Tafuta

Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana 2018: Dhamana, wajibu na haki za wanawake katika maisha na utume wa Kanisa! Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana 2018: Dhamana, wajibu na haki za wanawake katika maisha na utume wa Kanisa! 

Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana: nafasi ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa!

Dhamana na utume wa wanawake ndani ya Kanisa unajidhihirisha wazi kwa njia ya Bikira Maria; Kumbe, Kanisa linapaswa kushikamana pamoja na “wanawake wa shoka” ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, wanarithisha: imani na tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii kwa watoto wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Jumapili ya XXX ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, yaani, Jumapili tarehe 28 Oktoba 2018 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga rasmi maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018. Taarifa kutoka kwa Monsinyo Guido Marini, Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa inaonesha kwamba, Ibada ya Misa Takatifu itaanza saa 4:00 asubuhi kwa saa za Ulaya.  

Mababa wa Sinodi katika taarifa zao kutoka kwenye Makundi mbali mbali wanasema, wanataka kuliona Kanisa likitekeleza sera na mikakati itakayowawezesha vijana kuwa chachu ya wema, uzuri na utakatifu wa maisha; mambo msingi yanayolipyaisha Kanisa la Kristo kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Upendo na ukarimu; mfumo dume na ubaguzi wa kijinsia pamoja na mchango wa wanawake ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kupembuliwa kwenye Sinodi. Mababa wa Sinodi wanasema, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, kauli mbiu ya maadhimisho ya Sinodi hii, “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” inamwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Mambo msingi ya kuzingatia ni: utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini; kuwasindikiza vijana, ili hatimaye, waweze kufanya maamuzi magumu katika maisha na wito wao. Ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni changamoto ambayo Mababa wa Sinodi wanataka kuona inamwilishwa katika vipaumbele vya Kanisa, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wa Mungu; Chombo cha huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini walei wawe mstari wa mbele katika kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya chachu ya Injili ya Kristo na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Ikumbukwe kwamba, watu leo hii, wanasikiliza na kuvutwa zaidi na watu wanaoshuhudia kile wanachohubiri, kumbe, vijana wajengewe uwezo wa kuwa ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake. Kanisa liwasaidie vijana kukutana na Kristo kwa njia ya Neno, Sakramenti na huduma kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, kielelezo makini cha imani katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kanisa liwe mstari wa mbele kupigania haki msingi za binadamu, utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi. Si haba, kusikia kwamba, Mama wakuu wa Mashirika ya Kitawa nao pia wameomba kushiriki katika kupiga kura ili kupitisha maamuzi yanayotolewa na Sinodi, badala ya kuwa wasikilizaji tu.

Uwepo umoja na mshikamano kati ya watawa na wakleri na kwamba, wanawake wanasubiri kusikia matokeo ya Tume lengo ni kuwawezesha wanawake kufahamiaka, kuheshimiwa, kuthaminiwa pamoja na kushirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake; ili wanawake waweze kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Bila mchango wa wanawake, Kanisa litapoteza nguvu yake ya kujipyaisha tena. Dhamana na utume wa wanawake ndani ya Kanisa unajidhihirisha wazi kwa njia ya Bikira Maria; Kumbe, Kanisa linapaswa kushikamana pamoja na “wanawake wa shoka” ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, wanarithisha: imani na tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii kwa watoto wao.

Wanaume na wanawake, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wapendane na kukamilishana; bila kuwadharau, kuwabeza na kuwanyanyasa wanawake. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa ni changamoto kubwa inayohitaji kupembuliwa kwa kina na mapana, kwa kujikita katika hija ya ukweli na uwazi; toba na wongofu wa kimisionari pamoja na kuweka sera na mikakati itakayoliwezesha Kanisa kuunda mazingira bora zaidi ya malezi na makuzi ya watoto! Wanawake washirikishwe pia katika malezi na majiundo ya Majandokasisi. Sauti ya wanawake, inapaswa kusikilizwa ndani ya Kanisa. Wanawake wanaoshiriki Sinodi wengi wao ni “vigogo” kutoka vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu; waandishi wa vitabu na wadau katika utume wa vijana.  Idadi ya wanawake inapaswa kuongezwa katika Sinodi, kwani wanawake ni rasilimali muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Wanawake washirikishwe katika mchakato wa kufanya maamuzi katika maisha na utume wa Kanisa. Bikira Maria awe ni mfano bora katika shule ya ufuasi wa Kristo Yesu. Vijana wawe ni nyota ya Msamaria mwema kwa njia ya huduma; nyota ya umisionari, matumaini na majadiliano ya kidini na kiekumene. Kimsingi, Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, dhamana na utume wa wanawake katika Kanisa hauna budi kuimarishwa, kwa kukazia zaidi makuzi, malezi na majiundo endelevu, ili kuondokana na mfumo dume unaowanyima wanawake haki zao msingi. Majadiliano ya kidini na kiekumene ni mambo muhimu katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu.

Sinodi Vijana: Wanawake
24 October 2018, 12:11