Tafuta

Kardinali Lorenzo Baldisseri: Matunda ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana 2018 yameiva! Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia 2019 iko njiani! Kardinali Lorenzo Baldisseri: Matunda ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana 2018 yameiva! Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia 2019 iko njiani! 

Kardinali Baldisseri: Matunda ya Sinodi ya Vijana 2018 yameiva!

Kanisa linaendelea kujizatiti katika maadhimisho ya Sinodi katika maisha na utume wake, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuzima kiu ya matumaini ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia, ili kujikita katika ekolojia fungamani mintarafu mwanga wa Waraka wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, Kanisa linaendelea kujizatiti katika maadhimisho ya Sinodi katika maisha na utume wake, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuzima kiu ya matumaini ya watu wa familia ya Mungu wanaoishi katika Ukanda wa Amazonia, ili kujikita katika ekolojia fungamani mintarafu mwanga wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Huu ni Waraka  unaokazia kwa  namna ya pekee kabisa, utunzaji bora wa mazingira kuwa ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo endelevu na fungamani kwa sababu, mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Matumizi mabaya ya rasilimali za dunia, uchoyo, ubinafsi sanjari na uwajibikaji duni umepelekea uharibifu mkubwa wa mazingira, kiasi cha binadamu kujisikia kuwa ni mtawala wa mazingira na mwenye haki ya kutumia rasilimali hizi kadiri anavyopenda; matokeo yake ni uchafuzi mkubwa wa mazingira unaoendelea kuwatumbukiza wengi katika umaskini. Kardinali Baldisseri anasema,  Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana limekuwa ni tukio lenye utajiri na uzoefu mkubwa wa maisha na utume wa Kanisa ambao umejikita katika mshikamano wa utu wa binadamu.

Ni tukio ambalo limewashirikisha wadau mbali mbali katika maisha na utume wa vijana wa kizazi kipya pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa vijana wenyewe ili kuchangia mawazo, matatizo, changamoto na matamanio yao halali katika medani mbali mbali za maisha, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa watu wa Mataifa. Mababa wa Sinodi katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018, wamesafiri pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakafanya kazi kwa umoja na mshikamano, huku wakizingatia mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa, kiasi hata cha kujisikia kuwa ni fumbo la mwili mmoja, unaoteseka na kufurahia, ili kwa njia ya neema ya Mungu, Kanisa liweze kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na matumaini kwa watu wa Mataifa.

Kardinali Baldisseri anaendelea kufafanua kwamba, Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana imegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo  zimejikita katika mawazo ya Injili yanayowaonesha wale wafuasi wa Emau, waliokuwa wanaandamana na Yesu; Yakafunguliwa macho yao nao wakamtambua; Wakatoka kwa haraka kwenda kutangaza kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka kweli kweli kutoka kwa wafu! Hii ndiyo changamoto ambayo Mababa wa Sinodi wanayataka Makanisa mahalia kuimwilisha katika maisha na utume wa Kanisa, daima yakijitahidi kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano na vijana, kwa kuandamana na kukaa na vijana, ili kuwasaidia kung’amua maisha yao; kutafsiri matukio mbali mbali katika mwanga wa Maandiko Matakatifu na hatimaye, kufanya maamuzi magumu ambayo watapaswa kuyatekeleza haraka, kwa kushikishana mang’amuzi yao baada ya kukutana na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emau.

Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018 imewajengea vijana imani na matumaini kwa Kristo na Kanisa lake; imewataka vijana kuwa ni Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa, daima wakiendelea kutafuta maana halisi ya maisha mintarafu mwanga wa Injili ya Kristo na kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuwa ni dira na kiongozi wa maisha yao angavu. Kardinali Baldisseri anaendelea kufafanua kwamba, kwa mara ya kwanza, Kanisa limetumia “Costituzione Apostolica Episcopalis Communio” yaani “Hati ya Kitume kuhusu Sinodi za Maaskofu” iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Mwezi Septemba 2018 inafanya mabadiliko makubwa katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kama chombo cha uinjilishaji kinachopaswa kuwahusisha watu wa Mungu ili kujenga sanaa na utamaduni wa kusikilizana, kupanga, kuamua na kutekeleza sera na mikakati ya maisha na utume wa Kanisa.

