Tafuta

Vatican News
Kardinali Pietro Parolin amewataka wafanyakazi wa Mahakama za Vatican kuzingatia haki na huruma katika shughuli zao! Kardinali Pietro Parolin amewataka wafanyakazi wa Mahakama za Vatican kuzingatia haki na huruma katika shughuli zao!  (Vatican Media)

Ufunguzi wa Mwaka wa Mahakama Vatican: haki na huruma!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, amewataka wadau katika Mahakama za Vatican kutenda kwa kuzingatia ukweli na haki; wanapotoa hukumu zao, wamwangalie Kristo Yesu, aliye Njia, Ukweli na Uzima, ili aweze kuwasaidia kutoa maamuzi yao na kuwabariki wanapotekeleza dhamana na wajibu huu nyeti katika maisha ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake wakati wa kufungua Mwaka wa Mahakama ya Vatican alikazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa kudumisha: umoja na uaminifu; kuendeleza mpango mkakati wa utume wa maisha ya ndoa na familia; kuimarisha umoja, ukarimu na upendo aminifu kwa watu wa ndoa, kwani Kanisa linataka kujielekeza zaidi kwa ajili ya kudumisha imani, afya na ustawi wa watu wa ndoa na familia!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi, tarehe 16 Februari 2019 amezindua Mwaka wa Mahakama ya Vatican kwa Ibada ya Misa Takatifu, iliyohudhuriwa na mahakimu, wanasheria, mawakili pamoja na wafanyakazi wa Mahakama za Vatican. Kardinali Parolin, amewataka wadau katika Mahakama za Vatican  kutenda kwa kuzingatia ukweli na haki; wanapotoa hukumu zao, wamwangalie Kristo Yesu, aliye Njia, Ukweli na Uzima, ili aweze kuwasaidia kutoa maamuzi yao na kuwabariki wanapotekeleza dhamana na wajibu huu nyeti katika maisha ya watu.

Wafanyakazi wa Mahakama wawe na mang’amuzi ya mazito ya kuweza kugundua sheria ipi inayohitajika na hatimaye, kuipatia tafsiri sahihi kwa kuzingatia haki na kweli inayofumbatwa katika huruma! Ili kuweza kufikia katika hatua hii, kuna haja ya kuzifahamu fika sheria, kanuni na taratibu za Mahakama ya Kanisa Katoliki. Kuna wakati ambapo hekima na busara ya kibinadamu inapaswa kupyaishwa kwa mwanga wa tunu msingi za Kiinjili, yaani haki inapaswa kuangaliwa kwa mwanga wa huruma.

Kardinali Parolin anasikitika kusema, leo hii kuna mwelekeo mkubwa wa watu kutaka kuvunjilia mbali sheria, taratibu na kanuni kana kwamba, ni mambo yaliyopitwa na wakati. Haya yanatokea pia hata katika maisha ya kiroho! Mwanadamu anataka kumweka Mungu pembezoni kabisa kwa maisha na vipaumbele vyake na matokeo yake ni kuongezeka kwa dhambi duniani. Katika hali na mzingira kama haya, Mama Kanisa anapenda kuwatangazia watu upendo, huruma na msamaha wa Mungu kama ulivyofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele.

Kwa hakika, Mwenyezi Mungu anataka kumkomboa mwanadamu kwa kuzingatia haki inayofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho. Heri za Mlimani ni muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Kristo Yesu, ni dira na mwanga katika maisha ya wafuasi wa Kristo. Haki inayoelezewa na Kristo Yesu katika mafundisho yake ni uaminifu kwa Mungu na jirani; tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu. Haki kwa Mungu na mwanadamu ni mambo msingi katika utekelezaji wa shughuli za Mahakama zinazojikita katika majadiliano ya upendo.

Parolin: Mahakama
19 February 2019, 15:04