Tafuta

Vatican News
Mkutano wa Kanisa Kuhusu Kuwalinda Watoto Wadogo: Vipaumbele vinavyopaswa kutekelezwa! Mkutano wa Kanisa Kuhusu Kuwalinda Watoto Wadogo: Vipaumbele vinavyopaswa kutekelezwa! 

Mkutano Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Vipaumbele vyabainishwa!

Jitihada hizi hazina budi kuwasilishwa kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kwa haraka iwezekanavyo, katika ukweli, ukamilifu na ufafanuzi makini kadiri inavyowezekana! Wajumbe wa mkutano huu kutoka Sekretarieti kuu, wakati wa kuchangia mawazo yao, wameonesha nia ya kutaka kufuata nyayo za Baba Mtakatifu Francisko katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuandika “Motu Proprio” yaani “Barua Binafsi” kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo. Waraka huu, utasindikizwa na Sheria Mpya ya Vatican mintarafu mada hii ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa litachapisha “Vademecum” yaani “Mwongozo” na kwamba, Baba Mtakatifu ameonesha nia ya kuunda “Kikosi Kazi cha wataalam na Mabingwa” kitakachoyasaidia Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia kukabiliana na changamoto ya nyanyaso za kijinsia.

Haya ndiyo mambo makuu ambayo Kanisa limeamua kuyafanyia kazi kama sehemu ya utekelezaji wa mambo msingi yaliyogusiwa kwenye Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo uliokuwa unafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019 kwa uwepo na ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu Francisko! Jumatatu, tarehe 25 Februari 2019 kumefanyika mkutano wa ufuatiliaji na hatimaye, utekelezaji wa maazimio haya! Huu ni mkutano ambao umewahusisha viongozi waandamizi kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na Kamati Kuu ya Mkutano Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo.

Padre Federico Lombardi, SJ., Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger/Benedikto XVI, ambaye pia ni Mratibu wa Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo ameelezea mambo msingi yanayopaswa kufanyiwa kazi mara moja bila kuchelewa kama ilivyoshuhudiwa na msukumo wa pekee kutoka kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Katika muktadha huu, sheria, kanuni na taratibu mbali mbali zimebainishwa na kwamba, huu ni msingi unaoweza kusaidia kuandika Nyaraka na kuunda Kikosi Kazi, kwa ajili ya kupambana na nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Jitihada hizi hazina budi kuwasilishwa kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kwa haraka iwezekanavyo, katika ukweli, ukamilifu na ufafanuzi makini kadiri inavyowezekana! Wajumbe wa mkutano huu kutoka Sekretarieti kuu, wakati wa kuchangia mawazo yao, wameonesha nia ya kutaka kufuata nyayo za Baba Mtakatifu Francisko katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Jambo la msingi ni Kanisa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuwasikiliza waathirika wa nyanyaso za kijinsia.

Pili, waamini walei wahusishwe kikamilifu, kwa kuwapatia malezi na majiundo makini; kwa kuwasaidia kupata nyenzo za kuzuia nyanyaso za kijinsia katika medani mbali mbali za maisha pamoja na kufuata ushauri wa wataalam waliotaulimiwa katika masuala haya! Tatu, viongozi hawa wameamua kufanya mkutano wa Sekretarieti kuu ya Vatican ili kupembua kwa kina na mapana utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa mintarafu “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”.

Utuatiliaji Nyanyaso
26 February 2019, 11:37