Tafuta

Vatican News
Kardinali Parolin asema, ameguswa sana na ushuhuda wa imani ya Wakristo nchini Iraq. Kardinali Parolin asema, ameguswa sana na ushuhuda wa imani ya Wakristo nchini Iraq.  (ANSA)

Kardinali Parolin: Nimeguswa na ushuhuda wa Wakristo Iraq!

Ni watu wanaoteseka, wanaouwawa na kudhulumiwa kwa vile tu ni wafuasi wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu. Mababa wa Kanisa wanasema, hawa ni Wakristo wanaodhulumiwa ulimwenguni lakini wanapata faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kuendelea kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia mkesha wa Noeli, yaani tarehe 24 hadi tarehe 28 Desemba 2018 amekuwa na ziara ya kichungaji nchini Iraq kama kielelezo cha mshikamano wa umoja na udugu wa watoto wa Mungu, hasa katika eneo hili ambalo limegeuka kuwa ni uwanja wa vita. Kardinali Parolin na ujumbe wake, wametembelea taasisi mbali mbali zinazoendeshwa na kumilikiwa na Kanisa huko Iraq. Amekagua Kituo cha Familia Takatifu; Kituo cha Mtakatifu Paul, Kituo cha Radio ya Jimbo, Mar Behman pamoja na kutembelea Monasteri ya Sarah.

Akiwa Mosoul, Kardinali Parolin ametembelea Makanisa na kuzungumza na familia ya Mungu maeneo hayo! Uwanda wa Ninawi una historia ndefu katika maisha ya Wakristo, kielelezo cha imani na mateso mbali mbali. Hata leo hii watu wanaoishi katika eneo hili wamejaribiwa; wakasalitiwa hata na ndugu zao wenyewe; nyumba zao za ibada zikaharibiwa na kunajisiwa! Yote haya yalijitokeza kunako mwaka 2014 na huo ukawa ni mwanzo wa kuibuka kwa wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum.

Kardinali Parolin anasema, sasa familia ya Mungu nchini Iraq inahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni shuhuda na chombo cha haki, amani na upatanisho, daima ikijitahidi kujenga na kuimarisha umoja na udugu wa watoto wa Mungu! Katika mahojiano maalum na Vatican News, Kardinali Parolin anakiri kwamba amebahatika kutembelea Iraq na kushuhudia kwa macho yake mwenyewe imani ya Kanisa la mashuhuda wa Kristo.

Licha ya changamoto zote hizi, lakini bado ni Wakristo ambao wanapenda kushuhudia furaha ya Injili, ukarimu na shukrani hasa kwa Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekuwa karibu sana na Kanisa hili katika shida na mahangaiko yake. Imekuwa ni ziara ya kichungaji iliyojikita katika imani na matumaini katika maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho sanjari na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi kwa watu wa Mungu ambao wameteseka sana kwa vita na mipasuko ya kijamii, kisiasa na kidini.

Kardinali Parolin anakaza kusema, katika mahubiri yake amekazia sana umuhimu wa ushuhuda wa imani unaomwilishwa katika matendo kama kielelezo cha imani ya Kanisa la Kristo huko Mashariki ya Kati. Kanisa la Kiulimwengu linawashukuru na kuwapongeza Wakristo huko Mashariki ya Kati kwa uaminifu na udumifu wao licha ya changamoto mbali mbali wanazoendelea kukumbana nazo katika maisha yao. Ni watu wanaoteseka, wanaouwawa na kudhulumiwa kwa vile tu ni wafuasi wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu. Mababa wa Kanisa wanasema, hawa ni Wakristo wanaodhulumiwa ulimwenguni lakini wanapata faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kuendelea kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Kardinali Parolin anasema, ameguswa kwa namna ya pekee kwa kuona jinsi ambavyo Wakristo hawa wanavyoishi na kumwilisha imani yao katika matendo kama kielelezo cha kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu. Wanajisikia kuwa na “ile jeuri” ya kuwa Wakristo na wanataka kuendelea kuwa Wakristo licha ya madhulumu na nyanyaso wanazokumbana nazo katika safari ya maisha yao ya kila siku. Anasema, kila sehemu aliyotembelea na kukutana na familia ya Mungu nchini Iraq ilikuwa na mvuto na mashiko ya pekee, lakini zaidi, ameguswa alipofika Mosul na kuona jinsi ambavyo mji huu ulivyo vurugwa na kusambaratishwa kwa vita! Inasikitisha kuona nyumba za ibada na makazi ya watu yamegeuka kuwa magofu yasiyofaa tena kwa matumizi ya binadamu. Licha ya Makanisa haya kuharibiwa kwa kiasi kikubwa na mabomu, lakini bado yamekuwa ni kielelezo cha imani ya uwepo wa Mungu kati pamoja na watu wake.

