Tafuta

Vatican News
Masista wa Ivrea wametakiwa kuwa ni mashuhuda wa vyombo vya Injili ya huruma ya Mungu kwa maskini! Masista wa Ivrea wametakiwa kuwa ni mashuhuda wa vyombo vya Injili ya huruma ya Mungu kwa maskini!  (2018 Getty Images)

Masista wa Ivrea wametakiwa kuwa ni mashuhuda wa Injili ya upendo!

Masista wa Ivrea wamehaswa kuwa mashuhuda wa Injili ya huduma ya upendo wa Mungu kwa maskini, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na matumaini Barani Afrika na sehemu nyingine za dunia, kama ilivyokuwa hata kwa Askofu Pierre Claverie wa Oran pamoja na watawa wenzake 18 waliotangazwa kuwa Wenyeheri, huko Algeria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Desemba, Masista watano wa Shirika la Masista wa Upendo wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Ivrea, kutoka Tanzania na Kenya, wameweka nadhiri zao za daima katika Ibada ya misa takatifu iliyoongozwa na  Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha na Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Ndoa na Familia ya Yohane Paulo II, kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria, Trastevere, Jimbo kuu la Roma, nchini Italia.

Watawa wa Shirika la Upendo la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Ivrea maarufu kwa jina la “Masista wa Ivrea” wamehaswa kuwa mashuhuda wa Injili ya huduma ya upendo wa Mungu kwa maskini, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na matumaini Barani Afrika na sehemu nyingine za dunia, kama ilivyokuwa hata kwa Askofu Pierre Claverie wa Oran pamoja na watawa wenzake 18 waliotangazwa kuwa Wenyeheri, huko Algeria na Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu.

Masista wa Ivrea kama urithi wao kutoka kwa Mwenyeheri Antonia Maria Verna, muasisi wa Shirika; wameachiwa: Ibada kwa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Fumbo la Ekaristi Takatifu na Msalaba kama nyenzo msingi za maisha na huduma ya Injili kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Askofu Mkuu Vincenzo Paglia katika mahubiri yake; amekazia umuhimu wa utakatifu wa maisha na unyofu wa moyo kama chemchemi ya Injili ya huduma ya upendo na matumaini kwa watu wanaoteseka kutokana na umaskini, ujinga na magonjwa.

Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili ili aweze kuwa ni Tabernakulo ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu. Hata leo hii, waamini wanaitwa kuwa watu wasiokuwa na mawaa mbele ya Mwenyezi Mungu ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka; upendo unaoweza kukita mizizi yake katika sakafu ya nyoyo za watu. Upendo ni nguzo thabiti ya mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika umoja, udugu na mshikamano wa kweli! Upendo wa kidugu katika maisha ya kitawa unavunjilia mbali kuta za utengano unaofumbatwa katika mipaka ya nchi, lugha na rangi ya mtu.

Askofu Mkuu Paglia anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, Nadhiri ya: Ufukara, Utii na Usafi kamili ni kwa ajili ya huduma kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kwa namna ya pekee, ameelezea kuhusu uadui ambao Mwenyezi Mungu aliuweka kati ya nyoka na mwanamke, kiasi hata cha nyoka kulaaniwa kuliko wanyama wote na kuliko hayawani wote walioko mwituni. Lakini, Mwenyezi Mungu alimpatia mwanamke dhamana ya kukiponda kichwa cha nyoka, ili kuvunjilia mbali uwepo wa dhambi. Hii ndiyo chemchemi ya Mashauri ya Kiinjili. Watawa walioweka nadhiri zao za daima, wanaitwa na kutumwa kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa kutoa maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo kama walivyofanya wafiadini kutoka Algeria.

Bikira Maria alisadaka maisha yake kwa ajili ya Mpango wa Mungu, akawa ni Mama wa Mungu na Kanisa; akajitoa pia kwa ajili ya huduma kwa Mitume wa Yesu kwa njia ya sala. Kumbe, Ibada kwa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na Huduma ya Upendo ni sawa na chanda na pete, na kamwe haviwezi kutenganishwa, bali vinafungamana na kukamilishana. Huu ni mwaliko wa kumwilisha Injili ya huduma ya upendo kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kuwa mfuasi wa Kristo maana yake ni kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengine.

Masista walioweka nadhiri za daima, wawe ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma ya upendo, kwa kutambua kwamba, wamepambwa kwa tunu msingi za maisha zinazosimikwa katika utu, udugu, umoja, upendo na mshikamano wa dhati. Watambue kwamba, kuna furaha kubwa kutoa kuliko kupokea. Kumbe, Mashauri ya Kiinjili ni kwa ajili ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani inayofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu, kwa kuyafia malimwengu, tayari kuambata utakatifu wa maisha. Watawa waendelee kuwa karibu na Kristo Yesu kwa njia ya Neno, Sakramenti za Kanisa na huduma makini kwa maskini, daima wakijitahidi kujenga na kudumisha umoja katika maisha kijumuiya.

Masista walioweka nadhiri za daima mbele ya Sr. Raffaella Giudici, SCIC, Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Upendo wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Ivrea ni: Elizabeth Donati Kingo, Sr. Leticia Cyprian Mjungu; Sr. Masline Adhiambo Bumbria, Sr. Stella Ezekiel Bilinje pamoja na Sr. Angela Jeremiah Jorrow. Masista hawa wanataka kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwani wanayaweza mambo yote katika Yeye awatiaye nguvu! Shirika la Masista wa Upendo wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Ivrea, linaendelea kutoa huduma zao sehemu mbalimbali duniani hasa katika shule, hospitali na vituo mbalimbali vya matendo ya huruma kwa wahitaji. Barani Afrika wanafanya utume wao: Nchini Tanzania, Kenya na kwa bahati mbaya kutokana na vita na hali kuendelea tete kwa ajili ya usalama na maisha ya watawa, Shirika liliamua kusitisha huduma yake kwenye hospitali za Libya ambako wamekuwa huko kama mashuhuda wa Injili ya huduma na upendo kwa miaka zaidi ya hamsini! Masista wa Ivrea wanafanya pia utume wao huko: Uturuki, Lebanon, Israeli, Albania, Mexico na Pennsylvania, Marekani. Huko kote wanaitwa na kutumwa kutangaza Injili ya matumaini na mapendo, kwa kutambua kwamba, hekima, ukuu na utukufu wa Mwenyezi Mungu vinafumbatwa katika Fumbo la Msalaba!

Vatican News itawakosea haki, wale wote walijisadaka kwa ajili ya kuwaongoza Masista hawa katika Mafungo yao ya kiroho; walioandaa Ibada na Nyimbo za Liturujia, lakini zaidi, wale waliojisadaka ili kuhakikisha kwamba, familia ya Mungu kutoka Afrika Mashariki, inapata kile ambacho roho inapenda, yaani “Ugali wa sembe ambao ni nadra sana kupatikana katika mazingira ya Ulaya, “Chips dume” yaani mihogo ya kukaangwa iliyokuwa kivutio kwa wengi, kwani kufumba na kufumbua ikawa imetoweka yote, pamoja na Pilau, ingawa safari hii hakukuwepo na “take away”. Yaani, hata kama walikuwa ugenini, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ilifana sana kwa kuhitimishwa na “disco bubu”.

Masista wa Ivrea
10 December 2018, 09:36