Tafuta

Vatican News
Vatican: Maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu! Vatican: Maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu!  (ANSA)

Chakula bora; maji safi na salama ni haki msingi za binadamu!

Maji safi na salama ni muhimu sana katika mchakato mzima wa maboresho ya afya ya binadamu, ustawi na maendeleo yake. Maji yanaendelea kuwa ni sehemu muhimu ya agenda za Jumuiya ya Kimataifa hasa katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, tarehe 13 Desemba 2018 limeadhimisha warsha ya siku moja, ilioongozwa na kauli mbiu “Maji, Kilimo na Chakula: Tujenge ya Mbeleni”. Monsinyo Fernando Chica Arellano, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye: Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo wa Umoja wa Mataifa, IFAD pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP., katika hotuba yake ya kufunga rasmi warsha hii, amekazia umuhimu wa wadau mbali mbali kulinda na kutunza vyanzo vya maji; kwa kuwa na kilimo endelevu pamoja na watu kupata lishe bora kama sehemu ya mbinu mkakati wa Jumuiya ya Kimataifa wa kupambana na baa la njaa duniani, linalodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na inaendelea kuwa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa. Ikiwa kama suala zima la maji halitashughulikiwa kikamilifu, kwa siku za usoni, linaweza kuwa ni chanzo kikuu cha kinzani na migogoro ya kimataifa. Maji safi na salama ni muhimu sana katika mchakato mzima wa maboresho ya afya ya binadamu, ustawi na maendeleo yake. Maji yanaendelea kuwa ni sehemu muhimu ya agenda za Jumuiya ya Kimataifa hasa katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Lakini, maji yanapaswa kutambulika kwanza kabisa kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kamwe isigeuzwe kuwa biashara inayoweza kumilikiwa na kuendeshwa na makampuni binafsi. Sera na kilimo endelevu zisaidie hifadhi ya ardhi, kwani uharibifu wa mazingira ni chanzo kikuu cha maafa, umaskini na magonjwa. Kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, baadhi ya nchi duniani zimekumbwa na ukame wa kutisha, joto kali na mafuriko ambayo yanaendelea kutishia amani na usalama wa watu na mali zao. Kila watu wawe makini kutunza mazingira na vyanzo vya maji.

Monsinyo Fernando Chica Arellano anaendelea kufafanua kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuboresha mifumo ya maji safi na salama sanjari na kujikita katika sera za uhakika wa usalama wa chakula duniani, ikizingatiwa kwamba, idadi ya watu hadi kufikia mwaka 2050 itakuwa imeongezeka maradufu. Inakadiriwa kwamba, ifikapo mwaka 2050, ongezeko la mahitaji ya chakula litakuwa ni asilimia 60%. Ufugaji wa kisasa unatumia kiasi kikubwa cha maji, kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, vyanzo vya maji vinatunzwa na kuendelezwa.

Ukuaji wa miji ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga kama sehemu ya maboresho ya mchakato wa usambazaji na ugavi wa maji. Vatican inaendelea kukazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kudumisha umoja, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto ya maji, chakula na utunzaji bora wa ardhi kwa sasa na kwa siku za mbeleni! Ushirikiano huu unaweza kujengwa katika ubadilishanaji wa habari; rasilimali watu; ujuzi na maarifa; sera na mikakati, ili wote waweze kusonga mbele katika maendeleo fungamani na wala isiwepo nchi inayobaki nyuma kimaendeleo!

FAO: Madrid

 

14 December 2018, 10:57