Tafuta

Vatican News
Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wazee duniani kwa njia ya mifumo ya hifadhi za jamii! Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wazee duniani kwa njia ya mifumo ya hifadhi za jamii! 

Vatican: Jumuiya ya Kimataifa iwalinde na kuwatetea wazee!

Askofu mkuu Bernardito Auza, anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete, kuwalinda na kuendeleza utu, heshima na haki msingi za wazee sehemu mbali mbali za dunia. Wazee wanaelemewa na umaskini, magonjwa, upweke na nyanyaso. Ni watu wanaokosa mahitaji yao msingi kama vile chakula, huduma za afya pamoja na usafiri. Walindwe dhidi ya utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema wazee na wagonjwa ni muhimu sana katika maisha na utume wa kanisa kwani sala na sadaka zao zinalitegemeza Kanisa. Huu ni mwaliko kwa wazee kuhakikisha kwamba, wanakuwa karibu na vijana ili kuwarithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Waendeleze majadiliano na watoto wadogo pamoja na vijana kwani katika maisha yao, wamebahatika kuwa na kumbu kumbu, ujuzi, maarifa na imani, mambo msingi wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya na kamwe wasijisikie kuwa ni watu waliopitwa na wakati.

Wazee watambue kwamba, wao ni mzizi wa maisha ya jumuiya, kumbe, ni wajibu wao kurithisha uzoefu na kumbu kumbu za maisha. Wazee wawasaidie watoto kung’amua maana ya maisha, tunu za maisha ya Kikristo na kiutu na kwamba, uzoefu wao, tayari ni shahada tosha kabisa katika maisha. Ni katika mazingira kama haya, Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete, kuwalinda na kuendeleza utu, heshima na haki msingi za wazee sehemu mbali mbali za dunia.

Wazee wanaelemewa sana na umaskini, magonjwa, upweke na nyanyaso. Ni watu wanaokosa mahitaji yao msingi kama vile chakula, huduma za afya pamoja na usafiri. Wazee ni waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi. Wazee wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Wazee washirikishwe kikamilifu katika maisha ya kijamii, ili kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwalinda wazee kwa kuwajengea mifumo bora ya hifadhi za jamii na kamwe wasionekana kuwa kama ni mizigo kwa Serikali.

Inasikitisha kuona kwamba, wazee wengi wanaanza kutumbukizwa kwenye utamaduni wa kifo kwa kukumbatia sera za kifo laini au euthanasia. Huu ni ukatili na unyama dhidi ya wazee ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya jamii. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa, tangu anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi anapofikia uzeeni! Umoja, upendo na mshikamano ni mambo msingi katika kudumisha majadiliano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya, changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko.

Huduma za Kijamii
16 April 2019, 10:16