Tafuta

Mafungo ya Kwaresima kwa Mwaka 2019: Tunu msingi za Kiinjili katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo! Mafungo ya Kwaresima kwa Mwaka 2019: Tunu msingi za Kiinjili katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo! 

Mafungo ya Kwaresima 2019: Utume wa Kanisa

Mama Kanisa anapenda kuendeleza mchakato wa ujenzi wa dunia iliyo bora zaidi inayofumbatwa katika utamaduni wa umoja, upendo na ukarimu wa kidugu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ambazo kwa baadhi ya watu zinazonekana kana kwamba, zimepitwa na wakati! Huu ni utajiri ambao Abate Bernardo Francesco Maria Gianni anapenda kumshirikisha viongozi wa Kanisa kwa sasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafungo ya Kwaresima kwa mwaka  2019 kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na waandamizi wake wa karibu, kuanzia tarehe 10-15 Machi 2019, huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma, yanaongozwa na Abate Bernardo Francesco Maria Gianni kutoka Abasia ya “San Miniato al Monte”. Kauli mbiu ya tafakari hizi ni “Mji wenye tamaa kali. Kwa ajili ya mwono na alama za kipasaka ulimwenguni”. Lengo ni kujenga utamaduni wa ukarimu! Huu ni mchakato kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu,  anayewaangalia walimwengu na hivyo kutoa mwaliko wa kujenga umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii na kiutu, ili kushirikishana cheche za: imani, matumaini na mapendo.

Mama Kanisa anapenda kuendeleza mchakato wa ujenzi wa dunia iliyo bora zaidi inayofumbatwa katika utamaduni wa umoja, upendo na ukarimu wa kidugu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ambazo kwa baadhi ya watu zinazonekana kana kwamba, zimepitwa na wakati!  Huu ni utajiri ambao Abate Bernardo Francesco Maria Gianni anapenda kumshirikisha Baba Mtakatifu Francisko pamoja na waandamizi wake, ili kuweza kukabiliana na changamoto za shughuli za kichungaji na maisha ya kijamii zinazoibuliwa kila kukicha katika ulimwengu mamboleo.

Abate Gianni anasema, ufunuo wa uso wa Kristo Yesu, mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake, ndiyo changamoto iliyoko mbele yake kwa wakati huu, ili kweli Yesu aweze kufahamika na kupendwa na hatimaye, aweze kuwasaidia watu wa Mungu kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa ukarimu, huku wakiwa na tamaa na shauku kali isiyopitwa na wakati wala kumezwa na malimwengu. Huu ndio mchakato wa ujenzi wa Yerusalemu mpya unaojikita katika fadhili za Kimungu, zinazoleta mvuto kwa watu wa Mataifa, ili kuendeleza na kudumisha mradi mkubwa wa haki na amani duniani.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujibidisha kumtafuta Mwenyezi Mungu kati ya watu wa mijini! Kila mwamini katika maisha, wito na utume wake, awe na jeuri ya kulitafakari Fumbo la Mungu ambalo ni muhtasari wa upendo! Mafungo haya ni mwendelezo wa tafakari ya Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa na ni moja ya nguzo muhimu sana katika kipindi hiki cha Kwaresima.

Miji inapaswa kuwa ni madaraja ya kuwakutanisha watu katika umoja na upendo, tayari kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Huu ndio mwelekeo sahihi katika mchakato wa shughuli za kichungaji. Abate Bernardo Francesco Maria Gianni ambaye ni mtawa wa Shirika la Wabenediktini, anasema, hata watawa mijini, wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa sadaka na majitoleo kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani inayotolewa kwa moyo wa unyenyekevu na kiasi kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Watawa na wakleri katika maisha, wito na utume wao, wawe kweli ni mfano bora wa kuigwa katika: kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha na utume wao. Watambue kwamba, wao wameitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.

Kipindi cha Kwaresima ni wakati muafaka wa kuzima kiu ya uwepo endelevu wa Mungu inayowawezesha waamini kutambua kwamba, wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kwa wafu; ufufuko unaoleta maisha ya uzima wa milele. Hiki ni kipindi cha kukuza na kudumisha cheche za imani, matumaini na mapendo, kwa kutembea katika mwanga wa tunu msingi za maisha ya Kiinjili, ili hatimaye, kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo na ukarimu.

Abate Bernardo Francesco Maria Gianni anakiri kwamba, hiki ndicho kiini cha mafungo ya Kwaresima kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na waandamizi wake. Kanisa linatambua kwamba, linao wajibu na dhamana kubwa ya kuwasaidia watu kukuza na kudumisha cheche za imani, matumaini na mapendo katika maisha yao. Huu ni wakati wa kuwasha tena moto wa shauku ya matumaini, kwa wale waliokata tamaa; watu wanaotembea katika giza la imani, matumaini na mapendo. Huu ndio wakati uliokubalika wa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi ndani ya waja wake, tayari kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka kwa ari na nguvu mpya!

Mafungo: Abate

 

11 March 2019, 09:27