Tafuta

Vatican News
Kanisa litaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu! Kanisa litaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu!  (AFP or licensors)

Kardinali Parolin: Kanisa litaendelea kutetea haki msingi za binadamu!

Haki msingi za binadamu zinafumbatwa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo, msingi wa amani na maridhiano kati ya watu; hizi ni haki zinazoheshimu sheria maumbile na sheria ya Mungu na kwamba, haki hizi zinakwenda sanjari na wajibu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa Joseph Ratzinger/Benedikto XVI, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha LUMSA kilichoko mjini Roma, kuanzia tarehe 15-16 Novemba 2018 wanafanya kongamano la VIII la kimataifa linalojadili kuhusu: uhuru wa kidini, haki asilia, mabadiliko katika uhuru na utamaduni wa haki msingi za binadamu pamoja na upotoshwaji wa dhana hizi katika Jumuiya ya Kimataifa! Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi, tarehe 15 Novemba 2018, katika hotuba yake elekezi amebainisha mchango wa Mama Kanisa katika kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu kwa njia ya majadiliano na diplomasia ya kimataifa.

Haki msingi za binadamu zinafumbatwa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo, msingi wa amani na maridhiano kati ya watu; hizi ni haki zinazoheshimu sheria maumbile na sheria ya Mungu na kwamba, haki hizi zinakwenda sanjari na wajibu. Baada ya Vita Kuu ya Dunia, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wakaanza kubainisha haki msingi za binadamu mintarafu Fumbo la Mungu; wakawafunulia walimwengu maana ya maisha, yaani ukweli wa ndani wa binadamu; umuhimu wa maisha ya kiroho; utu na heshima ya binadamu pamoja na uhuru wa watoto wa Mungu. Kumbe, Kanisa kwa nguvu ya Injili linatangaza haki msingi za binadamu zinazofumbata sheria ya Mungu dhidi ya uhuru usiokuwa na mipaka.

Kardinali Parolin amegusia kuhusu ukoloni wa kiitikadi.  Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu haki msingi za binadamu dhidi ya kile kinachodaiwa kuwa ni “Haki Mpya” ambazo kimsingi zinasigana na tamaduni, mila na desturi za mataifa mengi. Haki msingi za binadamu zinatambua na kuheshimu: utu na heshima ya binadamu; uhuru wa kweli; haki na amani dhidi ya utandawazi wa ubinafsi. Sheria ya Mungu ambayo imepiga chapa katika dhamiri ya mwanadamu inapaswa kuheshimiwa na wote. Kanisa limeendelea kutetea haki msingi za binadamu kwa njia ya kidiplomasia kwa kutambua kwamba, kwa njia ya mashirika ya kitawa na kazi za kitume, Kanisa limeendelea kusimama kidete kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Kanisa linakazia umuhimu wa kujikita katika kanuni maadili na utu wema hasa katika masuala ya “Uhandishi jani” ambao kwa sasa unaendelea kupenya zaidi katika mchakato wa kurutubisha vinasaba kwenye mazao kwa njia ya kibayolojia; upandikizaji wa viungo vya binadamu pamoja uzalishaji wa binadamu kwa njia ya chupa. Maendeleo haya ya sayansi na teknolojia yanahatarisha uhai wa binadamu na kutaka kumng’oa Mwenyezi Mungu kutoka katika maisha ya mwanadamu. Kanisa Katoliki limefuta adhabu ya kifo katika Mafundisho na Mapokeo yake kwa kukazia njia zinazotetea na kulinda: maisha ya watu, amani na usalama wao dhidi ya adui; kwani hizi ni njia zinazodumisha utu, ustawi na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kufanya marekebisho kwenye Katekisimu ya Kanisa Katoliki, kifungu namba 2267 kinachozungumzia kuhusu adhabu ya kifo na tafsiri mpya inapaswa kuingizwa katika vipengele mbali mbali vya Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Kanisa Katoliki limefuta adhabu ya kifo katika Mafundisho na Mapokeo yake kwa kukazia njia zinazotetea na kulinda maisha ya watu, amani na usalama wao dhidi ya adui; kwani hizi ni njia zinazodumisha utu, ustawi na mafao ya wengi.

“Kwa kweli leo, kutokana na uwezekano ambao serikali inao siku hizi wa huweza kufaulu kuzuia uhalifu kwa aliyetenda kosa asiweze kuleta madhara bila kumwondolea kabisa uwezo wa kujikomboa mwenyewe, kesi ambazo kumuua mkosaji ni lazima kabisa kabisa ni cheche sana na “kwa kweli karibu haziko kabisa”. Kanisa linafundisha kwa mwanga wa Injili kwamba “Adhabu ya kifo haikubaliki kwa sababu inadhuru haki na utu wa mtu”. Kanisa linaendelea kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, adhabu ya kifo inaondolewa duniani kote!

Kanisa kwa njia ya diplomasia ya kimataifa, linaendelea kupigania haki msingi za wakimbizi na wahamiaji duniani kwa kuragibisha kampeni ya “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji”. Huu ni Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaolenga kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima yao! Unakazia umuhimu wa jamii kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kukusanya maoni; kwa kupunguza gharama za kuwahudumia wahamiaji sanjari na kudumisha usalama na maisha bora zaidi. Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa wahamiaji unapania pamoja na mambo mengine kuboresha: ulinzi na usalama; haki msingi za binadamu pamoja na kupatiwa huduma ya msaada wa kisheria pale haki zao zinapovunjwa.

Mkataba huu unawatupia jicho wakimbizi na wahamiaji hatari kwa maisha na usalama wa raia wengine. Watu hatari wanaweza kurejeshwa makwao;  uwezekano wa kudhibiti uhuru wa wakimbizi. Kimsingi “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji” unapania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa kwa baadhi ya serikali pamoja na kuangalia umuhimu wa kutumia nguvu ya wakimbizi katika kuzalisha na kutoa huduma, mwishoni ni suala la udhibiti wa mipaka!  

Baba Mtakatifu Francisko anakazia kwa namna ya pekee: umuhimu wa “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowakirimia. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika tamko lao kuhusu “Dignitatis humanae” yaani “Uhuru wa kidini” wanasema, utu na heshima ya binadamu; maana na misingi wa uhuru wa kidini; dhamiri nyofu, umuhimu wa mahusiano kati ya binadamu na Mwenyezi Mungu; uhuru wa kidini unaofumbatwa katika maisha ya kijumuiya, kifamilia na kwamba, haya ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa ili kulinda na kukuza uhuru wa kuabudu!

Kardinali Pietro Parolin anahitimisha hotuba yake elekezi kwa kusema, haki msingi za binadamu zinaweza kufupishwa katika Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani kama inavyofafanuliwa na Kristo Yesu kwa njia ya Mfano wa Msamaria Mwema, kwani haki msingi za binadamu ni sehemu ya vinasaba vilivyopigwa chapa katika Injili ya Kristo, kwa kukazia: utu na heshima ya binadamu; nafasi ya Mungu katika maisha pamoja na dhamiri nyofu. Haya ni mambo msingi katika kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu! Hii ni changamoto changamani na endelevu katika maisha na utume wa Kanisa.

Haki Msingi za Binadamu
16 November 2018, 15:46