Cerca

Vatican News
Kardinali Jean Lous Tauran katika maisha na utume wake, amechangia sana mchakato wa majadiliano ya kidini! Kardinali Jean Louis Tauran katika maisha na utume wake, amechangia sana mchakato wa majadiliano ya kidini!  (� Vatican Media)

Mchakato wa majadiliano ya kidini: 2018-2019: Umoja na Udugu

Katika maisha na utume wake, Kardinali Jean Louis Tauran, alijitahidi kujenga umoja na udugu; hali ya kuheshimiana na kuthaminiana kati ya Wakristo na Waislam, juhudi zilizopewa kipaumbele cha pekee wakati wa uongozi wa Mtakatifu Paulo VI. Alijitahidi kukutana na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa dini ya Kiislam

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hayati Kardinali Jean Louis Tauran katika maisha yake kama Padre, Askofu na Kardinali alijitosa bila ya kujibakiza katika huduma kwa Kristo na Kanisa lake, akajisadaka katika mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Hadi dakika ya mwisho, hapo tarehe 5 Julai 2018 aliendelea kuwa ni chombo cha majadiliano ya kidini, sasa apumzike kwa amani!

Katika maisha na utume wake, Kardinali Jean Louis Tauran, alijitahidi kujenga umoja na udugu; hali ya kuheshimiana na kuthaminiana kati ya Wakristo na Waislam, juhudi zilizopewa kipaumbele cha pekee wakati wa uongozi wa Mtakatifu Paulo VI. Alijitahidi kukutana na kuzungumza na viongozi maarufu wa dini ya Kiislam kama vile Salman bin Abdulaziz Al Saud, mlinzi mkuu wa misikiti mitakatifu sana duniani yaani ile ya Mekka na Madina. Kifo cha Kardinali Tauran anasema Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, kimeacha pengo kubwa!

Viongozi wa kidini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, walituma salam za rambi rambi kutokana na msiba wa Kardinali Tauran. Baraza linaendelea na utume wake kwa njia ya ushuhuda wa urafiki na udugu; ili kusimama kidete kulinda, kutetea uhuru wa kuabudu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baraza la Kipapa kwa kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha Majadiliano ya Kidini na Kitamaduni (Kaiciid) kilichoanzishwa tarehe 26 Novemba 2012 kwa ushirikiano wa Falme za Kiarabu, Hispania, Australia na Vatican ikiwa ni nchi mwanachama mtazamaji na mwanzilishi, bado kinaendeleza majadiliano ya kidini na kitamaduni katika nchi mbali mbali ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku kuu ya Vesakh/Hanamatsuri kwa ajili ya waamini wa dini ya Kibudha, iliyoadhimishwa mwezi Mei, 2018, liliwataka waamini wa dini hizi mbili kusimama kidete kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi hadi vitokomee kabisa kutoka kwenye uso wa dunia! Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini katika ujumbe wake kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na ‘ID AL-FITR 1439 H. / 2018 A.D. lilikazia umuhimu wa kuachana na “dhana” ya mashindano yasiyokuwa na tija wala mashiko na kuanza kujielekeza zaidi ushirikiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku kuu ya “Deepaval” au “Diwali” yaani “Sherehe mwanga” kwa waamini wa dini ya Kihindu, liliwaalika: Wakristo na Wahindu kushikamana kwa ajili ya ulinzi wa watu wanyonge ndani ya jamii”. Kilele cha sherehe hii kilikuwa hapo tarehe 7 Novemba 2018. Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini anasema, maadhimisho ya sherehe hii kwa mwaka 2018, yalipania kusaidie kujenga na kudumisha moyo wa urafiki na udugu kati ya waamini; amani na furaha katika familia na jumuiya katika ujumla wake. Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limeendelea kushirikiana kwa karibu na waamini wa dini mbali mbali kwa njia ya majadiliano pamoja na kushirikishana: uzoefu na mang’amuzi mbali mbali ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kama ilivyojitokeza hivi karubu kwa kutembelewa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni ili kutathmini yaliyopita na kuweka sera na mikakati ya utekelezaji kwa siku za usoni.

Ujumbe wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini pia mwezi Desemba 2018 umeshiriki katika Jukwaa la Tano la Udumishaji wa Amani katika Jamii ya Kiislam, huko kwenye Falme za Kiarabu kwa wajumbe kukazia umuhimu wa kukuza na kudumisha tunu mbali mbali kwa ajili ya kudumisha amani duniani. Viongozi wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini walibahatika pia kutembelea na kuzungumza na viongozi wa serikali, kidini na Kanisa huko Morocco na Falme za Kiarabu na matunda ya juhudi hizi za majadiliano ya kidini ni hija za kitume za Baba Mtakatifu Francisko anazotarajia kuzitekeleza mwanzo mwa mwaka 2019. Lengo ni kuendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu; majadiliano na utamadunisho mambo msingi yanayoendelea kupewa kipaumbele cha pekee na Kanisa katika ulimwengu mamboleo!

Majadiliano ya Kidini
15 January 2019, 08:55