Cerca

Vatican News
Papa Francisko akutana na kuzungumza na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Palestina. Papa Francisko akutana na kuzungumza na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Palestina.  (ANSA)

Papa Francisko akutana na kuzungumza na Rais Abbas wa Mamlaka ya Palestina.

Viongozi hawa wameridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Palestina na Vatican sanjari na mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Palestina mintarafu makubaliano yaliyofikiwa na pande hizi mbili kunako mwaka 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

 

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 3 Desemba 2018 amekutana na kuzungumza kwa faragha na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Palestina na baadaye amekutana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na Rais Abbas, viongozi hawa wameridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Palestina na Vatican sanjari na mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Palestina mintarafu makubaliano yaliyofikiwa na pande hizi mbili kunako mwaka 2015.

Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, wamegusia pia mchakato wa upatanisho ndani ya wananchi wa Palestina, kama sehemu muhimu ya kuweza hata kufikia upatanisho kati ya Palestina na Israeli katika ujumla wake, ili hatimaye, suluhu ya mataifa mawili, iweze kushika mkondo wake. Changamoto hii inapaswa kuendelezwa kwa kasi zaidi na Jumuiya ya Kimataifa, ili hatimaye, kuridhia matamanio halali ya watu wa Mungu kutoka katika mataifa haya mawili.

Kwa namna ya pekee, viongozi hawa wawili wamjikita zaidi katika katika umuhimu na dhamana ya Mji wa Yerusalemu, unaopaswa kutambuliwa, kulindwa na kudumisha utambulisho wake kama Mji Mtakatifu wa dini za Watoto wa Abrahamu! Mwishoni mwa mazungumzo yao, Baba Mtakatifu Francisko na Rais Mahmoud Abbas wameangalia kwa masikitiko makubwa vita na kinzani zinazoendelea kupekenyua maisha ya watu huko Mashariki ya Kati na kuita Jumuiya ya Kimataifa kujibidisha zaidi katika kutafuta amani ya kudumu na majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa kuzingatia mchango unaotolewa na Mashirika ya kitawa na kazi za kitume katika maeneo haya, ili kupambana na misimamo mikali ya kidini na kiimani inayohatarisha mahusiano na mafungamano ya kijamii huko Mashariki ya Kati!

 

03 December 2018, 14:12