Hapa ni mahali ambapo waamini wamekuwa wakikimbilia kusali, kutafakari na kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa mateso na mahangaiko yao, wakiwa na imani na matumaini ya faraja kutoka mbinguni! Kardinali Parolin anasema, vita aina mipaka wala macho, wananchi wote wa Iraq wameathirika ndiyo maana alipokuwa Mosul, Meya wa Jiji alifika kumsalimia na wote kwa pamoja wakatembea wakiwa wameshikana mikono, kielelezo cha umoja na mshikamano katika ujenzi wa Iraq mpya unaofumbatwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kutambua kwamba wote ni watoto wa Mungu. Huu ni wakati wa ujenzi wa msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Iraq.

Hija hii ya kichungaji ni kielelezo makini cha mshikamano wa umoja na udugu wa Kanisa la Kristo unaotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko. Familia ya Mungu nchini Iraq imeguswa kwa namna ya pekee, kwa uwepo wa Kardinali Parolin, kama mwakilishi wa Baba Mtakatifu katika maadhimisho ya Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2018. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, iko siku isiyokuwa na jina, ataweza kutembelea Iraq ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo ya watoto wa Mungu. Kardinali Parolin anaungana na familia ya Mungu nchini Iraq kuwasihi viongozi wa Serikali kuandaa mazingira yatakayomwezesha Baba Mtakatifu Francisko kutembelea na hatimaaye kusali na Wakristo huko Iraq. Baba Mtakatifu akifanikiwa kwenda huko, litakuwa ni tukio ambalo litawatia shime, ari na moyo mkuu katika maisha na utume wao, katika mchakato mzima wa kukabiliana na changamoto zilizoko mbele yao!

Kardinali Parolin anakaza kusema, kwa sasa Kanisa linajiandaa kwa ajili ya mkutano maalum dhidi ya nyanyaso za kijinsia, mwezi Februari, 2019. Mkutano huu utakaoongozwa na mambo makuu matatu: uwajibikaji, dhamana ya uwajibikaji; ukweli na uwazi. Ni mkutano ambao umeitishwa na Baba Mtakatifu Francisko na utwashirikisha viongozi wakuu kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, ili kuimarisha mbinu mkakati wa kupambana na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo; kuganga na kuponya athari hizi pamoja na kuwasikiliza waathirika ili haki iweze kutendeka. Lengo kuu ni kujenga mazingira salama kwa makuzi na malezi ya watoto wadogo sanjari na kuendelea kumwilisha sera na mbinu mkakati wa kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia kadiri ya mazingira ya Makanisa mahalia pamoja na kuhakikisha kwamba, tunu msingi za maisha ya Kiinjili zinatekelezwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa.

Kardinali Parolin anahitimisha mahojiano maalum na Vatican News, kwa kumtakia heri na baraka Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2019, mwaka ambao tayari unaonesha cheche za sera na mipango ya maisha na utume wa Kanisa kwa siku za usoni. Anamtakia afya njema, ari na moyo mkuu, ili aweze kuendelea kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Aendelee kuwa ni faraja kwa maskini na wale wote wanaoteseka na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Awashe moto wa matumaini kwa wale waliokata tamaa katika maisha. Watu wengi wanamwona Baba Mtakatifu Francisko kama alama ya: umoja, upendo na mshikamano wa kidugu. Kardinali Parolin anasema, licha ya changamoto za maisha na utume wake wa kila siku, haya ndiyo matashi mema, ambayo anapenda kumwombea Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka mpya wa 2019.

Kardinali Parolin: Iraq 2018
31 December 2018, 10:44