Tafuta

Vatican News
Abate san Miniato: tafakari za Mafungo ya Kwaresima kwa Mwaka 2019 ni ujenzi wa utamaduni wa ukarimu! Abate san Miniato: tafakari za Mafungo ya Kwaresima kwa Mwaka 2019 ni ujenzi wa utamaduni wa ukarimu!  (Vatican Media)

Mafungo ya Kwaresima 2019: Ujenzi wa utamaduni wa ukarimu!

Huu ni mchakato wa Yesu anayewaangalia walimwengu na hivyo kutoa mwaliko wa kujenga umoja, mshikamano na mafungamano, ili kushirikishana cheche za matumaini, kwa ajili ya ujenzi wa dunia iliyo bora zaidi, inayofumbatwa katika umoja na udugu. Hii ni changamoto ya ujenzi wa utamaduni wa upendo na ukarimu unaofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican kuanzia Jumapili tarehe 10 hadi Ijumaa tarehe15 Machi 2019, watasitisha shughuli zote za kitume na kwenda “kujichimbia Mlimani”, kwenye nyumba ya mafungo ya “Divin Maestro” huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma, ili kujipatia muda wa kusali na kutafakari, tayari kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Mafungo yanaongozwa na Abate Bernardo Francesco Maria Gianni kutoka Abasia ya “San Miniato al Monte”. Kauli mbiu ya tafakari hizi ni “Mji wenye tamaa kali. Kwa ajili ya mwono na alama za Kipasaka Ulimwenguni”.

Hii ni sehemu ya Shairi lililotungwa na Mario Luzi, mwezi Desemba 1997. Kila siku itaongozwa na tema maalum ili kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo na ukarimu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Maamuzi mbele, uchoyo na ubinafsi ni mambo ambayo yanaendelea kukwamisha mchakato wa utamaduni wa upendo, ukarimu na mshikamano kati ya watu. Abate Bernardo Francesco Maria Gianni katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, aliguswa sana na mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kuandaa mafungo ya Kwaresima kwa mwaka 2019. Anasema, hii ni dhamana nyeti na nzito, lakini ameipokea kwa moyo wa shukrani na kwamba, Shairi la Mario Luzi ni muhimu sana kwa nyakati hizi, kuweza kutafakari kuhusu maisha na utume wa Kanisa. Ni Shairi linalotoa mwanga katika maadhimisho ya Liturujia, ili kumtukuza Mungu na mwanadamu kutakasika na hatimaye, kukombolewa.

Huu ni muda wa kumtafuta Mwenyezi Mungu kadiri ya mazingira na fursa zilizopo mintarafu mwanga wa Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Evangelii gaudium” yaani “ Furaha ya Injili”. Mario Luzi katika shairi lake anafafanua na kupembua kwa kina dhana ya mambo msingi katika maisha, kumbu kumbu, matumaini, udugu, ugumu na changamoto za maisha katika ulimwengu mamboleo, mwaliko wa kupyaisha tena Injili ya huruma na upendo kati ya watu wa Mungu. Ni fursa ya kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kulipyaisha Kanisa lake kwa kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari, tayari kuwapokea na kuwasikiliza wengine shida na mahangaiko yao ya ndani! Pale inapowezekana kuweza kujibu changamoto hizi kadiri ya fursa na uwezo uliopo! Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, anaendelea kukazia umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza katika mambo msingi ya maisha ya kiroho.

Mtakatifu Riccardo wa S. Vittore alikuwa anapenda kusema, “Ubi amor, ibi oculos” yaani “Pale penye upendo, hapo kuna kutazama kwa makini”. Huu ni mchakato wa Yesu anayewaangalia walimwengu na hivyo kutoa mwaliko wa kujenga umoja, mshikamano na mafungamano, ili kushirikishana cheche za matumaini, kwa ajili ya ujenzi wa dunia iliyo bora zaidi, inayofumbatwa katika umoja na udugu. Hii ni changamoto ya ujenzi wa utamaduni wa upendo na ukarimu unaofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili. Lengo ni kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; haki na amani; upendo na ukarimu kwa wageni; daima maskini na wanyonge wakipewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya kisiasa, kijamii, kitamaduni na kiuchumi. Shairi hili limesheheni utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na kitamaduni, nyenzo muhimu sana katika mchakato wa kuwafunda na kuwaimarisha watu katika wito wao mtakatifu.

Mafungo 2019
08 March 2019, 16:34