Tafuta

Vizingiti vya upatikanaji wa mafunzo vimewakilishwa na umasikini, migogoro ya kisilaha, uhamiaji na matukio ya mabadiliko ya tabianchi Vizingiti vya upatikanaji wa mafunzo vimewakilishwa na umasikini, migogoro ya kisilaha, uhamiaji na matukio ya mabadiliko ya tabianchi 

Askofu Mkuu Zani:Elimu ikikosekana,hakuna hata wakati endelevu!

Tarehe 24 Januari,kwa mara ya kwanza inaadhimishwa Siku ya Kimataifa ya Elimu,iliyopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako Desemba 2018. Katika fursa ya siku hii, Askofu Mkuu Vincenzo Zani,Rais wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki,anazungumzia juu ya changomoto za elimu katika nyakati za sasa, kati ya hizo ni suala la uhamiaji

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Tarehe 24 Januari 2019 ni siku ya Kimataifa ya elimu duniani ambayo inaadhimishwa kwa mara kwa kwanza tangu kupitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Desemba mwaka 2018 kwa kutambua umuhimu wa elimu katika kubadili dunia ili kuweza kufikia ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu. Katika fursa hiyo Askofu mkuu Vincenzo Zani, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki akihojiana na Vatican News anazungumzia juu ya mafunzo kwa wote na mafunzo ambayo yanatazama upande wa Mungu na maagano ya shule na familia. Kwa maana hiyo uchaguzi wa maadhimisho ya kimataifa ya siku ya Elimu ni mwafaka. Ni maadhimisho ya kimataifa ili kuhamasisha uelewa zaidi kwa serikali zote duniani na watu juu ya mada msingi wa elimu kwa watoto na kama zana ya kuweza kuondokana na umaskini.

Juhudi ya elimu ya pamoja,fungamani na yenye kuwa na mafao

Katika fursa ya kuadhimisha siku hii, Takwimu za Umoja wa Mataifa kwa upande zinaonyesha changamoto zilizopo, kwani watoto milioni 265 hawana uwezo wa kwenda shule; watoto milioni 617 ambao wangekuwa wamemaliza shule ya msingi hawawezi kusoma hata kuandika au kufanya hesabu rahisi ambapo chini ya asilimia 40 ya watoto wa kike waliopo kusini mwa jangwa la Sahara ndiyo wanahitimu elimu ya sekondari, huku watoto milioni 4 na watoto wakimbizi hawahudhurii shule kwa sababu ya mizozo. Kutokana na takwimu hizo ni wazi kabisa ya kwamba siku hii inatambua umuhimu wa kufanya jitihada zaidi ili kuhakikisha kweli panakuwapo na elimu kwa wote, yenye usawa na kiwango kama wanavyodhibitisha hilo kuwa watu wote wanaweza kweli kuwa na fursa za kupata elimu ambayo iwasaidie kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii na kuchangia maendeleo endelevu. Vizingiti vya upatikanaji wa mafunzo vimewakilishwa na umasikini, migogoro ya kisilaha, uhamiaji na matukio ya mabadiliko ya tabianchi.

Baba Mtakatifu anasema kuwa uhuru wa elimu unakomboa ukoloni wa kiitikadi

Siku ya Kimataifa ya Elimu kwa mara ya kwanza, imeungwa mkono hata na Baba Mtakatifu Francisko,mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana Jumapili tarehe 20 Januari 2019 ambapo amewatia moyo jitihada za UNESCO ili kuendeleza na kukuza amani duniani kwa njia ya elimu na  kuwa na matashi yake mema ili elimu hii iweze kuwa ni kwa ajili ya wote, fungamani  na inayotoa uhuru dhidi ya ukoloni wa kiitikadi. Katika kuzungumzia changamoto mpya na matukio ya juhudi za elimu, Askofu Mkuu Vincenzo Zani anathibitisha kuwa ni wazi kwamba ilikuwepo tayari Siku ya kimataifa ya wanafunzi na Siku ya walimu duniani, lakini haikuwapo bado siku ya Elimu kama utambuzi wa jitihada za dunia na kujivika elimu ili kuweza kutoa suluhisho la matatizo ya kijamii ya sasa na endelevu, kwa maana hiyo anapongeza uchaguzi wa siku hii na  kwamba ni ya busara! Siku kama hii inajikita katika sura nzima ya ulimwengu ambayo imejaa na tayari matatizo mengi hasa mivutano kwa ngazi ya utamaduni;watu kwa ngazi ya kuenea kwa teknolojia ambazo zinabadili kwa kina michakato ya elimu.