Mchakato huu, umetumiwa kwa majaribio wakati wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia; ukaimarishwa wakati wa maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018 na sasa utekelezaji wake unapaswa kumwilishwa katika Mabaraza ya Kipapa pamoja na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki pamoja na taasisi zake. Mafanikio ya mchakato huu yataonekana kwa wakati wake! Mkazo ni Neno la Mungu, Majadiliano katika Makundi madogo madogo, ili kutoa nafasi kwa washiriki kuchangia kikamilifu katika mada zinazojadiliwa; kwa Mababa wa Sinodi kubadilishana uzoefu na mang’amuzi yao. Sekretarieti ya Sinodi za Maaskofu imepewa dhamana kubwa ya kuratibu maadhimisho haya.

Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia: Baba Mtakatifu Francisko ameamua kwamba, Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2019 iongozwe na kauli mbiu “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kujikita katika masuala ya haki, amani na mshikamano; utume na huduma ya upendo, ili kuhakikisha kwamba, Injili ya Kristo inatamadunishwa katika uhalisia wa maisha ya wananchi wa Amazonia, ili Kanisa liweze kupata sura mpya ya watu wa Amazonia kwa kuwa na mihimili yake ya uinjilishaji. Hii ni changamoto inayohitaji ari, ujasiri na moyo wa kuthubutu, kwani kila jambo linawezekana mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kardinali Baldisseri anakaza kusema, kuna uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote na ukoloni wa kiitikadi pamoja na ukoloni mamboleo, unaofumbatwa katika nguvu ya kisiasa na kiuchumi inayotishia: ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Amazonia. Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia inapania pamoja na mambo mengine: kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji na kitume kwenye Ukanda wa Amazonia. Kwa kukabiliana kwa dhati kabisa na uhaba mkubwa wa mihimili ya uinjilishaji wa kina, hali inayowafanya waamini wa Amazonia kukosa huduma makini na endelevu za kichungaji, kiasi hata cha kujisikia kwamba, wametelekezwa na Mama Kanisa.

Hapa mkazo ni sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya watu mahalia; Katekesi ya awali na endelevu; malezi na makuzi ya familia ya Mungu katika eneo hili; Sakramenti za Kanisa, Liturujia kama chombo cha kumtolea Mungu sifa na utukufu na mwanadamu kukombolewa. Kanisa linapenda kujizatiti zaidi katika masuala ya kiekolojia na utunzaji bora wa mazingira, haki jamii, utamadunisho; ushiriki wa wananchi katika siasa na masuala ya kiuchumi pamoja na kukuza tasaufi ya ekolojia. Kardinali Baldisseri anaendelea kufafanua kwamba, tangu mwaka 2007, Baba Mtakatifu wakati huo akiwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires, alishiriki kikamilifu katika mkutano mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean ulioadhimishwa huko Aparecida alishuhudia mwenyewe utajiri mkubwa uliokuwa unafumbatwa katika maisha na tamaduni za watu wa Ukanda wa Amazonia.

Baba Mtakatifu akasikitishwa na uharibifu mkubwa wa mazingira, kiasi kwamba, alipotembelea eneo hili kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, mwezi Januari, 2018 akataka amana na utajiri wa familia ya Mungu kutoka Ukanda wa Amazonia ulindwe na kudumishwa! Kumbe Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Amazonia itajikita katika masuala ya ekolojia fungamani ambako huko kuna Makampuni makubwa ya Kimataifa ambayo yamewekeza katika uchimbaji wa madini, gesiasilia na uvunaji wa misitu. Kuna watu wanaoendesha kilimo cha mashamba makubwa kwa ajili ya nishati uoto, hali inayotishia sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ndiyo sera na mkakati wa Mama Kanisa unaowashirikisha watu wengi ili kupembua kwa kina na mapana changamoto za utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote; ekolojia fungamani na endelevu kama sehemu ya mbinu mkakati wa sera na utume wa Kanisa sanjari na kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili katika Ukanda wa Amazonia.

Sinodi ya Vijana 2018

 

 

21 March 2019, 10:11