Tafuta

Vatican News
Kardinali Pietro Patolin anawataka waamini kuwa ni mashuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Kardinali Pietro Patolin anawataka waamini kuwa ni mashuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! 

Kardinali Parolini: Waonesheni jirani zenu imani na upendo!

Wakristo wawe mashuhuda hai kwa jirani ili kumwona Kristo Yesu katika maisha yao, kielelezo cha imani inayofumbatwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Wakristo wanapaswa kuwa ni alama hai itakayowawezesha wengine kuuona wokovu na kupata upendo wa kweli unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maisha ya Mkristo yanapaswa kuwa ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko, utakaowawezesha jirani kumwona Kristo Yesu katika maisha ya waamini, kielelezo cha imani inayofumbatwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Wakristo wanapaswa kuwa ni alama hai itakayowawezesha wengine kuuona wokovu na kupata upendo wa kweli unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa tarehe 4 Januari 2019 na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Mwaka mpya 2019 kwa ajili ya wafanyakazi wa Vatican kwenye eneo la viwanda mjini Vatican. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema, Ukristo kabla ya kuwa dini inayojikita katika kanuni maadili na utu wema, ni mchakato wa upendo unaomkutanisha mwamini na Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, kiini cha imani ya Kikristo.

Hata leo hii, Kristo Yesu anaendelea kufanya safari ya kukutana na waja wake katika: Neno, Sakramenti, lakini zaidi katika jirani maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanamkaribisha Kristo Yesu katika mazingira ya maisha ya familia zao; kwa kutubu na kumwongokea Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa, tayari kuanza maisha mapya na kutembea katika mwanga wa Kristo Yesu aliyezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Kama ilivyokuwa kwa Yohane Mbatizaji, kumtambulisha Yesu kwa Wafuasi wake kama Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu, ni wajibu pia kwa Wakristo kuhakikisha kwamba, wanamtambulisha Kristo Yesu kama sehemu ya ushuhuda wa maisha na utume wao. Kristo Yesu apewe kipaumbele cha kwanza, licha ya udhaifu na mapungufu yanayoweza kujionesha katika maisha ya waamini! Lakini, ikumbukwe kwamba, daima, mwamini anayo kiu ya kutaka kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yake, ili kuonja upendo wa dhati unaokata kiu ya maisha!

Kardinali Parolin anakaza kusema, upendo wa Kristo ni imara na thabiti na kwamba, Kristo anatambua kiu kubwa ya upendo iliyoko moyoni mwa mwanadamu. Mwamini kwa kutambua kwamba, anathaminiwa na kupendwa na Kristo Yesu, anaweza kuwa kweli ni chombo na shuhuda wa upendo wa Mungu kwa jirani zake, kwa kuwaonesha wengine uwepo endelevu wa Kristo katika maisha yao!

Ushuhuda wa kwanza, unapaswa kujikita katika maisha ya kifamilia, kati ya marafiki, mahali pa kazi na katika medani mbali mbali za maisha! Hii ni changamoto pevu na endelevu kutokana na ubinafsi, uchoyo na kiburi cha mwanadamu. Waamini wawe ni chachu ya ushuhuda wa Kristo utakaowawezesha watu kutubu na kumwongokea Mungu, ili hatimaye, hata wao, kuweza kujiunga na umati mkubwa wa waamini katika kumshuhudia Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai! Mwishoni, wafanyakazi wamemshukuru Kardinali Pietro Parolin, anayeendelea kuimarisha ushuhuda wa imani katika eneo la kazi hali ambayo inakuza umoja, urafiki na udugu sehemu za kazi, kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo!

Parolin: Ushuhuda wa amini

 

 

05 January 2019, 09:56