Cerca

Vatican News
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia linafanya mkutano kuhusu mafundisho tanzu ya Kanisa: Imani na Maadili! Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia linafanya mkutano kuhusu mafundisho tanzu ya Kanisa: Imani na Maadili! 

Tume za Mafundisho Tanzu ya Kanisa Barani Asia zinakutana!

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, kuanzia tarehe 15-18 Januari 2019 linafanya mkutano unaowashirikisha wenyeviti wa Tume za Mafundisho Tanzu ya Kanisa kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Asia. Kardinali Luis Francisco Ladaria, anaongoza ujumbe kutoka katika Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, kuanzia tarehe 15-18 Januari 2019 linafanya mkutano unaowashirikisha wenyeviti wa Tume za Mafundisho Tanzu ya Kanisa kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Asia. Kardinali Luis Francisco Ladaria, anaongoza ujumbe kutoka katika Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Itakumbukwa kwamba, tarehe 23 Februari 1967, Mtakatifu Paulo VI aliagiza Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kuanzisha Tume za Mafundisho Tanzu ya Kanisa, kama chombo cha huduma kwa Baraza na Maaskofu wenyewe mintarafu masuala yanayohusu imani na maadili.

Katika maelezo yake, Mtakatifu Paulo VI alisema, ikiwa kama tatizo hili la kichungaji ni kubwa kwa tume hizi za Maaskofu, basi suala hili linaweza kupelekwa kwenye Tume nyingine kwa ufafanuzi zaidi. Kunako mwaka 1982, umoja na ushirikiano wa kidugu kati ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa pamoja na Tume za Mafundisho Tanzu ya Kanisa kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki uliimarishwa zaidi kwa wakati ule na Kardinali Joseph Ratzinger ambaye baadaye, alichaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kardinali Ratzinger alitaka wenyeviti wa Tume hizi kukutana mara kwa mara katika ngazi ya mabara kwa kuwahusisha wajumbe kutoka Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, ili kuweza kutafuta suluhu ya pamoja kwa kuzingatia mipaka, dhamana na wajibu wa kila upande. Tangu wakati huo, mikutano kama hii imeadhimishwa sehemu mbali mbali za dunia. Kwa wenyekiti kutoka Amerika ya Kusini, walikutana huko Bogotà kunako mwaka 1984; Bara la Afrika, huko Kinshasa, DRC., mwaka 1987; Bara la Ulaya, huko Vienna, mwaka 1989; Barani Asia, huko Hong Kong kunako mwaka 1993.

Mzunguko wa pili ulianza kunako mwaka 1993 na mkutano wa pili kwa Amerika ya Kusini ukafanyika huko Guadalajara. Mkutano wa Amerika ya Kaskazini uliadhimishwa huko San Francisco kunako mwaka 1999. Na hivi karibuni, mkutano wa Bara la Afrika uliadhimishwa huko Dar Es Salam kunako mwaka 2009 na kwa Bara la Ulaya mkutano huu ukafanyika kunako mwaka 2015 huko Esztergom-Budapest. Kumbe, ni kutokana na ushirikiano na mshikamano kati ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia umeandaliwa huko Bangkok, nchini Thailand, kwa lengo la Baraza kutaka kuyasaidia Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake katika kulinda, kuendeleza na kudumisha Mafundisho Tanzu ya Kanisa, kwa kupembua kwa kina na mapana changamoto za imani na maadili zinazoitatiza familia ya Mungu Barani Asia.

Baraq la Asia
12 January 2019, 15:19