Tafuta

Vatican News
Imegota miaka 6 tangu Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipong'atuka kutoka madarakani mwaka 2013 Imegota miaka 6 tangu Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipong'atuka kutoka madarakani mwaka 2013  (Vatican Media)

Papa Mstaafu Benedikto XVI: Miaka 6 iliyopita! Aliitikisa dunia!

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI baada ya kutafakari kwa kina, akaona alikuwa anaishiwa nguvu za kuweza kutekeleza majukumu haya kwa ufanisi mkuu. Hili ni tukio ambalo limeweka historia kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ni kiongozi ambaye amewashangaza sana walimwengu, kwani walidhani kwamba, ni mtu aliyekuwa na uchu wa madaraka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 11 Februari 2013, Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, (1858) sanjari na Kumbu kumbu ya Mkataba wa Lateran (1929), imegota miaka sita tangu Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipoamua kwa hiyari yake mwenyewe, kung’atuka kutoka madarakani kutokana na uzee pamoja na kuanza kuzorota kwa afya yake, ili kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine, kuendeleza dhamana na wajibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Huu ni wajibu unaofumbatwa katika utekelezaji wa majukumu haya kwa njia ya maadhimisho mbali mbali ya Mafumbo ya Kanisa, mikutano pamoja na hija za kitaifa na kimataifa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI baada ya kutafakari kwa kina, akaona alikuwa anaishiwa nguvu za kuweza kutekeleza majukumu haya kwa ufanisi mkuu. Hili ni tukio ambalo limeweka historia kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ni kiongozi ambaye amewashangaza sana walimwengu, kwani walidhani kwamba, ni mtu aliyekuwa na uchu wa madaraka!

Papa Mstaafu Benedikto XVI aliliongoza Kanisa kwa hekima na busara, akalitaka Kanisa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kuambata zaidi imani, matumaini na mapendo, mambo makuu yanayojionesha katika Nyaraka zake za Kitume. Aliwataka kwa namna ya pekee kabisa, viongozi kulisafisha Kanisa kutokana na kashfa mbali mbali, sakata ambalo limevaliwa njuga sasa na Baba Mtakatifu Francisko, yaani: nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo!

Tayari imekwisha undwa Kamati kuu itakayoratibu mkutano maalum wa Kanisa kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia utakaofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019. Mkutano huu utaongozwa na mambo makuu matatu: uwajibikaji, dhamana ya uwajibikaji; ukweli na uwazi. Ikumbukwe kwamba, mchakato huu ulianzishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa kukutana na kuzungumza na wahanga wa nyanyaso za kijinsia. Ilikuwa ni nafasi ya kusikiliza kwa makini, kusali, kuomboleza na hatimaye, kufanya maamuzi machungu katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliongoza katika kipindi cha majaribu magumu katika maisha na utume wake, lakini akasimama kidete, kwa imani na matumaini ili kuhakuhakikisha kwamba, Kanisa linayavuka mawimbi mazito ya bahari, kwa kumtegemea na kujiaminisha kwa Kristo Yesu. Alilitaka Kanisa kutambua na kuendeleza amana na utajiri wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ambao yeye binafsi aliushiriki kikamilifu! Kanisa linapaswa kuwa ni Sakramenti ya wokovu kwa watu wote, Neno la Mungu lipewe kipaumbele cha kwanza, na waamini waadhimishe mafumbo ya Kanisa kwa uelewa mpana zaidi. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akakazia kwa namna ya pekee zaidi, umuhimu wa Katekisimu ya Kanisa

Kanisa limeanzishwa na Kristo na linaendelea kuwepo ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Kumbe, Kanisa halina budi kuwa ni chombo cha utume wa kutangaza, kujenga na kudumisha Ufalme wa Mungu. Kama walivyowahi kusema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Kumbe, Kanisa linapaswa kuendelea kuwa ni chombo cha huduma na sauti ya maskini na wale wote wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu amaonesha mshikamano wa dhati na binadamu wote, changamoto na dhamana kwa Kanisa katika ulimwengu mamboleo! Kamwe, Kanisa lisiridhike na hali yake, kwani litaanza kujitafuta lenyewe na matokeo yake ni kumezwa na malimwengu.

Kanisa liwe ni chombo cha kuhamasisha upendo kwa Mungu na jirani. Ili kuweza kufikia utekelezaji wa dhamana na wajibu huu, kuna haja ya Kanisa kuendelea kujitakasa na kujitakatifuza. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, alilitaka Kanisa kujifunza kusimama kidete huku likiwa huru dhidi ya chachu za wanasiasa wanaotaka kulitumia kwa ajili ya mafao yao binafsi. Kanisa liwe ni chombo cha Ibada kwa Mwenyezi Mungu  na huduma kwa binadamu!

Andrea Monda, Mkurugenzi mkuu wa Gazeti la L’Osservatore Romano katika tahariri yake anasema, pengine, wengi wanamkumbuka zaidi Mtakatifu Yohane Paulo II na kusahau kwamba, hata Joseph Ratzinger amechangia sana katika mchakato wa utakatifu wa Yohane Paulo II katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kumheshimu na kumpongeza sana mtangulizi wake, Papa Mstaafu Benedikto XVI, Kiongozi mwenye busara, hekima na nguvu aliyethubutu kuleta mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa! Lakini kama ilivyo kwa baadhi ya watu, walitaka kumnyong’onyeza kwa sababu zao binafsi!

Lakini ukweli wa mambo utaendelea kushamiri katika historia ya maisha na utume wa Kanisa. Utashi wa kutaka kuleta mageuzi ndani ya Kanisa ni nguvu aliyoionesha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro! Kunahitajika ujasiri, hekima na busara, ikisukumwa na nguvu ya ndani, kuweza kuamua kukaa pembeni na kuendelea kusali kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa! Bravo, Papa Mstaafu Benedikto XVI! Endelea kulisindikiza Kanisa kwa sala, sadaka na tafakari zako!

B16 Kung'atuka madarakani
13 February 2019, 12:42