Cerca

Vatican News
Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Umuhimu wa utume wa Kanisa katika kutenda haki! Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Umuhimu wa utume wa Kanisa katika kutenda haki!  (AFP or licensors)

Mkutano Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Utume wa Kanisa

Ukweli na uwazi; toba na wongofu wa ndani ni mambo msingi katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Kanisa kwa kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuwalinda watoto wadogo, kumelifedhehesha sana mbele ya walimwengu, sasa ni wakati wa kujikita katika utume wake na kutenda haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Kanisa linapaswa kuonesha ujasiri kwa kusimama kidete kulinda na kutetea maisha na utume wake. Liwe tayari kuanzisha mfumo utakaolisaidia kurekebisha kasoro na mapungufu ya kibinadamu yaliyojitokeza kiasi cha kusababisha kashfa kama ilivyo wakati huu, kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Ukweli na uwazi; toba na wongofu wa ndani ni mambo msingi katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Kanisa kwa kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuwalinda watoto wadogo, kumelifedhehesha sana mbele ya walimwengu, sasa ni wakati wa kujikita katika utume wake na kutenda haki.

Hii ni sehemu ya hotuba elekezi iliyotolewa na Sr. Veronica Openibo SHCJ, kutoka Nigeria, Jumamosi, tarehe 23 Februari 2019, kwenye Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo. Sr. Veronica Openibo amejikita zaidi kuhusu ukweli na uwazi kama sehemu ya utume wa Kanisa. Ikumbukwe kwamba, Kanisa lina asili mbili: Asili ya Kimungu kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu na kwamba, Kanisa pia lina asili ya Kibinadamu kwa sababu linaendeshwa na binadamu wenye karama na mapungufu yao!

Huu ni wakati wa kusimama tena na kuendelea na safari kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema; kwa kuzingatia misingi ya ukweli na uwazi; toba na wongofu wa ndani pamoja na Kanisa kujiwekea sera na mikakati ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia imechafua maisha na utume wa Kanisa na kwa baadhi ya majimbo hasa nchini Marekani yamefilisika kwa sababu viongozi wakuu wa Kanisa hawakuwajibika barabara kuwalinda na kuwatetea watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Hiki ni kipindi cha kuchunguza dhamiri, ili kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata neema na huruma ya Mungu kama dira na mwongozo kuelekea utakatifu wa maisha. Amri za Mungu ziwe ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Mkutano huu ambao umewawezesha viongozi waandamizi wa Kanisa kukutana na kusikiliza shuhuda za nyanyaso za kijinsia iwe ni nafasi kwa Kanisa kushughulikia kashfa hii moja kwa moja kwa kujikita katika misingi ya ukweli, uwazi na ujasiri!

Ni wakati muafaka kwa Kanisa kuchunguza na hatimaye kuibuka na mbinu mkakati wa kichungaji kuhusu: uchu wa mali na madaraka pamoja na matumizi mabaya ya madaraka ndani ya Kanisa; ubaguzi wa kijinsia; nafasi na dhamana ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na kuanzisha protokali itakayoliwezesha Kanisa kusimamia misingi ya ukweli, uwazi na uwajibikaji. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ipo hata Barani Afrika na Asia; kuna kesi na dalili za nyanyaso za kijinsia kwenye seminari, nyumba za malezi na hata katika nyumba za kitawa! Ni wakati wa kufungua macho, ili kuona ukweli na kuufanyia kazi bila kuchelewa sana! Kashfa hizi zimewagusa watoto wadogo, Kanisa halina budi sasa kujikita katika misingi ya ukweli na uwazi; ili kuganga na kuponya pamoja na kuhakikisha kwamba, haki inatendeka na wahusika wanapata adhabu kadiri ya makosa yao.

Kanisa liwe na ujasiri wa kuzungumzia kashfa hii, liwe tayari kukiri makosa na udhaifu wake; kwa kujenga na kuimarisha maadili na utu wema. Mchakato wa utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za Kanisa kwa watuhumiwa uzingatiwe. Umaskini, ujinga, magonjwa na vita, visilifanye Kanisa Barani Afrika na Asia kudhani kwamba, liko salama dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Sheria ni msumeno, iwashughulikie watuhumiwa wote bila upendeleo wa cheo, umri au anapotoka mtu, kwa kutambua na kuguswa na madonda makubwa yaliyosababishwa na kashfa hizi.

Sr. Veronica Openibo anakaza kusema, sera na mbinu mkakati unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwanza kabisa ni kuwasikiliza na hatimaye, kuwasaidia wahanga wa nyanyaso za kijinsia. Masuala ya kijinsia yajadiliwe katika ukweli na uwazi pamoja na kusaidia malezi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya. Biashara ya binadamu na viungo vyake, utumwa mamboleo pamoja na utalii wa ngono ni kati ya changamoto nzito kwa wakati huu. Yote haya ni mambo yanayoathiri utu, heshima na haki msingi za binadamu, kumbe, yanapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa.

Malezi na majiundo katika hatua mbali mbali za maisha ya kipadre na kitawa yapewe msisitizo wa pekee! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, wito wa kwanza ni utakatifu wa maisha. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, mapadre na watawa tangu mwanzo wanafundwa kutafuta na kukumbatia utakatifu wa maisha na utu wema. Uchaguzi na hatimaye, uteuzi wa majandokasisi kuelekea Daraja Takatifu uwe makini, vinginevyo huo ndio mwanzo wa kuwa na viongozi waliokengeuka na kutopea katika dhambi.

Sr. Veronica Openibo anahitimisha kwa kusema, Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaoongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika Utume” itakuwa ni nafasi ya kufanya tafakari ya Kibiblia na Kitaalimungu; katekesi makini pamoja na matendo ya ukarimu, yatakayolisaidia Kanisa kuinjilishwa tena, ili kupata ari na nguvu ya kushuhudia upendo ule wa kwanza kwa Kristo: aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili hatimaye, kuinjilisha kwa kujikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo makini cha imani tendaji inayobubujika kutoka katika tafakari makini ya Neno la Mungu. Lengo ni kuamsha tena ari na moyo wa kimisionari, ili kupyaisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayotekelezwa na Mama Kanisa.

Sr. Veronica Openibo anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa ujasiri wake katika kushughulikia kashfa ya nyanyaso za kijinsia katika ukweli na uwazi; kwa ari na moyo mkuu. Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, linamshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwapatia nafasi ya kuchangia mawazo, uzoefu na matarajio yao halali katika mkutano huu.

Sr. Veronica: Ukweli na Uwazi

 

 

23 February 2019, 12:41