Tafuta

Vatican News
Tarehe 21 Novemba: Siku kuu ya Bikira Maria Kutolewa Hekaluni & Siku ya Watawa Ndani Tarehe 21 Novemba: Siku kuu ya Bikira Maria Kutolewa Hekaluni & Siku ya Watawa Ndani  (Vatican Media)

Siku kuu ya B. Maria kutolewa Hekaluni & Siku ya Watawa wa ndani

Maadhimisho kwa Mwaka 2018 yanabeba uzito wa pekee, kwani hii ni siku maalum ya kutafakari makuu ya Mungu yanayofunuliwa kwa njia ya maisha ya watawa wa ndani, matunda ya neema kwa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, watawa ni nguzo ya sala kwa ajili pamoja na Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Novemba linaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kutolewa Hekaluni, sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Watawa wa Ndani. Waamini wanakumbushwa kwamba, Kanisa ni nyumba ya Sala na Ibada, mahali ambapo Mafumbo matakatifu yanaadhimishwa, ili kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kupata wokovu! Maadhimisho haya kwa Mwaka 2018 yanabeba uzito wa pekee, kwani hii ni siku maalum ya kutafakari makuu ya Mungu yanayofunuliwa kwa njia ya maisha ya watawa wa ndani, matunda ya neema kwa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, watawa ni nguzo ya sala kwa ajili pamoja na Kanisa. Watawa wa ndani wanaendelea kulitajirisha Kanisa la Kristo kwa matunda ya neema na huruma inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni siku ya kuendelea kutafakari kuhusu Katiba ya  Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko “Vultum Dei Quaerere” Yaani “Kuutafuta Uso wa Mungu” iliyotiwa mkwaju  kunako mwaka 2016 kwa ajili ya Wamonaki wa Mashirika ya Taamuli pamoja na Hati Elekezi ya Utekelezaji wake “Cor Orans” iliyotolewa na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ambalo tarehe 21 Novemba 2018 limeandaa kongamano kwa ajili ya watawa wa mashirika ya ndani.

Baba Mtakatifu ametoa ruhusa kwa wamonaki 300 kutoka mashirika ya utawa wa ndani kushiriki katika kongamano, fursa ya kusikiliza tafakari zitakazotolewa na viongozi wa Baraza, shuhuda kutoka kwa watawa wa ndani pamoja na kushirikishana uzuri wa maisha ya taamuli, changamoto na matumaini kwa siku za usoni. Hii ni siku ya sherehe na shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha ya taamuli yanayolitajirisha na kuupamba Uso wa Kanisa. Kongamano hili litahitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Kardinali Joao Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume.  

Baba Mtakatifu Francisko katika Katiba ya Kitume ya “Vultum Dei Quaerere” Yaani “Kuutafuta Uso wa Mungu” kwa ufupi anasema, kuna haja ya kudumisha majiundo makini; umuhimu wa tafakari ya Neno la Mungu; vigezo muhimu kwa Jumuiya ya Kimonaki ili kuweza kujitegemea pamoja na uwezekano wa kuunda Shirikisho la Wamonaki ndani ya Kanisa. Leo tungependa kukazia kwa namna ya pekee kuhusu tema mbali mbali zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kusaidia mchakato wa tafakari ya kina kuhusu maisha ya kitaamuli ndani ya Kanisa.

Tema ya kwanza ni majiundo makini: awali na endelevu bila kushikwa na kishawishi cha kutafuta idadi na mafanikio na kwamba, malezi yanahitaji muda na nafasi kubwa zaidi, yaani kati ya miaka tisa hadi kumi na miwili. Baba Mtakatifu anasema tema ya pili ambao ni muhimu sana ni Sala kwani hiki ni kiini cha maisha na utume wa Wamonaki na wala si hali ya mtawa kujiangalia mwenyewe. Mwaliko ni kupanua wigo ili kuweza kuwakumbatia watu wengi zaidi hasa wale wanaoteseka na kusumbuka katika maisha yao. Hawa ni wafungwa, wakimbizi, wahamiaji; watu wanaoteswa na kudhulumiwa; familia zenye madonda na makovu ya maisha; watu wasiokuwa na fursa za ajira; maskini, wagonjwa na waathirika wa dawa za kulevya. Wamonaki wanapaswa kusali na kuombea binadamu, ili kweli jumuiya za kitawa ziweze kuwa ni shule ya sala inayorutubishwa kwa ”Kashfa ya Msalaba”.

Tema ya tatu na ya nne ni Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu na Upatanisho. Baba Mtakatifu anapenda kutoa kipaumbele cha pekee kwa tafakari ya Neno la Mungu, chemchemi ya maisha ya kiroho na kiungo makini cha maisha ya kijumuiya, changamoto na mwaliko wa kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya wamonaki. Tafakari ipewe kipaumbele cha pekee kwa mtawa mmoja mmoja na jumuiya katika ujumla wake, ili kutambua na kumwilisha mapenzi ya Mungu katika maisha yao.

