Tafuta

Vatican News
Sherehe ya Noeli ni kipindi cha mshikamano unaofumbatwa katika huduma! Sherehe ya Noeli ni kipindi cha mshikamano unaofumbatwa katika huduma!  (Vatican Media)

Mshikamano wa upendo unafumbatwa katika huduma!

Mshikamano wa upendo unaofumbatwa katika huduma ni sehemu ya utu wa binadamu unaopaswa kulindwa na kudumishwa, hasa kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa watoto ambao ni waathirika wakuu katika vita, kinzani na migogoro ya kijamii. Miradi hii inapania kutoa nafasi kwa watoto na vijana wakimbizi na wahamiaji kuendelea na mfumo wa elimu na malezi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tamasha la Muziki wa Noeli kwa Mwaka 2018 linakita ujumbe wake kwa wakimbizi na wahamiaji, hususan watoto wakimbizi wanaojikuta wakitumbukia katika majanga haya na hivyo kulazimika kuishi kwenye kambi za wakimbizi. Hawa ni watoto wanaokimbia nchi na familia zao, ili kutafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi kwa siku za usoni! Kwa bahati mbaya, watoto katika hali na mazingira kama haya, wengi wao hawana tena fursa ya kusonga mbele na elimu, ili kuwajengea uwezo wa kupambana na hali na mazingira yao kwa sasa na kwa siku za usoni!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Giuseppe Versaldi, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, alipokuwa anawatambulisha wasanii watakaoshiriki katika Tamasha la Muziki wa Noeli kwa Mwaka 2018 hapa mjini Vatican, kwa Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 14 Desemba 2018, kwa ajili ya kuchangia gharama za elimu, malezi na makuzi ya watoto na vijana. Miradi inayolengwa kwa mwaka huu ni ule wa Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurentes" iliyoanzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2013 baada ya uzoefu na mang'amuzi yake huko nchini Argentina na mradi wa pili ni ule wa Utume wa Shirika la Wadon Bosco nchini Uganda.

Mshikamano wa upendo unaofumbatwa katika huduma ni sehemu ya utu wa binadamu unaopaswa kulindwa na kudumishwa, hasa kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa watoto ambao ni waathirika wakuu katika vita, kinzani na migogoro ya kijamii. Miradi hii inapania pamoja na mambo mengine, kutoa nafasi kwa watoto na vijana wakimbizi na wahamiaji kuendelea na mfumo wa elimu na malezi, ili waweze kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi! Kardinali Giuseppe Versaldi anasema, lugha ya sanaa na muziki katika kipindi cha Noeli inajikita katika upendo na mshikamano, ili kushangilia ujio wa Mwana wa Mungu anayewachangamotisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni wasanii wa huruma na upendo wa Mungu kwa watoto wadogo!

Itakumbukwa kwamba, Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurentes" iliyoanzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2013 baada ya uzoefu na mang'amuzi yake huko nchini Argentina.  Kwa sasa taasisi hii, inapania kuendelea kuwapa vijana uzoefu na mang’amuzi ya kutambua na kushuhudia Injili ya maisha sanjari na kukuza elimu na malezi bora kwa vijana wa kizazi kipya nchini Iraq, mahali ambako kwa sasa kumegeuka kuwa ni uwanja wa vita, kinzani na misigano ya kila aina.

Miradi: Uganda & Iraq

 

 

14 December 2018, 14:25