Cerca

Vatican News
Shirika la Mtakatifu Gaetano linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu Mashemasi wa Kudumu walipopewa Daraja! Shirika la Mtakatifu Gaetano linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu Mashemasi wa kudumu walipopewa Daraja!  (ANSA)

Jubilei ya Miaka 50 ya Mashemasi wa Kudumu: Kanisa Katoliki

Papa Francisko analipongeza Jimbo kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu Mashemasi Saba wa kudumu kutoka Shirika la Mtakatifu Gaetano walipopewa Daraja ya Ushemasi wa Kudumu. Papa anapenda kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa matunda ya kazi ya mikono ya Mashemasi hawa wa kudumu, mintarafu mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuna makundi mawili ya Mashemasi ndani ya Kanisa. Kuna Mashemasi wa mpito kuelekea Daraja Takatifu la Upadre na kuna Mashemasi wa kudumu ambao wengi wao ni watu wa familia, lakini wanajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa kadiri ya Sheria, Taratibu na Kanuni za Kanisa Katoliki, lakini zaidi ni watu wa huduma ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili.

Huduma ya Sakramenti ya Daraja Takatifu tangu mwanzo, imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Uaskofu ambao ni utimilifu wa Sakramenti ya Daraja; Upadre na Ushemasi. Kumbe, Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na Mapadre. Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo kwa kupewa chapa isiyofutika na hufananishwa na Kristo aliyejifanya “Shemasi” yaani mtumishi wa wote.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu Beniamino Pizziol wa Jimbo Katoliki Vicenza, Italia, anapenda, kuchukua fursa hii, kulipongeza Jimbo kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu Mashemasi Saba wa kudumu kutoka Shirika la Mtakatifu Gaetano walipopewa Daraja ya Ushemasi wa Kudumu. Baba Mtakatifu anapenda kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa matunda ya kazi ya mikono ya Mashemasi hawa wa kudumu, mintarafu mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Changamoto ya Mashemasi wa kudumu ilipokelewa kwa moyo kitume na Mtumishi wa Mungu Padre Ottorino Zanon, kwa ushauri wa Askofu Rodolfi wakati ule. Hii ikawa ni fursa ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu kiroho na kimwili na kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji. Mashemasi wa kudumu, wakawa ni faraja kwa watoto yatima na vijana waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Mashemasi hawa wakajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na makuzi yao: kiroho na kimwili. Kimsingi, Mashemasi wa kudumu wamekuwa ni vyombo vya huduma ya Injili kwa Mungu na watu wake. Baba Mtakatifu anaendelea kuwakumbuka na kuwaombea wingi wa neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwa kutunza na ulinzi wa Bikira Maria wa Mlima Berico.

Mashemasi ni wahudumu wakuu wakati wa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, hasa wakati wa Ibada ya Misa Takatifu. Mashemasi wanaweza kusimamia na kubariki Ndoa Takatifu. Ni wahudumu wa Neno kwa kutangaza, kuhubiri na kulishuhudia katika huduma mbali mbali za upendo. Dhana ya Mashemasi wa kudumu, ambao kimsingi wanapewa Ushemasi wa huduma kadiri ya mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Barani Afrika ni wachache sana, lakini kazi ya huduma kwa kiasi kikubwa inatekelezwa na Makatekista.

Parolin: Mashemasi wa Kudumu
22 January 2019, 09:21