Elimu ni ahadi lazima kuvaliwa njuga

Ili kuweza kuwasaidia vijana wakabiliane na changamoto  kiukweli elimu ni ahadi ambayo lazima ivaliwe njuga.  Watoto kuacha shule na mapambano ya kutokujua kusoma na kuandika, bado ni changamoto kubwa ya elimu ambayo ni msingi, hivyo Askofu Mkuu Zani anathibitisha kwamba, mipango mikubwa ya miaka iliyopita ya  kupambana na ujinga, imeleta mafanikio makubwa, lakini wakati huo huo wa kupambana na matatizo hayo basi yanajitokeza mengine. Moja ya masuala makubwa leo hii ni yale ya uhamiaji, ambapo ni mamilioni na mamilioni sasa katika dunia, kati ya wakimbizi hao, waathirika hasa  ni watoto ambao hawana uwezekano wa kuendelea na mafunzo yao wakiwa wadogo. Kiukweli ni hali hasi ya kipeo kikubwa na matokeo haya lazima jitihada za elimu zitafuta namna ya kukabiliana.

Elimu inaweza kusaidia hata utamaduni wa makutano

Elimu inawezekana kusadia hata utamaduni wa makutano, kwa maana inapozungumzwa suala la elimu, Askofu Mkuu Zani anafikiria hatua nyingi zilizo patikana kwenye utume wa Baba Mtakatifu Francisko, hasa katika Wosia wake wa Laudato SI, pale anapothibitisha kuwa, elimu itakuwa na mafao iwapo  juhudi zake hazitakuwa tasa, kwa maana ya kusema kama hakuna kuhangaika hata kueneza mitindo mipya inayotazama thamani nyingi za kuwa binadamu, awali ya yote kuhusiana na maisha, jamii na mahusiano. Na zaidi Askofu Mkuu anafafanua kwamba,tunapogusa mada ya mahusiano ni kugusa kitovo kikuu cha maisha ya mtu,maisha ya utamaduni wa nchi, na kwa maana hiyo nchi ambayo haijikiti kuwekeza katika elimu,haitazami wakati wendelevu.

Wajibu ambao shule inapaswa ijikite ni kuwa na urafiki wa dhati na familia

Akiendelea kusisitiza juu ya maombi ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusiana na elimu kwa wote, Askofu Mkuu Zani amefikiria kwa haraka juu ya Waraka wa Populorum Progressio wa Mtakatifu Paulo VI ambapo ndani ya waraka huo ulikuwa na mambo matatu yenye nguvu ambayo yanahusisha katika mwendelezo wa utume wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, hata Baba Mtakatifu Francisko. Katika waraka huo unasema: leo hii tunateseka na ukosefu mkubwa wa mawazo. Ni mawazo yasiyo ya maana, mawazo yetu ya kijuu tu. Sisi tunaishi katika utamaduni wa baada ya ukweli na ambao kila uhakika ni sawa sawa na kinyume chake. Na jambo la pili na lenye nguvu sana, lilikuwa linahusu ubinadamu, kwa maana anasema kwamba hakuna ubinadamu wa kweli, ikiwa haujajifungulia kwa aliye juu mbinguni. Haiwezekani kumwelimisha mtu kikamilifu kama hauwezi kukubali kujifungulia kwa aliye juu kabisa. Na jambo la tatu kwa mujibu wa Mtakatifu Paulo VI alisema: sisi tunateseka kwa sababu ya ukosefu mkubwa wa udugu. Kwa maana hiyo, Askofu Mkuu anaongeza kusema, ni muhimu hata kwa ajili ya uwajibu ambao shule inapaswa ijikite kutafuta maagano au urafiki wa kweli na familia.

Elimu inaanzia ndani ya familia

Kwa kufafanua juu ya maagano au urafiki na familia, Askofu Mkuu Zani anathibitisha kwamba, eneo la kwanza la elimu ni katika familia. Hatua za kwanza ambazo zinasaidia mtu kuondokana na ubinafsi ili kuweza kujifunza mtindo, thamani,maadili, mwenendo na mambo mengine yanayofuata ni ndani ya familia. Inaonesha wazi unapofanya kazi katika shule za watoto wadogo na vyuo vikuu ya kwamba, vijana ambao nyuma yao hawana familia thabiti ni wale wanaoteseka zaidi. Kwa maana hiyo kile ambacho kimeweza kubainishwa daima kwa ngazi ya kawaida ya kimataifa, ndiyo pia hata kwa upande wa  Kanisa na Shughuli nzima ya Kanisa, kuwa msingi kwa sababu ni lazima kuunda mkakati kati ya taasisi mbalimbali za elimu lakini awali ya yote ni kuanzia ndani ya  familia na baadaye shuleni.

 

24 January 2019, 11:31