Tafuta

Vatican News
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Vietnam unaendelea kuimarika zaidi. Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Vietnam unaendelea kuimarika zaidi.  (AFP or licensors)

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Vietnam unaimarika!

Baba Mtakatifu Francisko anaitaka familia ya Mungu nchini Vietnam kumwilisha Injili ya Kristo katika maisha yao, kwa kuendelea kuwa ni wakristo na raia wema, tunu msingi za maisha ya kijumuiya! Vatican inaishukuru Serikali ya Vietnam kwa kushirikiana na Kanisa kiasi cha kuliwezesha kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Vietnam.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa saba wa kikosi kazi cha ushirikiano kati ya Vatican na Vietnam umehitimishwa hivi karibuni huko mjini Hanoi, Vietnam. Ujumbe wa Vietnam kwenye mkutano huu uliongozwa na Bwana Bui Thanh Son, Naibu Waziri wa mambo ya nchi za nje na ujumbe wa Vatican uliongozwa na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Wajumbe wa nchi hizi mbili wameridhishwa uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Vietnam sanjari na uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Vietnam na kwamba, kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na maboresho makubwa katika ngazi mbali mbali pamoja na viongozi wa pande hizi kutembeleana ili kubadilishana mawazo kama ilivyokuwa kwa Askofu mkuu Marek Zalewski, Balozi wa Vatican asiyekuwa mkazi alipotembelea Vietnam. Mahusiano haya yanaendelea kuimarishwa kwa njia ya majadiliano, ili kukuza hali ya kuaminiana na hatimaye, kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya nchi hizi mbili.

Uwakilishi wa Balozi wa Vatican asiyekuwa na makazi nchini Vietnam ni sehemu ya mbinu mkakati wa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili. Wajumbe wa mkutano wa kikosi kazi wamekazia ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko unaoitaka familia ya Mungu nchini Vietnam kuhakikisha kwamba, inajitahidi kumwilisha Injili ya Kristo katika maisha yao, kwa kuendelea kuwa ni wakristo na raia wema, tunu msingi za maisha ya kijumuiya! Vatican inaishukuru Serikali ya Vietnam kwa kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Kanisa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kiasi hata cha kuliwezesha Kanisa Katoliki nchini Vietnam kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini humo!

Kwa upande wake, Chama na Serikali ya Vietnam inaendelea kuboresha mchakato wa sera na mikakati yake ili kuimarisha zaidi: uhuru wa kuabudu pamoja na kuhakikisha kwamba, waamini wa dini mbali mbali nchini humo wanatekeleza sheria, taratibu na kanuni za nchi, ili waweze kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na ujenzi wa nchi yao katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kitaifa. Mkutano wa kikosi kazi, umefanyika katika mazingira ya amani na utulivu. Mkutano wa tisa, utafanyika mjini Vatican na kwamba, tarehe ya mkutano huu itapangwa kwa kutumia njia za kidiplomasia. Ujumbe wa Vatican uliokuwa unaongozwa na Monsinyo Antoine Camilleri kwa kuambatana na Askofu mkuu Joseph Vu Van Thien wa Jimbo kuu la Hanoi, ulipata nafasi ya kumtembelea Waziri mkuu wa Vietnam Bwana Nguyen Xuan Phuc pamoja viongozi wengine wakuu wa Serikali 

27 December 2018, 09:29