Tafuta

Vatican News
Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani 2019: Mshikamano wa upendo wa kidugu na wagonjwa! Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani 2019: Mshikamano wa upendo wa kidugu na wagonjwa!  (ANSA)

Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani 2019: Mshikamano wa kidugu!

Kardinali Peter Turkson, anaongoza ujumbe wa mshikamano na udugu kutoka Vatican katika maadhimisho ya Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani kwa mwaka 2019 huko Calcutta, nchini India kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mmepata bure, toeni bure”. Mt. 10:8. Maadhimisho haya yanafanyika nchini India ambako kuna changamoto kubwa ya umaskini, magonjwa, ujinga na ubaguzi wa kila aina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, kuanzia tarehe 8-12 Februari 2019 anaongoza ujumbe wa mshikamano na udugu kutoka Vatican katika maadhimisho ya Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani kwa mwaka 2019 huko Calcutta, nchini India kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mmepata bure, toeni bure”. Mt. 10:8. Maadhimisho haya yanafanyika nchini India ambako kuna changamoto kubwa ya umaskini, magonjwa, ujinga na ubaguzi wa kila aina.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha mshikamano wake wa upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama ilivyokuwa kwa Mama Theresa wa Calcutta, shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini. Ni “mwanamke wa shoka” aliyethubutu kupenda wasiopendeka”.  Mama Kanisa kwa kutambua sadaka na majitoleo yake, tarehe 4 Septemba 2016, Baba Mtakatifu Francisko akamtangaza kuwa Mtakatifu. Hata leo hii, watawa wake, wanaendelea kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili kwa watu sehemu mbali mbali za dunia, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha sadaka na majitoleo yao kwa maskini, kama ilivyotokea huko Yemen, hivi karibuni.

Kardinali Peter Turkson pamoja na ujumbe wake huko India, anashiriki katika kongamano la shughuli za kichungaji kitaalimungu mintarafu sekta ya afya katika mwanga wa Mwongozo wa Wafanyakazi katika Sekta ya Afya uliozinduliwa rasmi, Mwezi Septemba 2017. Kimsingi Mwongozo huu unakazia umuhimu wa wafanyakazi katika sekta ya afya kuhakikisha kwamba wanatumia: akili, ujuzi, maarifa na weledi wao kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa; wawaoneshe huruma na upendo na kamwe wasiwageuze kuwa ni kichokoo cha majaribio ya kisayansi!

Wafanyakazi hawa wawaonjeshe: huruma na upendo; wawapatie kipaumbele wanachohitaji kwa uwepo na huduma yao makini; wawaelewe na kushirikishana; wawaonjeshe wagonjwa uvumilivu na utu wema sanjari na kukuza majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi na mafao ya mgonjwa mwenyewe! Kila mgonjwa anapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma na mapendo! Itakumbukwa kwamba, kwa mara ya kwanza kabisa, Siku ya Wagonjwa Duniani iliadhimishwa tarehe 11 Februari 1993, baada ya kuanzishwa rasmi na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1992, ili kuragibisha umuhimu wa huduma ya huruma na upendo kwa wagonjwa sehemu mbali mbali za dunia.

Mtakatifu Yohane Paulo II, alikazia pamoja na mambo mengine: majiundo endelevu na ya kina: kiroho, kimwili na kimaadili kwa wahudumu wa sekta ya afya kutoka katika taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki. Hizi ni siku za sala na tafakari kuhusu mateso na mahangaiko ya binadamu; mwaliko kwa waamini kumwangalia Kristo Yesu anayeendelea kuteseka kati ya ndugu zake maskini, wagonjwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Kardinali Turkson: Siku ya Wagonjwa India
07 February 2019, 15:17