Tafuta

Vatican News
Siku ya Wagonjwa Duniani 2019: Kauli mbiu "Mmepata bure, toeni bure" Siku ya Wagonjwa Duniani 2019: Kauli mbiu "Mmepata bure, toeni bure" 

Siku ya Wagonjwa Duniani, India: Yaliyojiri kwa mwaka 2019

Hii ni fursa ya kutafakari: kuhusu mateso ya mwanadamu katika mwanga wa maisha ya Kikristo! Wajumbe wamepembua: Misingi ya kitaalimungu katika huduma ya uponyaji pamoja na Taalimungu ya kuwasindikiza na kuwahudumia wagonjwa na wanaoteseka mintarafu tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko. Wajumbe pia wamepitia Mwongozo Mpya wa Wafanyakazi Katika Sekta ya Afya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya XXVII ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2019 huko Calcutta, nchini India kuanzia tarehe 9-12 Februari 2019 imekuwa ni nafasi ya kuweza kutafakari kwa kina na mapana  kuhusu mateso ya mwanadamu katika mwanga wa maisha ya Kikristo! Wajumbe wamepembua: Misingi ya kitaalimungu katika huduma ya uponyaji pamoja na Taalimungu ya kuwasindikiza na kuwahudumia wagonjwa na wanaoteseka mintarafu tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko.

Wajumbe pia wamepitia Mwongozo Mpya wa Wafanyakazi Katika Sekta ya Afya uliozinduliwa Mwezi Septemba 2017. Utume wa huduma ya afya kwa magonjwa kama vile ulemavu wa kuona na kusikia; mtindio wa ubongo; wazee waliokata tamaa pamoja na waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya! Wajumbe wametembelea na kuangalia vituo vya huduma ya afya sehemu mbali mbali za Calcutta. Kardinali Peter Turkson, Jumapili tarehe 9 Februari 2019, akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoka Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa. Jumatatu, tarehe 11 Februari 2019, kilele cha Siku ya Wagonjwa Duniani, Kardinali Patrick D’Rozario, C.S.C, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dhaka, mwakilishi maalum wa Papa katika maadhimisho ya Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2019, kwa kukazia kuhusu: mchakato wa tiba na huduma kwa wagonjwa uzingatie: utu, heshima na mahitaji msingi ya mgonjwa.

Baba Mtakatifu Francisko katika taalimungu ya kuwasindikiza na kuwahudumia wagonjwa na wanaoteseka anasema, huduma kwa wagonjwa na wale wote wanaoteseka ni utekelezaji wa Injili ya upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote. Ni sehemu ya mchakato wa kutangaza, kushuhudia na kujenga Ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama alivyofanya Msamaria mwema. Kumbe, ni wajibu wa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaoteseka.

Wajumbe wamepitia kwa mara nyingine tena, Mwongozo wa Wafanyakazi Katika Sekta ya Afya uliozinduliwa Mwezi Septemba 2017. Kimsingi unakazia umuhimu wa wafanyakazi katika sekta ya afya kuhakikisha kwamba wanatumia: akili, ujuzi, maarifa na weledi wao kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa; wawaoneshe huruma na upendo na kamwe wasiwageuze kuwa ni kichokoo cha majaribio ya kisayansi! Wafanyakazi hawa wawaonjeshe: huruma na upendo; wawapatie kipaumbele wanachohitaji kwa uwepo na huduma yao makini; wawaelewe na kushirikishana; wawaonjeshe wagonjwa uvumilivu na utu wema sanjari na kukuza majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi na mafao ya mgonjwa mwenyewe! Kila mgonjwa anapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma na mapendo!

Sekta ya afya inakabiliwa na changamoto kubwa ya kimaadili, ukosefu wa rasilimali fedha na watu; vifaa tiba na dawa; hali ambayo inapelekea watu wengi kupoteza maisha hasa katika nchi maskini zaidi duniani. Bado kuna idadi kubwa ya watu walioathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi, ambao bado hawajapata fursa ya kupatiwa dawa za kurefusha maisha; hawa pia ni changamoto kubwa inayohitaji mshikamano wa upendo, unaoongozwa na kanuni auni! Makampuni makubwa yanayotengeneza dawa, yanapaswa kuonesha moyo wa huruma na upendo kwa maskini badala ya kujikita katika kutafuta kupata faida kubwa.

Jumuiya ya Kimataifa ijenge mtandao wa umoja, mshikamano na udugu kwa ajili ya kuwasaidia watu wanaoteseka kutokana na magonjwa mbali mbali, hasa yale yasiyokuwa na tiba wala chanjo! Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Siku ya Wagonjwa Duniani ni nafasi kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutambua umuhimu wa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na maskini sehemu mbali mbali za dunia. Mtakatifu Yohane Paulo II anakaza kusema, hii ni fursa kwa waamini katika ngazi mbali mbali kujizamisha katika huduma kwa wagonjwa; kwa kukazia umuhimu wa mafunzo ya awali na endelevu katika huduma kwa wagonjwa.

Maadhimisho haya yasaidie watu kutambua na kukuza ari na moyo wa huduma ya maisha kiroho kwa wagonjwa na maskini. Wajumbe, 50 kutoka nje ya India wameshiriki na wajumbe wa ndani walikuwa ni 200, maadhimisho ambayo kwa Majimbo mengi yamefanyika Jumapili, tarehe 10 Februari 2019, ili kutoa nafasi kwa waamini wengi zaidi kushiriki katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani, 2019.

Siku ya Wagonjwa India

 

 

11 February 2019, 09:24