Tafuta

Vatican News
Kardinali Filoni anasema, vijana ni amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kardinali Filoni anasema, vijana ni amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. 

Kardinali Filoni: Vijana ni amana na utajiri wa Kanisa! Inalipa kuwekeza kwa vijana!

Lengo kuu la Sinodi ni kusaidia mchakato wa wongofu wa kimisionari unaojikita katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kusoma alama za nyakati, tayari kujibu kilio na matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya sanjari na kutangaza pamoja na kushuhudia Injili ya matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake elekezi wakati wa kufungua maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana yanayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” aliwataka Mababa wa Sinodi kuhakikisha kwamba, wanajenga sanaa na utamaduni wa kusikiliza vijana kwa makini na kuzungumza kwa ujasiri unaofumbatwa katika ukweli na uwazi. Lengo ni kusaidia mchakato wa wongofu wa kimisionari unaojikita katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kusoma alama za nyakati, tayari kujibu kilio na matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya sanjari na kutangaza pamoja na kushuhudia Injili ya matumaini kwa vijana.

Mama Kanisa anataka kuwajengea vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi inayosimikwa katika: haki, amani; ustawi, maendeleo, utu na heshima ya binadamu Katika maadhimisho ya sehemu ya kwanza, Mababa wa Sinodi wamekazia umoja na mshikamano wa Kanisa, wajibu na umuhimu wa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwasaidia vijana katika kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, kwa kuambatana na Kristo Yesu, chemchemi ya furaha ya Injili na matumaini!

Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika mahojiano maalum na Vatican News ana tumaini kwamba, Mababa wa Sinodi wataweza kutumia fursa hii kupembua kwa kina na mapana maisha na utume wa vijana wa kizazi kipya katika ulimwengu mamboleo. Ni muda muafaka wa kufanya tafiti katika ulimwengu wa vijana, ili kuwajengea vijana uwezo wa kuboresha maisha yao: kiroho, kisaikolojia na kiutu ili mwisho wa siku, waweze kukomaa na kuwajibika katika maisha na utume kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Vijana ni watu wanaopenda ukweli na uwazi; ni watu wenye bidii, ari na moyo mkuu, utajiri na amana kubwa katika maisha na utume wa Kanisa anasema Kardinali Filoni. Wadau mbali mbali wanapaswa kujiuliza swali la msingi, Je, ni ulimwengu wa namna gani wanataka kuwarithisha vijana wa kizazi kipya? Baba Mtakatifu Francisko anawataka walimwengu kuwajengea vijana uhuru unaowawajibisha: kufanya tafiti na mang’amuzi katika medani mbali mbali za maisha, tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, ili kukabiliana kwa ujasiri na changamoto za maisha katika ulimwengu mamboleo. Mababa wa Sinodi, wakitoa kipaumbele cha kwanza katika mwelekeo huu, kwa hakika, vijana wataweza kuwa na matumaini makubwa kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Umri wa ujana ni changamoto inayopaswa pia kuangaliwa, ili Kanisa liweze kutoa majibu muafaka kadiri ya umri wa vijana wenyewe. Kwani hapa anasema, Kardinali Fernando Filoni kuna watoto, vijana wanaopevuka, vijana na vijana wanaoelekea kwenye ukomavu, tayari kuanza maisha ya utu uzima. Kundi hili la mwisho, tayari linaweza kuwa na upeo mkubwa zaidi na kwamba, changamoto kubwa ni fursa za ajira na maamuzi ya wito katika maisha. Kumbe, mahitaji halali ya kila kundi la vijana yanapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma na upendo. Mahali vijana wanakotoka pia wanatofautiana kimsingi! Vijana wa mijini wanamahitaji yao makubwa pengine ikilinganishwa na vijana wanaotoka vijijini. Mahitaji ya vijana wa Bara la Afrika ni tofauti sana na mahitaji ya vijana kutoka: Ulaya, Amerika na Asia. Haya ndiyo mang’amuzi yanayoendelea kutolewa na Mababa wa Sinodi kuhusu maisha na utume wa vijana ndani na nje ya Kanisa.

Kardinali Fernando Filoni anakaza kusema, changamoto, matatizo na matamanio halali ya vijana ni shughuli pevu si tu kwa Mama Kanisa na hata katika jamii katika ujumla wake. Ulimwengu wa vijana ni changamoto changamani, kwani mwelekeo wake kwa wakati huu ni kutaka kuvunja mafungamano na familia, Kanisa na jamii. Vijana wanakabiliwa na changamoto ya kujisikia kuwa ni sehemu ya Kanisa. Hizi ni tafakari zinazoweza kuwasaidia vijana kufikia ukomavu na hatimaye, kuibua hekima na busara katika hija ya maisha yao ya kila siku! Mababa wa Sinodi sasa wameanza kuingia sehemu ya pili ya “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya Kutendea” inayozungumzia kuhusu: Kanisa: Imani na miito; mang’amuzi pamoja na kuwasindikiza vijana. Ni furaha na wajibu wa kuwasindikiza vijana katika safari yao ya imani, katika ulimwengu, maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Filoni

 

 

11 October 2018, 14:22