Cerca

Vatican News
Sehemu ya kwanza ya hati ya kutendea kazi: Kung'amua: Kanisa kusikiliza ukweli! Sehemu ya kwanza ya hati ya kutendea kazi: Kung'amua: Kanisa kusikiliza ukweli! 

Sinodi ya vijana: taarifa ya makundi: kusikiliza ili kujitambua!

Mababa wa Sinodi katika kikao chao cha tano wamehitimisha sehemu ya kwanza ya hati ya kutendea kazi: Kung’amua: Kanisa kusikiliza ukweli ili kuweza kujifahamu kikamilifu. Mababa wa Sinodi wanasema, kuna haja ya kuwasikiliza kwa makini vijana ili waweze kujitambua, kuendelea kushirikiana nao kwa karibu kwa kutambua lugha wanayoitumia, ili kuwajengea matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana wanaendelea na sala, tafakari sanjari na kushirikishana katika makundi maalum kadiri ya lugha wanazotumia. Mababa wa Sinodi katika kikao chao cha tano wamehitimisha sehemu ya kwanza ya hati ya kutendea kazi: Kung’amua: Kanisa kusikiliza ukweli ili kuweza kujifahamu kikamilifu. Mababa wa Sinodi wanasema, kuna haja ya kuwasikiliza kwa makini vijana ili waweze kujitambua; kushirikiana nao kwa karibu kwa kutambua lugha wanazotumia, ili kuweza kuwafikishia Habari Njema ya matumaini. Viongozi wa Kanisa wajenge sanaa na utamaduni wa majadiliano na vijana katika ukweli na uwazi, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko!

Mababa wa Sinodi wanakazia umuhimu wa vijana katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, viongozi wa Kanisa hawana budi kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima. Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ili kuwa karibu na binadamu mdhambi na hatimaye, akampatia nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu. Kanisa halina budi kujikita katika toba, wongofu wa ndani, unyenyekevu, ari na moyo mkuu; mambo msingi yanayopaswa kumwilishwa katika ushuhuda unaoakisi Fumbo la Utakatifu wa maisha na Sakramenti ya maisha hai. Vijana wasikilizwe kwa moyo wa huruma na mapendo.

Kanisa linawapokee na kuwasaidia kadiri ya matamanio yao halali, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga katika hatua mbali mbali za maisha, malezi na makuzi ya vijana: kwenye familia, shule na taasisi za elimu bila kusahau umuhimu wa maisha na utume wa vijana kwenye Parokia. Kuna kundi kubwa la vijana ambalo limejeruhiwa na kwamba, linahitaji kusikia Injili ya matumaini inayomwilishwa katika Katekesi makini na endelevu; katika huduma kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; malezi ya awali na endelevu kwa kuzingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Vijana wafundishwe kuthamini na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wasindikizwe kwa imani, matumaini na mapendo, ili waweze kung’amua wito katika maisha yao na hatimaye, kufanya maamuzi magumu na endelevu!

Vijana ni amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Changamoto za maisha ya kifamilia, kiuchumi, kijamii na kitamaduni; mambo yanayoibuka kwa kasi katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia yanayopaswa kushughulikiwa kikamilifu kwa kuwajengea vijana uwezo wa kupambana na hali zao, bila kutafuta njia za mkato katika maisha! Madhara ya vita, njaa, magonjwa, rushwa na ufisadi ni kati ya mambo yanayochangia hali ngumu ya maisha ya vijana, kiasi cha kuwakatisha tamaa. Kuna haja ya kuimarisha utandawazi wa mshikamano utakaotoa fursa ya ajira, elimu, ustawi na maendeleo endelevu ya vijana kwa kuondokana na utamaduni usiojali wala kuthamini utu, maisha na haki msingi za binadamu. Vijana wajikite katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, mambo yanayohatarisha umoja, upendo, mshikamano na mafungamano ya kijamii.

Taasisi za elimu na vyuo vikuu viwe ni jukwaa la kurithisha imani, maadili na utu wema; kwa kuwafunda vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano; tayari kujisadaka katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linajitahidi kuwafahamu vijana, kuwapokea, kuwasikiliza na kuwasindikiza katika hatua mbali mbali za safari ya maisha yao, daima Kanisa likikuza na kudumisha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” changamoto inayovaliwa njuga kwa sasa na Baba Mtakatifu Francisko.

Mababa wa Sinodi wanasema, vijana wathaminiwe na kushirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kujenga utamaduni na sanaa ya kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi; daima Kanisa likijitahidi kusoma alama za nyakati. Mazingira bora ya kifamilia, kishule na kikanisa yasaidie kujenga utamaduni wa watu kukutana kwa furaha na upendo. Wazazi na walezi wahakikishe kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu. Vijana wajengewe uwezo katika medani mbali mbali za maisha kwa kutambua kwamba, wao ndio watakaokuwa viongozi wa Kanisa na wadau katika shughuli za kisiasa, kiuchumi na kitamaduni. Vijana wafundwe kuwa mitume na wamisionari hodari wa Kanisa, ambao wako tayari kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili inayomwilishwa katika huduma, kielelezo cha imani tendaji.

Vijana watambue kwamba, Kanisa linaundwa na watu watakatifu pamoja na wadhambi wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Ulimwengu wa utandawazi, sayansi na maendeleo ya teknolojia ni fursa makini katika mchakato mzima wa uinjilishaji; kukosa na kukosea, ni sehemu ya ubinadamu, kutubu na kuongoka ni mchakato wa utakatifu wa maisha! Mabadiliko makubwa katika medani mbali mbali za maisha, yawawezeshe vijana kujiandaa kikamiliu katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kanisa kwa kusoma alama za nyakati, lianze kutoa kipaumbele cha pekee katika malezi na majiundo makini ya mihimili ya uinjilishaji, watu watakaokuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu, Injili na Kanisa, tayari kuwasaidia vijana katika maisha na utume wao!

Maboresho ya Liturujia yapewe msukumo wa pekee, ili Mungu atukuzwe na binadamu aweze kukombolewa! Tasaufi ya: haki, huruma ya huruma na upendo wa Mungu, iliwezeshe Kanisa kushughulikia kikamilifu changamoto za kashfa ya nyanyaso za kijinsia, ambazo zilimelichafua Kanisa kwa miaka ya hivi karibuni, ili kuendelea kukazia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kama sehemu muhimu ya Injili ya familia. Kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emmau, Kristo Yesu, awe ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, kwa kuona, kuamua na kutenda! Kanisa lijifunze kuthamini tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu zinazofumbatwa na waamini kutoka katika Makanisa machanga duniani.

Vyama vya kitume miongoni mwa vijana ni vyombo makini vya uinjilishaji wa marika pamoja na kutambua kwamba, useja kwa vijana, ni tunu muhimu sana katika ukuaji wao kiutu. Mapadre na watawa waendelee kuwa ni mashuhuda aminifu wa maisha na utume wao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Hii inatokana na ukweli kwamba, imani na matumaini ya waamini wengine yamepungua kutokana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ambayo imelikumba na kulitikisa Kanisa. Utakatifu wa maisha na uwepo wa dhambi ni changamoto petu katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa liendelee kusimamia haki, toba, wongofu wa ndani na msamaha, ili kuponya na kuganga madonda ya kashfa mbali mbali ndani ya Kanisa.

Sinodi:taarifa ya makundi
11 October 2018, 09:45