Tafuta

Vatican News
Utume wa kwaya: Wao ni vyombo vya upendo wa Mungu, kielelezo cha imani na huduma kwa watu wa Mungu! Utume wa kwaya: Wao ni vyombo vya upendo wa Mungu, kielelezo cha imani na huduma kwa watu wa Mungu!  (Vatican Media)

Utume wa waimbaji ndani ya Kanisa: Ni kupeleka upendo wa Kristo kwa walimwengu!

Nyimbo na muziki mtakatifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa zinawasaidia waamini kuzamisha Neno la Mungu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Kimsingi anasema Baba Mtakatifu Francisko, muziki ni chombo cha imani, amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu wote, Jumapili tarehe 25 Novemba 2018, amewakumbuka wanakwaya zaidi elfu nane kutoka katika nchi arobaini waliokuwa wanashiriki katika Kongamano la III la Kwaya Kimataifa, lililokuwa linaadhimishwa mjini Vatican kwa kutambua kwamba, muziki mtakatifu ni chombo cha ibada na uinjilishaji; ni amana na utajiri wa Kanisa; dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa ibada, unyenyekevu na unyofu wa moyo!

Hii inatokana na ukweli kwamba, nyimbo na muziki mtakatifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa zinawasaidia waamini kuzamisha Neno la Mungu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Kimsingi anasema Baba Mtakatifu Francisko, muziki ni chombo cha imani, amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa! Wanakwaya hawa, Jumapili, wameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu iliyongozwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya mchakato wa uhamasishaji wa uinjilishaji mpya!

Katika mahubiri yake, amewakumbusha wanakwaya kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa Mungu; ni watunzaji wa uzuri wa muziki mtakatifu; wao pia ni vyombo vya huduma ya uinjilishaji, wanaopaswa kusaidia mchakato wa kupyaisha maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kutukuzwa na kuabudiwa na mwanadamu aweze kupata wokovu. Kuhusu Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu wote, Askofu mkuu Fisichella amekaza kusema, ufalme wa Kristo umetundikwa kwenye Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu.

Yesu ni ufunuo wa ukweli, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, uliojionesha kwa njia ya maisha, maneno na matendo yaliyotekelezwa na Kristo mwenyewe. Anasema, upendo wa Mungu ni chachu inayoweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya walimwengu mamboleo. Amewataka wanakwaya hawa, kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa ukweli unaopaswa kutangazwa hadi miisho ya dunia kwa njia ya muziki mtakatifu. Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa anasema, “Cantare amantis est” yaani “kuimba ni kwa ajili ya mtu anayependa”. Upendo wao kwa Mwenyezi Mungu unafumbatwa katika muziki mtakatifu kama kielelezo cha imani na huduma kwa watu wa Mungu.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, amehitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, utume wa uimbaji ni huduma makini kwa ajili ya Kanisa. Muziki mtakatifu unasaidia sana maboresho na ushiriki wa waamini katika liturujia na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, changamoto kwa wanakwaya ni kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha waamini wengine furaha ya Injili kwa njia ya muziki mtakatifu. Ikumbukwe kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayowakirimia waamini matumaini ya kuimba huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, hadi pale atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho.

Muziki mtakatifu kiwe ni kielelezo cha furaha ya Injili, toba na wongofu wa ndani; imani na matumaini ya watu wa Mungu kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Wanakwaya wajitahidi kuimba na kulihudumia Kanisa, daima wakiwa tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Wanakwaya watambue kwamba wao ni mashuhuda na vyombo vya uzuri wa muziki mtakatifu na kwamba, maisha yao yote yanapaswa kuwa ni wimbo wa sifa na shukrani kwa Kristo Mfufuka!

Utume wa Kwaya

 

26 November 2018, 08:03