Cerca

Vatican News
Familia ya Mungu nchini Ufaransa, Jumapili tarehe 20 Januari 2019 inaandamana kupinga utamaduni wa kifo! Familia ya Mungu nchini Ufaransa Jumapili tarehe 20 Januari 2019 inaandamana kupinga utamaduni wa kifo!  (AFP or licensors)

Ufaransa kuandamana kupinga utamaduni wa kifo, 20 Jan. 2019!

Familia ya Mungu nchini Ufaransa Jumapili, tarehe 20 Januari 2019 itafanya maandamano makubwa ili kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, tukio ambalo linaungwa mkono na Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Ventura, Balozi wa Vatican nchini Ufaransa anayewataka waamini kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maisha ya binadamu ni matakatifu tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti yanapomfika mtu kadiri ya mapenzi ya Mungu. Mwenyezi Mungu ni asili na kikomo cha maisha ya mwanadamu. Hakuna mazingira yoyote yale yanayoweza kujitwalia haki na mamlaka ya kuharibu zawadi ya uhai. Mama Kanisa anafundisha na kukazia kwamba, uhai wa binadamu sharti uheshimiwe na ulindwe na kwamba, uhai ni sehemu muhimu sana ya haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, leo hii kuna wimbi kubwa la utamaduni wa kifo unaoendelea kuwanyemelea watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia!, Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Majiundo ya madaktari, kimsingi yanajikita katika: maisha ya kiroho, kiutu na maadili ya kibaiolojia bila kusahau sheria-Kanuni maadili, utu wema; uhuru na dhamiri nyofu. Ni katika muktadha huu, familia ya Mungu nchini Ufaransa, Jumapili, tarehe 20 Januari 2019 majira ya mchana, itafanya maandamano makubwa ili kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. 

Tukio ambalo linaungwa mkono na Baba Mtakatifu katika ujumbe mfupi ulioandikwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Luigi Ventura, Balozi wa Vatican nchini Ufaransa. Baba Mtakatifu katika ujumbe huo anasema, kuna haja ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai. Waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda na Injili ya uhai, kwa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha: uhai, utu na heshima ya binadamu. Utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba, zinazoungwa mkono kisheria ni juhudi za kutaka kubeza utu na heshima ya binadamu pamoja na dhamiri nyofu. Maandamano haya yanapania kuwa ni changamoto kwa familia ya Mungu nchini Ufaransa kuwa wakarimu kwa Injili ya uhai sanjari na kuheshimu dhamiri nyofu!

Wanawake
14 January 2019, 13:48