha maneno! Waandishi wa habari wajitahidi kujikita katika misingi na kanuni za taaluma zao kutangaza na kushuhudia ukweli; kukuza na kudumisha umoja na mafungamano ya kijamii. Majadiliano ya kidini na kiekumene, yapewe msukumo wa pekee katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji.

Baba Mtakatifu anawataka wadau wa tasnia ya habari, wawe wadumifu katika kutangaza na kushuhudia ukweli; wajenge na kudumisha mahusiano mema, waendelee kukemea mambo yanayosababisha vita; wadumu katika majadiliano ili kujenga jamii inayofumbatwa katika msingi wa haki, kwa kulinda uhuru wa kidini hata kama ni kundi dogo. Waandishi wa habari wajiepushe kutumiwa wanasiasa kwa ajili ya propaganda za kisiasa na kiitikadi; kwa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kuna haja ya kuheshimu uhuru wa dhamiri unaomwezesha mwamini kutafuta ukweli na kuukumbatia.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu inawataka waamini kujikita katika kutenda mema; kuendeleza na kudumisha majadiliano ya kidini; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi. Waamini wawe na ujasiri wa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar,  katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu iliyotiwa sahihi wakati wa maadhimisho ya Mkutano wa Majadiliano ya Kidini Kimataifa huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, hapo tarehe 4 Februari 2019, wameonesha dira na mwongozo wa hija ya: haki, amani na upatanisho miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali. Hii ni dhamana inayowafumbata na kuwaunganisha watu wote wenye mapenzi mema, daima wakijitahidi kuongozwa na dhamiri nyofu.

Lengo ni kujenga mazingira yatakayowawezesha watu kuishi katika ulimwengu unaosimikwa katika haki, upendo na mshikamano. Huu ni mwaliko wa kuondokana na kufuru ya kutumia jina la Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao binafsi, sababu za kuanzisha vita, ghasia, chuki na mipasuko ya kijamii. Maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuendelezwa na wote. Huu ni mwanzo wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kuimarisha madaraja ya amani kati ya watu wa Mataifa; kizazi cha sasa na kile kijacho! Waamini wa dini mbali mbali waongozwe na kanuni ya dhahabu: Mtendee jirani yale unaoyotaka akutendee. Mtakatifu Paulo VI anasema, amani si ndoto wala wazo la kufikirika ni zawadi na tunu inayoweza kupatikana na ni wajibu kuitafuta amani kwani ni jina jipya la maendeleo.

Dr. Paolo: Uhuru wa Kidini
04 April 2019, 15:51