Cerca

Vatican News
Papa Francisko anaendelea kujipambua kuwa mtetezi wa: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Papa Francisko anaendelea kujipambanua kuwa mtetezi wa: utu, heshima na haki msingi za binadamu. 

Papa Francisko ni mtetezi wa utu, heshima na haki msingi za watu

Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Haya ni mambo ambayo yamepewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu kusitishwa kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na Miaka 70 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Balozi Georrios F. Poulides kutoka Cyprus, Dekano wa Mabalozi na wawakilishi wa nchi na mashirika mbali mbali ya kimataifa mjini Vatican katika salam zake kwa Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 7 Januari 2019, amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Haya ni mambo ambayo yamepewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu kusitishwa kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na Miaka 70 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu. Lengo ni kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika: haki, amani na uhuru wa kweli.

Balozi Georrios F. Poulides anakiri kwamba, katika kipindi cha miaka 70 iliyopita kuna hatua kubwa imepigwa na Jumuiya ya Kimataifa katika kulinda haki msingi za binadamu, lakini bado kuna haja ya kusimama kidete, ili kupambana na baa la njaa, umaskini na ujinga duniani; vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; mifumo mipya ya utumwa mamboleo pamoja na kuhakikisha kwamba, uhuru wa kuabudu unapewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa. Athari za mabadiliko ya tabianchi, bado ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa, bila kusahau utengenezaji, ulimbikizaji na tishio la matumizi ya silaha za kinyuklia.

Balozi Poulides anasema, Baba Mtakatifu amekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta sera na mbinu mkakati, utakaosaidia kuleta suluhu ya matatizo na changamoto zinazomwandama mtu mzima: kiroho na kimwili; daima, utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yakipewa msukumo wa pekee. Hapa, Kanisa linaendelea kuragibisha maendeleo fungamani ya binadamu, ili kuweza kukabiliana kikamilifu na changamoto zinazojitokeza katika medani mbali mbali za maisha, lakini zaidi katika maisha ya kiroho na kijamii, ili hatimaye, kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote.

Ili kweli Jumuiya ya Kimataifa iweze kufikia malengo haya, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; umoja, udugu, ukarimu na mshikamano wa dhati, kama njia ya kupambana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine, utamaduni ambao umewatumbukiza watu wengi katika ulaji wa kupindukia sanjari na utamaduni wa kifo. Wazee, wagonjwa, maskini na wanyonge ndani ya jamii hawana tena nafasi, kiasi cha kuonekana kana kwamba ni mizigo!

Kadiri ya mwono sahihi wa Baba Mtakatifu, Jamii inapaswa kuwalinda na kuwategemeza maskini, wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto kubwa inayoendelea kutolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji duniani. Kanisa katika sera na mikakati yake ya huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maluum linakazia umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwakirimia hifadhi, usalama na utulivu! Hija za kitume za Baba Mtakatifu Francisko huko Chile na Perù kwa mwaka 2018 zilijikita zaidi katika utunzaji wa mazingira nyumba ya wote; umuhimu wa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu pamoja na kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii; uinjilishaji na utamadunisho.

Balozi Poulides anaendelea kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kujielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene unaofumbatwa katika vipaumbele vya maisha ya mwanadamu, kwa kuendeleza majadiliano, haki na upatanisho, kama ilivyojitokeza katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni; mwaliko ukiwa ni Wakristo kuendelea kujikita katika umoja unaofumbatwa katika utofauti. Hija za kichungaji nchini Lithuania, Letvia na Estonia zililenga kujenga umoja wa Kanisa katika utofauti wake, kwa kujikita katika majadiliano ya kiekumene. Baba Mtakatifu amekuwa akitoa kipaumbele cha kwanza kwa mateso na mahangaiko ya familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati, kiasi cha kulaani ukimya unaoendelea kuonesha na Jumuiya ya Kimataifa kuhusu vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo huko Mashariki ya kati.

 

Tarehe 7 Julai 2018 ilikuwa ni Siku ya Kiekumene: ili kusali na kutafakari juu ya mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Hawa ni waamini wanaolazimika kuyakimbia makazi na nchi yao kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hili ni tukio la kiekumene ambalo limeacha chapa ya kudumu katika ujenzi wa umoja na udugu wa Wakristo huko Mashariki ya kati. Balozi Georrios F. Poulides anakaza kusema, Kanisa limeendelea kuwekeza katika Injili ya matumaini kwa vijana kwa njia ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018. Hii imekuwa ni fursa kwa Kanisa kujenga na kudumisha sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuambatana na vijana katika maisha yao.

Kanisa pia limeendelea kuzamisha mizizi ya maisha na utume wake katika Injili ya familia kwa kuadhimisha Siku ya IX ya Familia Duniani, huko Ireland, maadhimisho ambayo yalipania kuwa ni chemchemi ya furaha ya Injili ya familia kwa walimwengu, kwa kumshukuru Mungu kwa kuwajalia wanadamu uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia unaofumbatwa katika upendo wa dhati kati ya bwana na bibi na wala si vinginevyo. Vijana na wazee wanapaswa kujenga jukwaa linalowakutanisha mintarafu utu na heshima ya binadamu.

Januari mwaka 2019, Panama ni mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani, itakayowashirikisha vijana kutoka kila sehemu ya dunia. Ni muda wa kutafakari vipaumbele vya maisha na utume wa vijana, changamoto, matatizo na fursa walizo nazo kama mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili. Balozi Georrios F. Poulides anahitimisha hotuba yake kwa Baba Mtakatifu kwa kusema, Jamii inapaswa kujenga utamaduni wa kuwapenda na kuwaheshimu vijana; na kuendelea kuwasaidia kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kuheshimu na kuthamini utu wa binadamu na haki zake msingi; daima mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza.

Dekano wa Mabalozi Vatican
08 January 2019, 09:35