Cerca

Vatican News
Kanisa linaendelea kujizatiti kuwasikiliza na kuwasindikiza vijana katika hija ya maisha yao! Kanisa linaendelea kujizatiti kuwasikiliza na kuwasindikiza vijana katika hija ya maisha yao!  (Vatican Media)

Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana: Kanisa linataka kuwasikiliza na kuwasindikiza vijana!

Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema, kusikiliza ni sehemu muhimu sana ya utambulisho wa Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

 

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, kimekuwa ni kipindi cha sala, tafakari, mang’amuzi, toba na wongofu wa kimisionari. Mababa wa Sinodi wamejitahidi kujenga sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza vijana, sasa ni wakati wa kurejea katika uhalisia wa maisha na utume wa vijana, tayari kumwilisha, hayo yaliyopembuliwa na Mababa wa Sinodi, ili kuwadhihirishia vijana kwamba, Kanisa linawapenda na kuwathamini na linataka kuwasaidia kutekeleza ndoto na matamanio yao halali!

Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema, kusikiliza ni sehemu muhimu sana ya utambulisho wa Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia umesheheni picha na matangazo ya kila aina, yanayowavuruga vijana, kiasi hata cha kuchafua ndoto za maisha yao kwa siku za usoni! Kisa ni mitandao ya kijamii! Wanasiasa nao wanaendelea kuwavuta vijana, kwa mbwembwe na matarajio ambayo wakati mwingine yanabakia katika ombwe, kwani yanakosa ukweli na roho thabiti katika utekelezaji wake. Takwimu zilizotolewa hivi karibuni nchini Italia zinaonesha kwamba, vijana wa kizazi hiki wengi wao wanaishi katika msongo wa mawazo kutokana na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa, kiasi hata cha kukosa matumaini ya leo na kesho iliyo bora! Ni kundi linaloelemewa na umaskini wa hali na kipato!

Ni vijana wanaofanana na watoto yatima, lakini wazazi wao bado wanaendelea kuishi. Hawa ni vijana ambao wamekosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha, ni sawa na “daladala iliyokatika usukani”. Kwa hakika, vijana wengi wananyanyasika kijamii, kwani takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 30% ya vijana wenye umri kati ya miaka 18-29 hawana fursa ya ajira nchini Italia, kiasi kwamba, hatima ya maisha yao kwa siku za usoni iko mashakani! Lakini pamoja na changamoto zote hizi, kuna vijana wanaothubutu kufanya maamuzi magumu katika maisha kwa kuamua kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya familia, licha ya changamoto wanazokutana nazo katika safari ya maisha! Kuna wasichana wanaoamua kuwa kweli ni tabernakulo ya Injili ya uhai kwa kukataa kishawishi cha utamaduni wa kifo, kiasi kwamba, hawa kweli ni mifano bora ya kuigwa na vijana wenzao!

Kardinali Bassetti anakaza kusema, Sinodi ya vijana imeangalia kwa kina na mapana matatizo, changamoto, fursa na matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya, tayari kuyapatia majibu mintarafu: mwanga wa Injili, Mapokeo hai na Mafundisho ya Kanisa, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Mama na mwalimu, kamwe hawezi kusahau mateso na matamanio halali ya vijana wake. Mama Kanisa anataka kuwaambia vijana, kwamba, “ I Care” yaani “Ninawathamini” na kwamba, vijana ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa na kwamba, ustawi, maendeleo na mafao yao kwa sasa na kwa siku za usoni ni kati ya vipaumbele vya Mama Kanisa ili kuwajengea tena vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi!

Kanisa linataka kuwasaidia vijana: kukua na kukomaa mintarafu tunu msingi za Kiinjili na utu wema; kwa kuhakikisha kwamba: wanapata malezi, makuzi endelevu na fungamani, yanayomwambata mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linataka kuendelea kujikita katika kanuni, sheria, taratibu na maadili ya kazi ili kudumisha: nidhamu, weledi, uadilifu na uwajibikaji kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha ya vijana kwa njia ya kazi na kama sehemu ya mapambano dhidi ya: umaskini, rushwa na ufisadi, mambo ambayo yanawatumbukiza vijana wengi katika majanga ya maisha!

Kardinali Bassetti katika barua yake anasema, hii ni changamoto ya kukuza na kudumisha uzalendo kwa kuwashirikisha vijana katika medani mbali mbali za maisha; daima haki msingi, utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi vikipewa kipaumbele cha kwanza! Kwa upande wao, vijana wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuchangia: vipaji na karama zao tayari kuyatakatifuza malimwengu, kwa kujenga uhusiano na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu, chemchemi ya maisha mapya na Injili ya matumaini kwa vijana!

Vijana wanapaswa kuwa na ari na mwamko wa kuweza kuwa na ndoto katika maisha; wapewe vigezo vitakavyowasaidia kufikiri na kutenda kwa makini; daima wakithamini rasilimali muda kwani “ujana ni mali na fainali ni uzeeni”. Vijana wawe na jeuri ya kupambana na changamoto za maisha kwa njia ya mwanga wa Injili, daima wakijikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni na kamwe wasiwe kama bendera inayofuata upepo!

Kardinali Bassetti

 

 

27 October 2018, 10:17