Cerca

Vatican News
Mwaka wa Watakatifu wakuu wa Huruma ya Mungu, Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma! Mwaka wa watakatifu wakuu wa Huruma ya Mungu, Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma! 

Mwaka wa Watakatifu wakuu wa Huruma ya Mungu Kiabakari, Musoma!

Waamini wa Parokia ya Kiabakari wameelezea kuhusu mafanikio ya Maadhimisho ya Mwaka wa Mitume wakuu wa Huruma ya Mungu, yaani Mtakatifu Yohane Paulo II na Sr. Faustina. Huu umekuwa ni wakati muafaka wa kuendelea kujikita zaidi katika kuimarisha matunda yaliyopatikana wakati wa Mwaka wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Marek Solczyn’ski, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, wakati wa ziara yake ya kichungaji Jimbo Katoliki Musoma, hivi karibuni, amekazia umuhimu wa waamini kukimbilia kwenye “Bahari ya huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu zinazopaswa kuadhimishwa kwa moyo wa Ibada, Uchaji na Imani thabiti. Amri za Mungu na Mashauri ya Kiinjili yawe ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Kituo cha Hija Kitaifa cha Huruma ya Mungu, Kiabakari kiwe ni shule ya sala, toba na wongofu wa ndani kwa waamini ndani na nje ya Tanzania.

Waamini wa Parokia ya Kiabakari katika risala yao kwa Askofu mkuu Marek Solczyn’ski wameelezea kuhusu mafanikio ya Maadhimisho ya Mwaka wa Mitume wakuu wa Huruma ya Mungu, yaani Mtakatifu Yohane Paulo II na Sr. Faustina. Huu umekuwa ni wakati muafaka wa kuendelea kujikita zaidi katika kuimarisha matunda yaliyopatikana wakati wa Mwaka wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, kielelezo makini cha imani tendaji! Imekuwa ni fursa ya kujikita katika katekezi na malezi endelevu kwa wakatekumeni, wanafunzi wa dini pamoja na waamini katika ujumla wao, mkazo zaidi ukiwa ni utume wa Jumuiya ndogondogo za Kikristo. Parokia imezindua Chama cha Wito kama sehemu ya utekelezaji wa changamoto ya maisha na utume kwa vijana, ili kuweza kuimarisha imani na kuwasindikiza vijana katika mang’amuzi ya miito yao, tayari kufanya maamuzi magumu katika maisha.

Waamini wamefanya ukarabati mkubwa wa Hekalu na Huruma ya Mungu, unaotarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2019. Parokia inaendelea kuimarisha mawasiliano sanjari na utekelezaji wa sera ya kujitegemea na kulitegemeza Kanisa mahalia kwa njia ya sadaka, zaka, michango na majitoleo ya hali na mali. Parokia inatambua mchango mkubwa unaofanywa na makatekista vigangoni, kumbe, waamini wameamua kuwawezesha kikamilifu. Parokia imejipanga walau kila mwaka kutenga kiasi cha shilingi milioni tano kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo sanjari ya ujenzi wa Makanisa vigangoni, ili kuwawezesha waaamini kupata mahali stahiki pa Ibada na Sala. Ujenzi huu unaelekezwa katika vigango vya Isaba, Busirime, Kamugegi, Ryamugabo pamoja na Mwanza-Buriga

Parokia imejizatiti kuanzisha miradi inayopania kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi, ili waweze kupata pia nguvu za kimaadili na kiutu. Parokia inajielekeza zaidi katika shughuli za kilimo na ufugaji wa kisasa sanjari na mchakato wa uboreshaji wa huduma kwa mahujaji wanaopenda kujipatia muda wa faragha na upweke ili kusali, kutafakari, toba na wongofu wa ndani.

Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania katika kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, Miaka 100 ya Upadre Tanzania na miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Jimbo Katoliki la Musoma ameandika Barua ya Kichungaji inayoongozwa na kauli mbiu “Upendo kwa Utume” na humo anapembua historia ya Jimbo Katoliki la Musoma. Parokia ya Kiabakari tarehe 20 Agosti 2017 imeadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, matunda na juhudi za ukuaji wa Kanisa Mahalia Jimbo Katoliki la Musoma, furaha ya uinjilishaji Tanzania.

Katika mahojiano maalum na Vatican News, Padre Wojciech Adam Koscielniak, Paroko wa Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, muasisi wa Parokia na Kituo cha Hija cha Kiabakari Jimbo Katoliki Musoma, chemchemi ya huruma ya Mungu ndani na nje ya Tanzania anasimulia historia ya Parokia ya Kiabakari iliyopewa msukumo wa pekee na Hayati Askofu Justin Samba wa Jimbo Katoliki la Musoma kwa wakati ule, aliyebariki jiwe la msingi la ujenzi wa Makao makuu ya Parokia kunako tarehe 26 Januari 1991 na kuzinduliwa rasmi na Askofu mkuu Agostino Marchetto, Balozi wa Vatican nchini Tanzania kwa wakati huo.

Padre Wojciech Adam Koscielniak anasema, maadhimisho haya yamesaidia sana     kuimarisha: imani, matumaini na mapendo ya familia ya Mungu Parokia ya Kiabakari kwa kumtolea sifa na shukrani Roho Mtakatifu aliyewezesha kumwilisha ndoto ya kuwa na Kituo cha Huruma ya Mungu Jimbo Katoliki Musoma katika kipindi cha miaka 25 na matunda yake yanaonekana sasa kwani Baraza la Maaskofu Katoliki wamekipandisha hadhi na kuwa sasa ni Kituo cha Hija Kitaifa. Kipindi chote hiki umekuwa ni muda muafaka kwa kuhamasisha Sakramenti ya Ndoa, Parokia ya Kiabakari na Mwaka wa Uimarishaji wa Familia Katoliki, Parokia ya Kiabakari. Kwa hakika, Parokia ya Kiabakari, kumenoga, nendeni mkajionee wenyewe!

Watakatifu wa Huruma
01 November 2018, 17:40