Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anasema: Upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani; kwa kujikita katika ustawi, mafao na maendeleo ya wengi! Papa Francisko anasema: Upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani; kwa kujikita katika ustawi, mafao na maendeleo ya wengi!  (AFP or licensors)

Siasa safi ni kwa ajili ya huduma ya ustawi na mafao ya wengi!

Kardinali Marc Ouellet anasema, vijana 35 kutoka katika nchi 13 za Amerika ya Kusini, wanaendelea kufundwa na Mama Kanisa, kama sehemu ya mchakato wa kuwandaa kuwa viongozi watakaoweza kusimama: kulinda, kutetea na kudumisha maendele, ustawi na mafao ya wengi! Hawa ni vijana wanaotoka katika sekta ya elimu, biashara, siasa na ustawi wa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Wanasiasa wanahimizwa kujenga na kudumisha umoja na urafiki na Kristo Yesu pamoja na kutambua nguvu na udhaifu wao kama binadamu. Mchakato wa kuingia katika masuala ya kisiasa unapania pamoja na mambo mengine: kujenga urafiki wa kijamii, ili kuleta mageuzi yanayokusudiwa kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Mtakatifu Oscar Arnulfo Romero katika maisha na utume wake, alipenda kuwahimiza waamini walei kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji katika mazingira yao, kama kielelezo cha imani tendaji.

Kardinali Marc Armand Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Kipapa Amerika ya Kusini anasema, vijana 35 kutoka katika nchi 13 za Amerika ya Kusini, wanaendelea kufundwa na Mama Kanisa, kama sehemu ya mchakato wa kuwandaa kuwa viongozi watakaoweza kusimama: kulinda, kutetea na kudumisha maendeleo, ustawi na mafao ya wengi! Hawa ni vijana wanaotoka katika sekta ya elimu, biashara, siasa na ustawi wa jamii. Wakiwa mjini Vatican wamefundwa sanaa ya kusikiliza kwa makini na kujadiliana na wengine katika misingi ya ukweli na uwazi. Vijana hawa wamefundwa kuhusu umuhimu wa tafakari ya Neno la Mungu pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.

Siasa ni wito na si kila mwamini ana wito wa kuwa ni mwana siasa! Ikumbukwe kwamba, siasa si njia pekee inayoweza kuwahakikishia watu haki, kumbe, medani mbali mbali za maisha, ziwe ni mahali ambapo patawasaidia waamini kuweza kuyatakatifuza malimwengu, kwa kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha haki, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Waamini wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 anasema, upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu. 

Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi. Papa anasema mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri! Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa amani inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano na watu kuaminiana na kuthaminiana badala ya kuangaliana kwa “jicho la kengeza”.

Hizi ni dalili za ubinafsi unaofumbatwa katika dhana ya utaifa usiokuwa na tija wala mashiko badala ya kukuza umoja na udugu, wao wanakuwa ni sumu ya kusambaratisha watu. Jamii inawahitaji wajenzi wa amani, watakaokuwa ni watangazaji, mashuhuda na vyombo vya wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake ambaye anawatakia watoto wake furaha.Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini imeandaa programu maalum itakayowahusisha vijana ishirini na sita ambao ni viongozi kutoka Amerika ya Kusini, ili kuweza kunolewa barabara mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Hii ni programu ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa kipindi cha miezi sita na hatima yake, itakuwa ni mjini Roma, kwa kukutana na kuzungumza na “vigogo wa Mafundisho Jamii ya Kanisa”. Mpango mkakati huu unaongozwa na kauli mbiu “Mafundisho Jamii ya Kanisa Dhamana ya Kisiasa Amerika ya Kusini. Kwa ajili ya Kizazi Kipya cha Wakatoliki Kutoka Amerika ya Kusini katika masuala ya Kisiasa”. Lengo la Tume hii, ni kusaidia kuwafunda vijana ili kuwa wanasiasa bora na makini huko Amerika ya Kusini, mintarafu mwanga wa Mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu.

Vijana hawa ni wale walioteuliwa miongoni mwa vijana wenzao kutoka Amerika ya Kusini. Kati ya “vigogo” kutoka Vatican watakaowafunda vijana hawa ni pamoja na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu. Wengine watakuwa ni Maaskofu wakuu pamoja na wataalam na mabingwa wa masuala ya mawasiliano ya jamii, uinjilishaji na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Wanasiasa Amerika ya Kusini
13 March 2019, 10:56