Tafuta

Vatican News
Kardinali Peter Turkson, anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano kujenga utamaduni wa amani duniani! Kardinali Peter Turkson, anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano kujenga utamaduni wa amani duniani!  (ANSA)

Wadau wa Tasnia ya mawasiliano, dumisheni Injili ya amani na utulivu duniani!

Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa ufupi, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu; ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa ufupi, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani inatishiwa sana na mashindano; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani! Dhamana hii inaweza kutekelezwa vyema zaidi ikiwa kama waandishi wa habari watajizatiti zaidi katika uandishi unaofumbata amani.

Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la maendeleo fungamani, kwa washiriki wa mkutano wa kimataifa juu ya “Uandishi wa amani” ulioandaliwa Baraza la Kipapa la Mawasiliano pamoja Baraza la Kipapa la Maendeleo fungamani. Mkutano huu umehudhuria na wajumbe wa Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki, SIGNIS pamoja na wadau mbali mbali kutoka katika tasnia ya mawasiliano ya jamii ndani ya Kanisa. Kutokana na athari za vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, waandishi wa habari wanayo dhamana kubwa kuhakikisha kwamba, wanakuwa makini katika kuandika habari zao, ili kulinda na kudumisha Injili ya amani duniani.

Mtakatifu Paulo VI aliwahi kusema, amani ni jina jipya la maendeleo endelevu ya binadamu, changamoto inayoendelea kuvaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake. Jamii inayofumbatwa katika utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, amani na maendeleo ni mambo msingi anasema, Kardinali Peter Turkson. Amani ya kweli inajikita katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani kwa binadamu, kama alivyowahi kusema, Mtakatifu Paulo VI wakati akihutubia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1965.

Dhana ya vita, kinzani na mipasuko inapata chanzo chake katika moyo wa binadamu, kumbe, kwanza kabisa mwanadamu haja budi kujikita katika mchakato wa kutafuta amani moyoni mwake, ili hatimaye, aweze kuwashirikisha pia jirani zake.Amani ya kweli ipate chimbuko katika undani wa mwanadamu. Ni kutokana na changamoto ya kutoweka kwa amani duniani, ndiyo maana hivi karibuni, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antònio Guterres amefungua ukurasa mpya wa amani katika ajenda za Umoja wa Mataifa, ili udhibiti wa silaha za maangamizi uwe ni kati ya vipaumbele vya Umoja wa Mataifa kwa wakati huu.

Mashindano ya utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha ni tishio kubwa kwa Injili ya amani duniani na daima waathirika wakuu ni nchi maskini zaidi duniani. Amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa unapaswa kujikita katika: haki, maendeleo fungamani ya binadamu, haki msingi za binadamu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na ushiriki mkamilifu wa wananchi katika maisha ya hadhara; kwa kujenga na kudumisha miundo mbinu inayohamasisha amani na utulivu pamoja na kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kuboresha huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya jamii sanjari na kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano na mshikamano wa kweli.

Kardinali Peter Turkson anawataka waandishi wa habari kutafuta vyanzo halisi vya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, ili kuanzisha mchakato utakaoweza kuganga na kuponya tatizo hili ambalo ni hatari kwa maendeleo ya wengi. Viongozi wenye dhamana katika kulinda na kudumisha amani wanayo dhamana nyeti sana katika Jumuiya ya Kimataifa. Waandishi wa habari wanatakiwa kuzama zaidi, ili kuibua ukweli kwa ajili ya: mafao, ustawi na maendeleo ya wengi; kwa kujikita katika haki na ukweli, kwani matukio makubwa ya maisha ya binadamu yanachagizwa na maisha ya familia ya Mungu kila siku ya maisha yao!

Injili ya amani
31 October 2018, 15:29