Tafuta

Vatican News
Rais Kim Jong-un wa Korea ya Kaskazini ameonesha nia ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Korea ya Kaskazini Rais Kim Jong-un wa Korea ya Kaskazini ameonesha nia ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Korea ya Kaskazini  (ANSA)

Rais Kim Jong-un ameonesha nia ya kumwalika Papa Francisko nchini Korea ya Kaskazini

Familia ya Mungu nchini Korea imefurahishwa sana na ziara hii ya kikazi ambayo itamwezesha Rais Moon Jae-in wa Korea ya Kusini kuwasilisha mwaliko kutoka kwa Rais Kim Jong-un, wa Korea ya Kaskazini, anayemwalika Baba Mtakatifu Francisko kutembelea nchini mwake. Rais Moon Jae-in wa Korea ya Kusini atakuwa nchini Italia na Vatican kati ya tarehe 17- 18 Oktoba 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 18 Oktoba 2018 anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Rais Moon Jae-in wa Korea ya Kusini. Tukio hili la kihistoria litatanguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kuombea amani nchini Korea, Jumatano tarehe 18 Oktoba 2018. Ibada hii itahudhuriwa pia na Rais Moon Jae-in wa Korea ya Kusini. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoka Korea wanajiandaa kikamilifu kwa ajili ya kuadhimisha matukio haya, kama kielelezo cha upendo na heshima ya Baba Mtakatifu Francisko kwa familia ya Mungu nchini Korea.

Kwa upande wake, Kardinali Andrew Yeom Soo-yung, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Seol, Korea ya Kusini ambaye pia ni Msimamizi wa kitume wa Jimbo kuu la Pyongyang, amefurahishwa sana na ziara hii ya kikazi ambayo itamwezesha Rais Moon Jae-in wa Korea ya Kusini kuwasilisha mwaliko kutoka kwa Rais Kim Jong-un, wa Korea ya Kaskazini, anayemwalika Baba Mtakatifu Francisko kutembelea nchini mwake. Rais Moon Jae-in wa Korea ya Kusini atakuwa nchini Italia na Vatican kati ya tarehe 17- 18 Oktoba 2018.

Kardinali Andrew Yeom Soo-yung anapenda kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekuwa mstari wa mbele kwa ajili ya kuombea amani, ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Korea na kwamba, hata wao wanamkumbuka kila siku katika sala zao, ili Mwenyezi Mungu aendelee kumlinda na kumtegemeza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni matumaini ya Kardinali Andrew kwamba, jitihada zote hizi zinazoendelea kutekelezwa na Jumuiya ya Kimataifa zitaweza kuzaa matunda ya haki, amani na maridhiano.

Kama Msimami wa kitume Jimbo kuu la Pyongyang, Kardinali Andrew anasali akiwa na matumaini kwamba, iko siku moja, Kanisa litaweza tena kutuma mapadre, watawa na makatekista huko Korea ya Kaskazini, kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa ili Mwenyezi Mungu aabudiwe na binadamu atakatifuzwe na kupewa wokovu na maisha ya uzima wa milele. Tangu mwaka 1948, Kanisa nchini Korea ya Kaskazini, limenyamazishwa, kwa lengo la kutaka kufutilia mbali mbegu ya imani iliyopanda nchini humo.

Hadi kufikia mwaka 1950 nchini Korea ya Kaskazini kulikuwa na waamini wapatao hamsini na tano elfu na kulikuwa na Makanisa hamsini na saba, yaliyokuwa yamesheheni wamisionari pamoja na huduma ya elimu na afya; kama sehemu ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Leo, nchini Korea ya Kaskazini, hakuna hata askofu, mapadre au watawa. Cheche za mabadiliko zilianza kujionesha kunako mwaka 1989, Serikali ilipoanza kutambua baadhi ya taasisi zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki nchini humo. Kanisa lina uhakika kwamba, kuna umati mkubwa wa Wakristo wanaokiri na kuungama imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kificho huko Korea ya Kaskazini, lakini iko siku wataibuka!

Korea ya Kaskazini

 

13 October 2018, 11:19