Tafuta

Vatican News
Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Ibada ya Toba na Wongofu wa ndani! Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Ibada ya Toba na Wongofu wa ndani!  (Vatican Media)

Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Toba na wongofu

Kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, hata wao viongozi wa Kanisa wameomba na kupata sehemu ya urithi wao kama wahudumu wa watu wa Mungu na kwa ajili ya wokovu wa roho zao, kwa matumaini kwamba, wataweza kutekeleza dhamana na utume wao wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu pamoja na kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wajumbe wa Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo ulioanza tarehe 21 – 24 Februari, walipata nafasi, Jumamosi, jioni, tarehe 23 Februari 2019 kufanya Ibada ya Toba iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko na baadaye mahubiri yakayotolewa na Askofu mkuu Philip Naameh, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana. Katika mahubiri yake, amejikita zaidi katika Injili ya Baba mwenye huruma kama inavyosimuliwa na Luka kuhusu Mwana Mpotevu! Pengine kwa Maaskofu hii imekuwa ni Injili ambayo wameitangaza mara nyingi katika maisha na utume wao; kwa kuwataka wadhambi kutubu na kumwongokea Mungu, lakini kwa kusahau kwamba, wao wanapaswa kuwa ni viongozi wa kwanza kutekeleza dhamana na wajibu wao kama wana wapotevu!

Kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, hata wao viongozi wa Kanisa wameomba na kupata sehemu ya urithi wao kama wahudumu wa watu wa Mungu na kwa ajili ya wokovu wa roho zao, kwa matumaini kwamba, wataweza kutekeleza dhamana na utume wao wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu pamoja na kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu! Lakini kwa bahati mbaya, viongozi wa Kanisa wameshindwa kusimamia haki kwa kuangalia kwa macho makavu giza lililokuwa linaandama maisha na utume wa Kanisa, kiasi hata cha kusaliti wajibu na dhamana yao ndani ya Kanisa, pale ambapo baadhi ya watu walitishia ustawi na maendeleo ya Kanisa.

Askofu mkuu Philip Naameh anasikitika kusema, ni kutokana na changamoto hizi, baadhi ya viongozi wa Kanisa wakajikuta wakipindisha ukweli, ili kulindana kama Maaskofu na kusahau wajibu unaowaunganisha kidugu! Kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, Kanisa likajikuta likipoteza heshima yake mbele ya watu wa Mataifa. Huu ndio mwanzo wa kuwa wanyenyekevu na kuanza kuchakarika kama kawaida bila ya kutafuta upendeleo wa aina yoyote ile. Kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, akatambua makosa yake, akaungama mbele ya Baba mwenye huruma na kumwambia yale yalimsibu katika maisha na kwamba, alikuwa tayari kukubali adhabu yake, ili mambo yaishe.

Lakini, Baba mwenye huruma, anapata furaha ya hali ya juu anapomwona Mwanaye aliyekuwa amepotea, anarejea nyumbani, yule aliyekuwa amekufa sasa amefufuka. Na huu unakuwa ni mwanzo wa furaha ya Injili! Tukio ambalo lilisaidia hata kuleta upatanisho wa kidugu hata na kaka mkubwa aliyekuwa hataki kuingia ndani kutokana na mwelekeo uliooneshwa na Baba mwenye huruma. Hii ndiyo changamoto ambayo Maaskofu na wakuu wa Mashirika wanapaswa kuifanyia kazi, ili kweli waweze kuwa ni watoto wapendwa wa Baba wa milele, kwa kuendelea kuwajibika kikamilifu katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia na ukatili kwa watoto wadogo, kwa kujikita katika ukweli na uwazi. Lakini hii ni njia ndefu na yenye magumu yake.

Mafanikio yanaweza kupatikana, ikiwa kama watakuwa na ujasiri wa kubadilisha mahusiano na mafungamano kati yao; kwa kuondoa vikwazo na changamoto wanazokumbana nazo pamoja na kujipatanisha na ndugu zao katika Kristo; ili kurejesha tena imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kwa njia hii, kazi kubwa mbele ya Maaskofu ni kurejesha tena mahusiano bora na waamini walei, ili kushirikiana katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Ibada ya Toba

 

24 February 2019, 15:19