Wamonaki wawe makini kusoma alama za nyakati ili kung’amua mapema mambo yanayoweza kuwapeleka mbali na mapenzi ya Mungu. Tafakari ya Neno la Mungu haina budi kumwilishwa katika matendo, kwa kujisadaka kwa ajili ya wengine katika upendo. Baba Mtakatifu anawataka wamonaki kuadhimisha Fumbo la Ekaristi na Sakramenti ya Upatanisho kwa kuwa na mwendelezo wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Toba na wongofu wa ndani ni mahali muafaka pa kutafakari Uso wa huruma ya Mungu na msamaha ili kuwa kweli ni manabii na mitume wa huruma ya Mungu na vyombo  vya upatanisho, msamaha na amani; mambo ambayo ulimwengu unahitaji sana kwa nyakati hizi!

Tema ya tano na ya sita ni maisha ya kidugu na uhuru wa wamonaki kama njia ya kujisadaka kwa ajili ya Mungu, Kristo na Kanisa lake na huu ni mtindo wa Uinjilishaji. Baba Mtakatifu anawataka wamonaki kuendelea kukua na kukomaa katika maisha ya kijumuiya yanayofumbata umoja wa kidugu. Jumuiya inazaliwa, inakua na kukomaa kwa kujikita katika umoja na wote. Hiki ndicho kielelezo cha tasaufi ya umoja na kutegemeana; ushuhuda makini katika ulimwengu mamboleo unaosheheni kinzani, mipasuko na ukosefu wa usawa.

Inawezekana na inapendeza kuishi kwa umoja na katika upendo licha ya tofauti za kizazi, majiundo na tamaduni. Tofauti hizi anasema Baba Mtakatifu ni tunu muhimu sana zinazotajirisha maisha ya kijumuiya, kwani umoja katika mshikamano hauna maana ya kufanana. Hapa wamonaki wanahamasishwa kuwaheshimu na kuwathamini wazee pamoja na kuwapenda vijana; ili kuweza kuweka uwiano kati ya kumbu kumbu ya sasa na mambo yajayo kwa siku za usoni katika Jumuiya husika.

Baba Mtakatifu akigusia kuhusu uhuru wa wamonaki anasema hapa inawezekana kuwa na udumifu, umoja na taamuli ya jumuiya moja lakini kwa upande mwingine, hali hii isiwafanye kutowategemea wengine au kujitenga na wala wasikumbwe na ugonjwa wa kujiamini mno!

Shirikisho na wamonaki wa ndani ni tema ya saba inayojadiliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume ”Kuutafuta Uso wa Mungu”. Shirikisho hili linakuwa ni muundo mbinu wa umoja kati ya monasteri zinazoshirikiana karama moja. Lengo ni kukuza na kudumisha taamuli katika monasteri sanjari na kusaidia majiundo pamoja na mambo msingi ya Shirikisho lenyewe. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, pendekezo hili litafanyiwa kazi. Tema ya nane ni Wamonaki wa ndani, alama ya umoja wa dhati kati ya Kanisa na mchumba wake Kristo. Eneo hili linafumbata maisha ya taamuli na utume wa nje ambao ni kawaida tofauti na ule wa ndani. Lakini tofauti hizi zinapaswa kuangaliwa kama ni utajiri mkubwa kwa Shirika husika.

Tema ya tisa inayojadiliwa na Baba Mtakatifu katika Waraka wake huu wa kitume ni kazi. Hapa anapenda kuunganisha ”sala na kazi” yaani ”Ora et Labora”, kwa kuonesha uaminifu na majitoleo ya dhati bila kumezwa na tabia ya walimwengu wa nyakati hizi, bali waoneshe ari na moyo wa taamuli, Hapa kazi inapaswa kutambuliwa kuwa ni mchango katika kazi ya uumbaji, huduma makini kwa binadamu na mshikamano na maskini, kwa kuwa na uwiano mzuri wa ushirikiano katika masuala haya yanayotekelezwa kila siku ya maisha.

Tema ya kumi inajikita katika Ukimya kuwa ni usikivu unaopata mwanga kutoka katika Neno la Mungu. Ni kielelezo cha utupu wa ndani ili kuunda mazingira ya kupokea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huu ni ukimya unaomsikiliza Mungu na kilio cha binadamu! Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa aliyefaulu kulipokea Neno kwa sababu alikuwa ni mwanamke mkimiya na ukimiya wake ulisheheni utajiri wa upendo.

Tema ya kumi na moja ni njia za mawasiliano ya jamii! Baba Mtakatifu anatambua na kuthamini maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano duniani na mchango wake katika uundaji wa mawazo na mahusiano ya watu duniani. Vyombo vya mawasiliano ni muhimu katika majiundo na mawasiliano ya kijamii, lakini hapa wamonaki wanapaswa kuwa na kiasi katika matumizi ya vyombo hivi vya mawasiliano ya kijamii, ili visiwe ni sababu ya kukwepa wajibu wa maisha ya kijumuiya, kukosa mwelekeo; kuathiri wito au kuwa ni kikwazo katika maisha ya taamuli.

Nikira Maria: Watawa

 

20 November 2018, 14:04