Tafuta

Vatican News
Askofu Mkuu Gianfranco Gallone, Balozi wa Vatican nchini Zambia, tarehe 19 Machi 2019 amewekwa wakfu na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Askofu Mkuu Gianfranco Gallone, Balozi wa Vatican nchini Zambia, tarehe 19 Machi 2019 amewekwa wakfu na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. 

Askofu mkuu Gallone, Balozi wa Vatican Zambia awekwa wakfu

Askofu mkuu Gallone katika maisha na utume wake analo jukumu sawa na la Mtakatifu Yosefu la kumlinda na kumtunza Kristo Yesu; atambue kwamba, anashiriki katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kwa njia hii ataweza kuendelea kutangaza na kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani, kwa njia ya zawadi ya neema aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa. Wao ni walengwa wa kwanza wa Habari Njema ya Wokovu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake alitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Huduma kwa maskini ni utambulisho na mtindo wa maisha ya Kikristo. Hija ya maisha ya mwamini katika sala, toba na wongofu wa ndani inafumbatwa katika huduma makini kwa maskini kama njia ya kukutana uso kwa uso na Fumbo la Mwili wa Kristo, unaonyanyasika kutokana na umaskini, ujinga na maradhi.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumanne, tarehe 19 Machi 2019, Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu, wakati alipokuwa anamweka wakfu Askofu mkuu Gianfranco Gallone, Balozi mpya wa Vatican nchini Zambia. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Italia.

Kardinali Parolin, amemtaka Askofu mkuu Gallone, kuiga mfano wa Mtakatifu Yosefu anayetajwa katika Maandiko Matakatifu kuwa alikuwa ni mtu: jasiri, mtiifu, msafi kamili, mwenye imani thabiti na hekima ya kimbingu, mtu wa haki, mchapa kazi mahiri, mwenye upendo na furaha kuu; mtu mkimya asiyependa makuu, aliyetekeleza dhamana ya kulinda na kuitunza familia takatifu kwa moyo thabiti! Ni mtu aliyejiweka wazi kupokea mshangao wa Mungu katika maisha yake, changamoto na mwaliko kwa waamini hata katika ulimwengu mamboleo, kudumu katika imani, matumaini na mapendo katika maisha na wito wao.

Huu ndio mwaliko hata kwa Askofu mkuu Gallone katika maisha na utume wake kwani, analo jukumu sawa na la Mtakatifu Yosefu la kumlinda na kumtunza Kristo Yesu; atambue kwamba, anashiriki kikamilifu katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kwa njia hii ataweza kuendelea kutangaza na kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani, kwa njia ya zawadi ya neema aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Paulo VI anawakumbusha Maaskofu kwamba, utimilifu huu wa Daraja Takatifu ni heshima inayofumbatwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu. Ni changamoto na mwaliko wa kuambata hija ya utakatifu wa maisha; kwa kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Hii ni safari inayomwezesha kiongozi wa Kanisa kuwa ni chombo na shuhuda wa Injili ya upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kama Askofu anatakiwa kukuza na kudumisha urika na Maaskofu wenzake, umoja na mshikamano na watu wa Mungu. Askofu anatakiwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Maskini, wanaoteswa na kunyanyaswa pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ndio wanaopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa. Siku ya mwisho, waamini watahukumiwa kadiri ya matendo yao kwa maskini! Haiwezekani mwamini kujiita Mkristo, huku akiwadharau na kuwabeza maskini, ambao wamepewa upendeleo wa pekee kabisa katika maisha na utume wa Kristo Yesu, kiasi hata cha kuwa ni mfano bora wa kuigwa!

Kardinali Parolin amekumbusha kwamba, Mwaka 2017, Vatican na Zambia ziliadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uhusiano wa Kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili. Mahusiano haya yalianzishwa na Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 27 Oktoba 1965 katika Waraka wake wa kitume “Africae gentes”. Amekumbusha kwamba, Zambia ina zaidi ya Wakristo milioni tano, sawa na asilimia 30% ya idadi ya wananchi wote wa Zambia. Ni nchi ambayo imeonesha ukarimu, udugu na mshikamano kwa kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi na wahamiaji kutoka Rwanda, Burundi na DRC. Dhamana na wajibu wa Askofu mkuu Gallone ni kuhakikisha kwamba, kama mwakilishi wa Baba Mtakatifu, anaimarisha mahusiano na mafungamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia.

Ashirikiane na Maaskofu mahalia katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, akionesha upendo kwa Kanisa na kwa watu wa Mungu nchini Zambia! Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni Baba Mtakatifu Francisko alimteua Askofu mkuu Gianfranco Gallone, kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Zambia. Askofu mkuu Gallone, alizaliwa tarehe 20 Aprili 1963 huko Ceglie Messapica, Brindis, Kusini mwa Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi akapewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 3 Septemba 1988. Baadaye akajiendeleza zaidi na kujipatia Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa na Taalimungu ya Liturujia.

Askofu mkuu Gallone alianza kufanya utume wake hapa mjini Vatican tarehe 19 Juni 2000 na kubahatika kutekeleza dhamana na utume wake huko Msumbiji, Israeli, Slovacchia, India pamoja na Sweden. Mwishoni, alihamishiwa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, Idara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Na tarehe 19 Machi 2019 akawekwa wakfu kuwa Askofu mkuu na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican.

Zambia
20 March 2019, 15:08