Cerca

Vatican News
Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya VIjana Duniani, Panama 2019 ni moto wa kuotea mbali! Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani Panama, 2019 ni moto wa kuotea mbali!  (AFP or licensors)

Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani, Panama 2019 moto wa kuotea mbali!

Januari mwaka 2019, Panama itakuwa ni gumzo la watu wa mataifa kutokana na maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, yatakayowashirikisha vijana kutoka kila sehemu ya dunia. Ni muda wa kutafakari vipaumbele vya maisha na utume wa vijana, changamoto, matatizo na fursa walizo nazo kama mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa viongozi wa Serikali ya Panama pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Panama na kwamba, atakuwepo nchini humo kuanzia tarehe 23-27 Januari 2019 ili kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 kama sehemu ya mchakato wa Mama Kanisa katika ujenzi wa sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwaongoza vijana kufikia ukomavu wa maisha na utume wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Januari mwaka 2019, Panama itakuwa ni gumzo la watu wa mataifa kutokana na maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, yatakayowashirikisha vijana kutoka kila sehemu ya dunia. Ni muda wa kutafakari vipaumbele vya maisha na utume wa vijana, changamoto, matatizo na fursa walizo nazo kama mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili. Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama, yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 22–27 Januari 2019, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe kama ulivyonena” Lk. 1:38.

Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta wa jimbo kuu la Panama anasema, hadi sasa vijana laki mbili tayari wamekwisha kujiandikisha kushiriki katika maadhimisho haya. Wengine 37, 000 wamekamilisha taratibu zote za usajiri na wengine 168, 000 wanaendelea kukamilisha. Hadi sasa kuna nchi 155 ambazo zimethibitisha kushiriki katika maadhimisho haya na kwamba, kuna vijana zaidi ya 37, 000 watashiriki kutoa huduma ya kujitolea wakati wa maadhimisho haya! Kwa hakika, hii itakuwa ni sherehe kubwa ya imani, matumaini na mapendo kwa vijana wa kizazi kipya.

Changamoto ya wakimbizi na wahamiaji ni kati ya tema zitakazojadiliwa kwa kina na mapana, ikizingatiwa kwamba, hii ni changamoto inayowagusa vijana wengi wanaotafuta fursa za ajira, hifadhi na usalama wa maisha yao kwa siku za usoni. Kwa sasa hii ni changamoto kubwa huko Amerika ya Kati, kwani kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Honduras, El Salvador na Guatemala wanaosafiri kwa makundi makubwa makubwa kuelekea nchini Marekani, ambako kwa sasa wanakumbana na “pazia la chuma”.

Amerika ya Kati ni Ukanda wa wafiadini na waungama imani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Oscar Armulfo Romero ambaye ni alikuwa mchungaji mwema na nabii, aliyejitahidi katika maisha na utume wake kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kuna watakatifu wengine kama Rosa wa Lima, Josè Sanchez wa Rio. Kanisa mahalia linataka kuhakikisha kwamba, hata vijana wasiokuwa na uwezo wa kiuchumi nao wanashiriki katika maadhimisho haya. Serikali kwa upande wake, inaendelea kushirikiana na Kanisa kwa karibu sana kuweza kukamilisha taratibu zote, tayari kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani huko Panama.

Baba Mtakatifu Francisko atapata nafasi ya kuteta na Maaskofu wa Amerika ya Kusini watakaohudhuria Siku ya Vijana Duniani huko Panama, ili kuwasikiliza. Familia ya Mungu Amerika ya Kati, inasubiri kwa hamu na matumaini makubwa ujio wa Baba Mtakatifu Francisko anayekwenda kuwafariji, kuwatia shime ili waweze kusonga mbele licha ya changamoto wanazokabiliana nazo! Kwa maombezi na tunza ya Bikira Maria, awasaidie kuona njia mpya ya kuweza kujenga jamii inayosimikwa katika upendo, umoja, udugu na mshikamano wa dhati.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa vijana wa kizazi kipya wanapoendelea kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama anawakumbusha kwamba, mapinduzi ya huduma ndiyo nguvu ya vijana wa kizazi kipya! Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano na maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa aliyediriki kusema, “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Huu ni ushuhuda wa ujasiri na ukarimu kwa mwamini aliyetambua siri ya wito wake, tayari kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani.

Vijana Panama 2019
12 December 2018, 16:05