Tafuta

Vatican News
Ujumbe wa Vatican: COP24: Mshikamano wa Kimataifa ni muhimu katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ujumbe wa Vatican: COP24: Mshikamano wa Kimataifa ni muhimu katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.  (foto-kraj)

Ujumbe wa Vatican COP24: Katowice: Mshikamano wa Kimataifa muhimu!

Ujumbe wa Vatican kwenye Mkutano 24 wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP24 Katowice, Poland. unakazia umuhimu wa utekelezaji wa Makubaliano ya Paris kama kielelezo cha mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano 24 wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP24 Katowice, Poland uliofunguliwa rasmi, Jumapili, tarehe 2 Desemba, 2018, unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 14 Desemba 2018. Wanachama wa Umoja wa Mataifa wanapaswa kuonesha mshikamano wa kimataifa kwa kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres anaendelea kutoa changamoto zaidi kwa viongozi wa serikali kufikia makubaliano ili hatimaye, kukamilisha mkataba huu ili kuokoa uchafuzi mkubwa wa mazingira duniani.

Monsinyo Bruno Marie Duffè Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na fungamani ya binadamu ndiye aliyeongoza ujumbe wa Vatican kwenye Mkutano 24 wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP24 Katowice, Poland. Vatican inakazia umuhimu wa utekelezaji wa Makubaliano ya Paris kama kielelezo cha mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote! Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ambao ulizinduliwa rasmi mwaka 2015 unakazia utunzaji bora wa mazingira kuwa ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo endelevu na fungamani kwa sababu, mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko.

Matumizi mabaya ya rasilimali ya dunia na uwajibikaji duni umepelekea uharibifu mkubwa wa mazingira, kiasi cha binadamu kujisikia kuwa ni mtawala wa mazingira na mwenye haki ya kutumia rasilimali hizi kadiri anavyopenda; matokeo yake ni uchafuzi mkubwa wa mazingira unaoendelea kuwatumbukiza wengi katika umaskini. Ujumbe wa Vatican umewataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwasikiliza wanasayansi na watafiti ili kudhibiti kikamilifu athari za mabadiliko ya tabia nchi ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuporomosha ubora wa maji safi na salama; usalama, uhakika na ubora wa chakula na lishe duniani na matokeo yake ni kuongezeka kwa vifo na majanga asilia kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira!

Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa changamoto kubwa ya maendeleo duniani. Athari zake ni pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; kuongezeka kwa joto; ukame; mafuriko; njaa, vita kati ya wakulima na wafugaji, pamoja na ongezeko kubwa la wadudu waharibifu wa mimea, na magonjwa ya mifugo na binadamu; kukauka kwa vyanzo vya maji; kuyeyuka kwa theluji n.k. Wakichangia mada katika mkutano huu Mercy Chirambo kutoka Caritas Malawi, CADECOM na Joseph Sapati Moeono Kolio wamekazia umoja na mshikamano wa kimataifa katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kwamba, haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo yake vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Mapambano dhidi ya umaskini ni hatua muhimu sana katika kulinda mazingira bora nyumba ya wote, hasa katika maeneo ambayo mara nyingi sana yameathirika na majanga asilia duniani.

Umoja na mshikamano wa kimataifa anasema Monsinyo Bruno Marie Duffè ni muhimu sana katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kama sehemu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kila mtu anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake katika kulinda na kutunza mazingira, lakini bila utashi wa kisiasa juhudi zote hizi zitagonga mwamba na binadamu wataendelea kupoteza maisha na mali zao kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Vatican:COP24

 

13 December 2018, 10:16