Tafuta

Vatican News
Familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini ina kiu ya haki, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu! Imechoshwa na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii! Familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini ina kiu ya haki, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu! Imechoshwa na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii!  (AFP or licensors)

Sudan ya Kusini: Kiu kuu ni: amani, ustawi na mafao ya wengi!

Maaskofu wamekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi, haki, amani, amani, maridhiano na umoja wa Kitaifa, kama sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa Amani uliotiwa sahihi tarehe 12 Septemba 2018 nchini Ethiopia. Askofu mkuu Gallagher amepata nafasi pia ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali ya Sudan ya Kusini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa, hivi karibuni amefanya ziara ya kikazi nchini Sudan ya Kusini. Amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini chini ya uongozi wa Askofu mkuu Paulino Lukudu Loro wa Jimbo kuu la Juba pamoja na viongozi wa Serikali ya Sudan ya Kusini. Viongozi hawa wa Kanisa, wamepembua kwa kina na mapana changamoto za maisha, utume na shughuli za kichungaji nchini humo tangu mwaka 2011 baada ya Sudan ya Kusini kujipatia uhuru wake kutoka Sudan Kongwe. Wamegusia athari za vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ya Kusini katika kipindi cha miaka mitano kwa sasa!

Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini wamemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko ambaye ameonesha upendeleo wa pekee kwa hali na mali kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini; kwa uteuzi wa Askofu mkuu Hubertus Matheus Maria Van Megen kuwa Balozi mpya wa Sudan ya Kusini. Maaskofu wamekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi, haki, amani, maridhiano na umoja wa Kitaifa, kama sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa Amani uliotiwa sahihi tarehe 12 Septemba 2018 huko Addis Ababa, Ethiopia. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher amepata nafasi pia ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali ya Sudan ya Kusini chini ya Rais Salva Kiir Mayardit.

Viongozi hawa wanaridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Sudan ya Kusini na Vatican na kwamba, kuna haja sasa ya kuanza utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa ili kurejesha tena mchakato wa amani na kwamba, Vatican inapenda kushiriki katika mchakato huu ili kurejesha amani, chachu ya maendeleo endelevu na fungamani nchini Sudan ya Kusini kwa kukazia elimu. Katiba ya Kitume “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” iliyotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko, inatoa vigezo muhimu vinavyopaswa kuzingatiwa katika sekta ya elimu, kwani lengo ni kujenga na kukuza umoja na udugu, upendo na mshikamano, daima maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza!

Hii ndiyo dhamana ya umissionari wa Kanisa linalotoka kifua mbele ili kuinjilisha na kutamadunisha mintarafu mwanga wa furaha ya ukweli wa Kikristo! Kigezo cha pili ni majadiliano katika ukweli na uwazi mintarafu mwanga wa Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa ili kukuza na kudumisha utamaduni wa watu kukutana. Kigezo cha tatu ni mwingiliano makini wa masomo mbali mbali yanayotolewa na vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu kwa kuzingatia ubunifu kadiri ya mwanga wa Ufunuo. Majiundo, tafiti, mbinu za ufundishaji na maudhui yanayotolewa yanapaswa kuzingatia Ufunuo na Utume wa Kanisa katika dhamana ya uinjilishaji. Mkazo unaotolewa na Mababa wa Kanisa katika mfumo wa elimu unajikita katika mambo makuu manne yaani: umoja wa kisayansi, mawasiliano ya utakatifu, maisha adili na umwilishaji wa upendo katika maisha ya watu mambo yanayobubujika kutoka katika Neno la Mungu, vinginevyo, sayansi haina mizizi na wala kamwe haiwezi kuacha kumbu kumbu hai katika akili na nyoyo za vijana wa kizazi kipya!

Sayansi na utakatifu wa maisha ni sawa na “uji kwa mgonjwa”. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher amekazia umuhimu wa elimu kwa vijana wa kizazi kipya, ili kushiriki katika ujenzi wa jamii inayofumbatwa katika misingi ya haki, amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ametembelea na kukutana na Jumuiya ya Seminari kuu ya Mtakatifu Paulo, Jimbo kuu la Juba na kuwataka walezi na majandokasisi kuhakikisha kwamba, wanabaki kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa Kanisa, sanjari na kujisadaka bila ya kujiachilia kwa ajili ya huduma ya upendo kwa familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini.

Ametembelea pia kambi ya wakimbizi na wahamiaji, inayowahudumia watu zaidi ya milioni 2.1 pamoja na kuwahakikishia uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu katika mahangaiko yao ya kila siku. Amepata pia fursa ya kukutana na kuzungumza na wawakilishi wa Serikali mbali mbali na Mataifa ya Kimataifa nchini Sudan ya Kusini. Askofu mkuu Gallagher amepata pia fursa ya kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu iliyohudhuriwa na Rais Kiir wa Sudan ya Kusini. Katika mahubiri yake, amekazia amani kama chachu ya maendeleo fungamani ya binadamu; umuhimu wa majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na David Shearer, Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye amemwabarisha zaidi kuhusu hali ya kisiasa nchini Sudan ya Kusini; hali ya usalama pamoja na shughuli mbali mbali zinazotekelezwa na Jumuiya ya Kimataifa nchini humo. Mwishoni, kabla ya kurejea tena mjini Vatican, alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wakleri pamoja na watawa kutoka Sudan ya Kusini, kwa kuwataka kuvalia njuga changamoto za uinjilishaji wa kina na fungamani nchini humo. Wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wanao wahudumia. Familia ya Mungu nchini Sudan, bado inasubiri kwa imani na matumaini makubwa hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo!

Askofu Mkuu Gallagher
05 April 2019, 16:26