Tafuta

Vatican News
Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana wameanza kusikiliza taarifa ya makundi Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana wameanza kusikiliza taarifa ya makundi  (Vatican Media)

Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana: Mang'amuzi ya miito na kuwasindikiza vijana!

Mababa wa Sinodi wanasema, maana ya wito itakayotolewa na Sinodi ijikite zaidi katika taalimungu, elimu ya Kanisa, uelewa wa binadamu pamoja na kusoma alama za nyakati na kwamba, wito ni mchakato wa kumtafuta, ili hatimaye, kumwambata Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana wanaendelea kuchambua: Sehemu ya pili ya “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya Kutendea” ambayo inajikita zaidi kuhusu: Kanisa: Imani na miito; mang’amuzi pamoja na kuwasindikiza vijana. Wameanza kutoa taarifa kutoka katika makundi makubwa 14, mawazo ambayo yatachangia kuandaa hati ya mwisho kutoka kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018. Vijana watambue kwamba, ujana ni tunu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, kamwe wasiuchezee kwani fainali iko uzeeni! Lakini, ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni muhimu sana katika malezi na makuzi ya ujana wenye tija! Vijana wasaidiwe kung’amua umuhimu wa rasilimali muda katika maisha yao, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu.

Maaskofu wanasema, Kanisa halina budi kuwa ni chombo cha mwaliko wa imani kwa vijana, ili waweze kuthubutu kumwendea Kristo Yesu ili kujionea wenyewe kama ilivyokuwa kwa Mitume wa kwanza, kiasi cha kuwashuhudia ndugu zao kwamba, wamekutana na Masiha, Kristo Yesu. Wanakumbusha kwamba, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Wito wa kwanza unapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambao ni maisha; Pili ni wito katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo, mintarafu kazi na karama za Roho Mtakatifu.

Mababa wa Sinodi wanaendelea kufafanua kwamba, kuna wito wa kiutu unaofumbatwa katika maisha; wito wa kikristo unaowaelekeza waamini kumfuasa Kristo kwa karibu zaidi kwa njia ya huduma na kwamba, kuna wito maalum pamoja na wito wa kitaaluma; miito yote hii ni muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa, unaoweza kusaidia mchakato wa utakatifu wa maisha, wito kwa watu wote.

Madhaifu na mapungufu ya kibinadamu yasiwe ni sababu ya kushindwa kuona huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa yanayowaonesha vijana kwamba, Kristo Yesu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkirimia binadamu furaha ya Injili!

Mababa wa Sinodi wanasema, maana ya wito itakayotolewa na Sinodi ijikite zaidi katika taalimungu, elimu ya Kanisa, uelewa wa binadamu pamoja na kusoma alama za nyakati na kwamba, wito ni mchakato wa kumtafuta, ili hatimaye, kumwambata Kristo Yesu. Kijana anayejisikia kuwa na wito hana budi kuhakikisha kwamba, maisha yake yanalandana na maisha ya Kristo, mapenzi ya Mungu pamoja na kukidhi masharti muhimu ya ufuasi wa Kristo Yesu na Kanisa lake, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Vijana wanapaswa kuwa wasikivu kwa Roho Mtakatifu, tayari kukumbatia toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, aliyekubali kupokea mpango wa Mungu katika maisha yake!

Mang’amuzi ya miito: Mababa wa Sinodi wanasema, tamaa ya kuwa na Mwenyezi Mungu imeandikwa katika moyo wa mtu kwa sababu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwa ajili ya Mungu. Mungu haachi kumvuta mtu kwake, na ni katika Mungu tu ndipo ambapo mtu anaweza kupata ukweli na heri ambayo hachoki kuitafuta. Lakini, si rahisi sana kwa vijana kung’amua mapenzi ya Mungu katika maisha yao, jambo linalowataka vijana kurejea tena katika chemchemi ya furaha ya kweli kwa kukutana na Kristo Yesu. Mang’amuzi ya miito ni chachu ya kukoleza fadhila mbali mbali za Kikristo. Mang’amuzi ya miito yawawezeshe vijana kuwa na furaha ya kweli katika maisha, kwa kumwambata Mungu, aliye asili ya wema na uzuri wote. Chemchemi ya baraka na neema.

Kuwasindikiza vijana: familia pamoja na wadau mbali mbali wanahimizwa kutekeleza dhamana na wajibu wao ili kuwasindikiza vijana kuweza kufanya maamuzi magumu katika maisha. Lakini, wazazi, walezi na viongozi wa maisha ya kiroho wanahitaji “kupigwa msasa” katika malezi, kwa kuwa na nyenzo na vigezo muhimu vinavyowaongoza vijana katika maisha yao. Kanisa ni Mama na Mwalimu na kwamba, Wakleri wanayo nafasi kubwa sana katika mchakato wa kuwasindikiza vijana katika safari ya miito yao. Wadau mbali mbali washikamane katika kuwalea na kuwasindikiza vijana, ili waweze kupata mang’amuzi mapana ya maisha na miito yao. Watu wa ndoa, wawe ni mifano bora kwa maisha ya ndoa na familia; wakleri na watawa, wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu na kwamba, familia yote ya Mungu inawajibikiana katika malezi pasi na ubaguzi wala kutegeana!

Sinodi vijana: miito
17 October 2018, 09:53