Tafuta

Vatican News
Mkutano wa Kimataifa kuhusu Biashara ya Binadamu na Mifumo ya utumwa mamboleo unafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 8-11-Aprili 2019. Mkutano wa Kimataifa kuhusu Biashara ya Binadamu na Mifumo ya utumwa mamboleo unafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 8-11-Aprili 2019. 

Mkutano wa Kimataifa kuhusu Biashara Haramu ya Binadamu Duniani

Mjini Vatican kuanzia tarehe 8-11 Aprili 2019 kunafanyika Mkutano wa Kimataifa kuhusu biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, Hawa ni watu wanaotumbukizwa katika mtego wa ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu; utalii wa ngono; kazi za suluba, ndoa za shuruti pamoja na watoto kuwa chambo cha vitakupelekwa mstari wa mbele kama chambo cha vita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kujizatiti, kuwajibika pamoja na kuonesha utashi wa kisiasa katika kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, ili kuondokana kabisa na janga hili linaloathiri utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kuwakamata na kuwashughulikia wafanyabiashara haramu ya binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ni tendo la haki, lakini suluhu ya kudumu ni toba na wongofu wa ndani, ili kuachana kabisa ya tabia hii chafu inayopandikiza utamaduni wa kifo!

Hizi ni juhudi za Baba Mtakatifu anazozishuhudia kwa maneno na matendo, ili kuweka bayana lengo dhahiri la Kanisa kuwa ni lile la kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu, vinavyofumbatwa katika huruma na upendo wa Mungu, mintarafu hali ya maisha bora kwa kila binadamu. Ikumbukwe kwamba, biashara haramu ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo, ndiyo tema ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameichagua kama sehemu ya tafakari ya Njia ya Msalaba, Ijumaa kuu kwa Mwaka 2019 kuzunguka Magofu wa Colosseo mjini Roma.

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu kuanzia tarehe 8-11 Aprili 2019 linaadhimisha Mkutano wa Kimataifa kuhusu biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, kwa kukazia umuhimu wa wadau kushikamana katika mapambano dhidi ya vitendo hivi viovu ndani ya jamii. Hawa ni watu wanaotumbukizwa katika mtego wa ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu; biashara na utalii wa ngono; kazi za suluba,  ndoa za shuruti pamoja na watoto kupelekwa mstari wa mbele kama chambo cha vita bila kuwasahau wanawake na wasichana wanaofanyishwa kazi za majumbani pengine kwa malipo kiduchu!

Mkutano huu wa faragha unahudhuriwa na watu 200, wakiwemo: Wakleri, watawa, pamoja na waratibu wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Hii ni fursa ya kupembua kwa makini Mwongozo wa Shughuli za Kichungaji Katika Biashara ya Binadamu, uliotolewa na kuridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 17 Januari 2019. Mkutano huu pamoja na mambo mengine, unalenga kuragibisha uelewa na madhara ya biashara ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo, ili kuweza kuitafutia ufumbuzi kutoka katika mizizi yake, ili hatimaye, kuutokomeza kabisa kutoka katika uso wa dunia! Pili, hii ni nafasi kwa wajumbe kubadilishana uzoefu, uelewa, mang’amuzi na njia muafaka ya kupambana na janga hili linalodhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Jumuiya ya Kimataifa ikisimama kidete na kujizatiti barabara kumaliza vita, migogoro, kinzani na mipasuko ya kijamii, itakuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti biashara haramu ya binadamu kwenye maeneo ya vita na migogoro duniani. Biashara haramu ya binadamu inadhalilisha utu na heshima ya binadamu, kwani mtu anageuzwa kuwa kana kwamba ni bidhaa na watu ambao wamefilisika kimaadili, watu wenye uchu wa madaraka, mali na utajiri wa haraka haraka. Watu wanaouzwa kama bidhaa, wakati mwingine, wanauwawa kikatili au kutelekezwa njiani, mambo yanayosababisha mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia. Biashara ya binadamu ni kashfa dhidi ya utu na heshima ya binadamu.

Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, vyombo vya ulinzi, usalama na sheria vinatekeleza vyema wajibu wake kwa kuwashughulikia kikamilifu wahalifu wote wanaojihusisha na biashara haramu ya binadamu ambayo kwa sasa imegeuka kuwa ni  ya kitaifa na kimataifa. Kumbe, kuna haja ya kuwa na ushirikiano kati ya Serikali mbali mbali na Mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na wadau mbali mbali ili kuhakikisha kwamba, biashara hii inavaliwa njuga hadi itokomee kabisa.

Ubaguzi wa aina yoyote ile ni kwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu! Biashara hii ni uhalifu dhidi ya ubinadamu kama ilivyo pia mifumo yote ya utumwa mamboleo kama vile: kazi za suluba, biashara ya ngono, biashara haramu ya viungo vya binadamu; yote hii ni mifumo ya utumwa mamboleo dhidi ya utu na heshima ya binadamu! Umaskini wa kutupwa, ukosefu wa maendeleo, ujinga, majanga asilia, rushwa na ufisadi; uchu wa fedha na mali; biashara ya haramu ya silaha na dawa za kulevya pamoja na vitendo vya utakatishaji fedha haramu ni kati ya mambo yanayochangia kuendelea kushamiri kwa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo!

Utumwa Mamboleo
08 April 2019, 08:52