Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Protase Rugambwa amewataka waamini kukimbilia toba na wongofu wa ndani na kwamba, ajidhaniaye kwamba, amesimama aangalie asianguke! Askofu mkuu Protase Rugambwa amewataka waamini kukimbilia toba na wongofu wa ndani na kwamba, ajidhaniaye kwamba, amesimama aangalie asianguke! 

Askofu mkuu Protase: Ajidhaniaye amesimama aangalie asianguke!

Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu amewataka waamini kukimbilia toba na wongofu wa ndani, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Mtu yeyote anayedhani kwamba, amesimama ajiangalie asianguke! Kila mtu achunguze vyema dhamiri yake, ili kuangalia mema ya kufuata na mabaya kuachana nayo katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya Wanafunzi Wakatoliki Watanzania wanaosoma na kuishi Roma, Jumapili, tarehe 24 Machi 2019 imeadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Kikanisa cha Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Petro, mjini Roma. Ibada hii imeongozwa na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu! Lengo la Ibada hii ya Misa Takatifu ni kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa wa familia ya Mungu kutoka Tanzania. Kuomba neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili kusonga mbele katika masomo na majukumu mbali mbali yanayotekelezwa na watanzania wanaoishi na kusoma Roma. Katika kipindi hiki cha Kwaresima, Mama Kanisa anawakirimia waja wake muda wa toba na wongofu wa ndani; muda wa sala na tafakari ya Neno la Mungu linalopaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama njia ya kujifananisha na Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia! Askofu mkuu Rugambwa katika mahubiri yake, amekazia kwa namna ya pekee kabisa, umuhimu wa kutumia muda uliokubalika kwa toba na wongofu wa ndani. 

Na kama anavyoonya Mtakatifu Paulo katika Waraka wake kwa Wakorintho akisema, wala watu wasinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu! Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kuwaonya hata watu wa kizazi kwani ajidhaniaye amesimama na aangalie asianguke! Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na upendo na kwamba, Neno lake ni dira na mwongozo wa watu wa nyakati zote na kwamba, anataka kuwaokoa waja wake kutoka katika njia mbaya na utumwa wa dhambi ili wasipate na mabaya kama ilivyotokea kwenye Agano la Kale, kwaTaifa teule la Mungu!

Askofu Mkuu Rugambwa anakaza kusema, hayao yaliyowasibu Waisraeli kwenye Agano la Kale yanaweza kuwasaibu hata watu wa nyakati hizi, kwa hiyo wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu vinginevyo wataangamia! Lakini, anakumbusha kwamba, upendo na huruma ya Mungu hata kama unafundishwa kwa ari na moyo mkuu, lakini bado kuna wakati waamini wanakata tamaa kwa kudhani kwamba huruma na upendo wa Mungu vimetoweka! Huruma na upendo wa Mungu upooo! Mwenyezi Mungu katika mpango wake wa kazi ya uumbaji, alimuumba mwanadamu ili: amjue, ampende, amtumikie na mwishowe aweze kufika kwake mbinguni, ili kupata furaha isiyokuwa na mwisho!

Kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, Mwenyezi Mungu alijibidisha sana kuwakomboa wateule wake, kumchagua Mtumishi wake Musa, ili aweze kuwa ni chambo cha ukombozi na kuambiwa kwamba, Mwenyezi Mungu ameyaona mateso ya watu wake, amesikia kilio chao na sasa ameshuka ili aweze kuwaokoa kutoka utumwani Misri. Huu ndio mpango unaoendelea kutekelezwa na Mwenyezi Mungu hata kwa watu wa nyakati hizi, ili aweze kuwaokomboa kutoka katika njia mbaya. Huu ni muda wa toba na wongofu wa ndani; ni kipindi cha kumrudia Mwenyezi Mungu ili kushiriki katika utukufu na maisha ya uzima wa milele! Lakini, ikumbukwe kwamba, nafasi hii ni kwa wale tu wanaosikia Amri, maagizo na mashauri ya Mungu, wataokolewa na kufurahia uzima wa milele! Wale wote wanaokwenda kinyume chake, kwa hakika wataangamia milele.

Askofu mkuu Protase Rugambwa, amekumbusha kwamba, hapa duniani, waamini wanafanya hija Jangwani kama lilivyo hata Kanisa linalosafiri hapa duniani kuelekea kwenye Nchi ya ahadi, nchi ambayo imejaa maziwa na asali, yaani Yerusalemu ya mbinguni, mahali ambapo waamini wataweza kumwomba Mungu uso kwa uso na kufurahia utukufu wake usiokuwa na mwisho! Lakini pale waamini wanapojisahau na kuanza kujitafutia miungu wao wa “bandia” na furaha za mpito, huo ni mwanzo wa kutopea katika maovu na hatima yake ni kuangamia milele! Hata katika hali na mazingira kama haya, bado huruma ya Mungu inawatafuta waja wake, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, wale watu wakawa na shingo ngumu. Wakamlilia na kumnung’unikia Mungu, naye akawasikiliza na kuwalisha chakula kilichoshuka kutoka mbinguni, akawanywesha maji kutoka mwambani! Mtume Paulo anasema, mwamba ule ni Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.

Daima Mwenyezi Mungu anatoa nafasi kwa waja wake, ili waweze kutubu na kumwongokea. Ni fursa ya kusimama na kuchunguza dhamiri kwa mwanga wa matukio katika maisha na utume wa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Lengo ni kutambua mema ya kufuata na mabaya ya kuachana nayo, tayari kumbata neema ya utakaso, ili kuonesha upendo kwa Mungu na jirani! Askofu mkuu Protase Rugambwa anahitimisha mahubiri yake kwa kusema, huu ndio muda uliokubalika, huu ndio muda wa toba na wongofu wa ndani, ili kuhesababiwa haki kama ilivyokuwa kwa Baba mwenye huruma, pale Mwana mpotevu alipotubu na kumwongokea Mungu, akarejea tena kwa Baba yake, ili kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka! Ajiadhaniaye amesimama, aangalie asianguke!

Mahubiri Rugambwa
25 March 2019, 15:09